MADRD, HISPANIA
TAJIRI namba moja duniani, Bill Gates, wa Marekani naye ameamua kuuvamia mchezo wa mpira wa miguu baada ya matajiri wengi kutoka nchi za Marekani, Russia na wa barani Asia kuwekeza katika mchezo huo.
Gates yupo katika mazungumzo na wababe wa soka la Ulaya, Real Madrid, kwa ajili ya kununua haki ya jina la uwanja wao, Santiago Bernabeu. Kama mazungumzo yakienda sawa, kuna kila sababu uwanja huo ukajulikana kwa jina la Santiago Bernabeu Microsoft.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, yupo katika mazungumzo mazuri na Gates na kuna kila dalili watu hao maarufu duniani wakaibadili historia ya uwanja huo wenye kumbukumbu nyingi katika soka.
Endapo Real Madrid itakubaliana na dili hilo, itajikuta ikiondoka na kitita cha dola 10 milioni kwa mwaka na Perez anataka kupunguza madeni mengi yanayoikabili timu hiyo.
Tayari Real Madrid na Gates wamekuwa katika uhusiano mzuri wa muda mrefu ambapo Gates amekuwa akitoa sapoti katika mfuko maalumu wa Real Madrid ambao umelenga kutoa misaada kwa nchi nyingi maskini hususan katika nyanja za elimu na michezo hasa nchi za Latini Amerika. Bill Gates amekuwa akiendelea kutajwa na Jarida la Forbes kuwa ni mtu tajiri duniani na kwa kipindi kirefu kati ya mwaka 1995 hadi mwaka 2009, ukiondoa mwaka 2008 ambapo alitajawa kushika nafasi ya tatu, Gates amekuwa mtu tajiri zaidi duniani.
Mwaka 2011 alitajwa kuwa ndiye Mmarekani tajiri zaidi. Lakini kwa mujibu wa mtandao wa Bloomberg Billionaires List, Gates ametajwa kuwa mtu tajiri zaidi duniani mwaka 2013. Kuwekeza kwake kwa njia moja au nyingine kunajaribu kuiokoa Real Madrid ambayo katika miaka ya karibuni imekuwa na madeni mengi makubwa.
Wakati hivi karibuni Perez alidai kwamba klabu hiyo ina deni la Euro 90 tu ambalo haliwasumbui kichwa, mtaalamu wa masuala ya fedha ya soka nchini Hispania, Guy de Liebana na kundi la mashabiki wa timu hiyo, walidai kwamba Madrid ina deni linalozidi Euro 500 milioni.
Utata huo wa deni pia umezidi baada ya Mkurugenzi wa Ufundi wa zamani wa Madrid, Jorge Valdano, kudai kwamba klabu hiyo ililazimika kumuuza kiungo wake mahiri, Mesut Ozil, kwenda Arsenal kutokana na madeni mengi yanayoikabili pamoja na manunuzi ya winga wa Tottenham, Gareth Bale.
Tayari klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya zimeanza kuuza haki za majina ya viwanja vyao kwa kampuni mbalimbali kwa ajili ya kujiongezea vipato licha ya mashabiki wa soka kulalamika kwamba klabu zinaweka mbele tamaa za pesa kuliko tamaduni za klabu.
Wakati Arsenal ikiwa imebadilisha jina lake la Highbury kwenda Emirates mara baada ya kudhaminiwa na Shirika la Ndege la Emirates ambalo linatamba kiuchumi kwa sasa, Manchester City imebadili jina la uwanja wake kutoka City of Manchester na kuwa Etihad.
Etihad ni Shirika la Ndege la Falme za Kiarabu na kwa sasa ndio wadhamini wa Manchester City ambayo inamilikiwa na Waarabu kutoka Falme za Kiarabu.
Uwanja wa Allianz Arena ambao unatumiwa na klabu mbili za Bayern Munich na 1860 Munich, pia unatumia jina la Allianz kutokana na kampuni kubwa inayoshughulika na masuala ya fedha ya Allianz kununua haki za jina la uwanja huo kwa kipindi cha miaka 30.
Desemba Mosi, 2005 Uwanja wa Westfalenstadion wa Borussia Dortmund, ulibadilishwa jina na kuitwa Signal Iduna Park. Dortmund ilipokea kiasi cha Euro 20 milioni kutokana na kubadilishwa kwa umiliki. Signal Iduna ni kundi la kampuni ya masuala ya Bima. Viwanja vingine ni Veltins Arena na uwanja wa Zenit uitwao, Gazprom Arena.
Inasemekana pia Shirika la Ndege la Qatar, limekuwa likiunyatia Uwanja wa Nou Camp wa Barcelona kwa ajili ya kuubadili jina. Hii ni kufuatia Qatar kufanikiwa kupata udhamini katika jezi za timu hiyo maarufu kwa sasa duniani.
Awali, jezi ya Barcelona ilikuwa haina tangazo lolote la biashara katika historia yake ya soka ambapo kuna wakati iliweka nembo ya Unicef ikiwa ni kama msaada wao kwa watoto.
No comments:
Post a Comment