Juma Kaseja |
KIPA Ally Mustapha ‘Barthez’ alimkimbia Juma Kaseja na kutimkia Yanga kutokana na kukosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha Simba na sasa Kaseja amerejea Yanga kwa mara nyingine.
Kaseja ambaye aliachwa na Simba baada ya kumaliza mkataba wake amesaini Yanga kwa kitita cha Sh40 milioni.
Barthez alikuwa kipa namba mbili wa Simba wakati ikinolewa na kocha aliyetupiwa virago, Mserbia Milovan Cirkovic.
Kaseja alisimama lango la Simba kwenye mechi zote za ligi kwa misimu miwili mfululizo pasipo kumwachia Barthez kudaka angalau mechi moja zikiwemo za kirafiki.
Benchi lilimkimbizia Barthez Yanga ambako sasa Kaseja amemfuata huko huko.
Mbali na Barthez kipa mwingine aliyekimbia benchi la Simba ni Deo Munishi ‘Dida’ ambaye kwenye mechi nne za mwisho kwenye ligi msimu huu alianza kuonyesha kiwango kizuri huku akiwa hajaruhusu bao hata moja kutinga kwenye nyavu zake lakini kuingia kwa Kaseja Yanga kunamuweka pabaya kupata namba.
Yanga kwa mara ya kwanza inasajili makipa watatu ambao wote waliwahi kuchezea Simba na tena walikuwa wote.
Dida na Barthez wamegoma kuzungumza lolote kuhusu usajili wa Kaseja ingawa habari za uhakika zinadai kwamba hawakutarajia hali hiyo kutokea.
Wakati anasajiliwa Barthez mashabiki wa Yanga walikuwa wakipaza sauti kwenye mechi za Simba msimu 2010/11 wakimtaka Barthez kumkimbia Juma Kaseja na kujiunga na Yanga ambayo ilikuwa na makipa Said Mohammed na Mghana Yaw Berko ambaye alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya bega mara kwa mara.
Barthez alijiunga Yanga mwaka jana na kuipa ubingwa wa ligi ukiwa msimu wake wa kwanza ingawa msimu wake wa pili umekuwa mbaya baada ya kupoteza namba kwenye kikosi cha kwanza tangu Yanga ilipotoka sare ya mabao 3-3, Oktoba 20.
Habari za ndani zinadai awali mwaka jana benchi la ufundi la Yanga lilimpa Barthez nafasi ya kuchagua kipa atakayefanya naye kazi lakini hakumtaka Kaseja, alimchagua Dida na ndiye aliyesajiliwa.
Kocha wa Yanga, Ernest Brandts amemtumia Dida kwenye mechi nne za mwisho kwenye ligi mzunguko wa kwanza dhidi ya Rhino Rangers, Mgambo JKT, JKT Ruvu na Oljoro JKT.
No comments:
Post a Comment