Barthez |
INGAWA hajaomba lakini kamati ya usajili wa Yanga imesisitiza haitamtoa wala haina mpango wa kumtoa kwa mkopo kipa, Ally Mustapha ‘Barthez’, baada ya ujio wa Juma Kaseja.
Barthez alisajiliwa Yanga misimu miwili iliyopita akitokea Simba katika usajili ambao uliaminika kumkimbia Kaseja aliyekuwa akitawala lango la wana Msimbazi wakati huo.
Lakini sasa Kaseja ametua Yanga na Barthez pamoja na kipa mwingine, Deo Munishi ‘Dida’, wamesisitiza kwamba hawahofii uamuzi wa uongozi wa klabu hiyo kumsajili Kaseja waliyemkimbia Simba.
Wachezaji hao wamesisitiza kwamba wanamheshimu mchezaji huyo kama mchezaji mwingine yeyote na benchi la ufundi ndilo litakaloamua hatma ya nani asimame langoni.
Barthez aliiambia Mwanaspoti jijini Dar es Salaam kuwa anamkaribisha Kaseja Yanga.
“Kuhusu nafasi ya kucheza, nafikiri hilo linabaki kwa kocha, nadhani yeye ndiye mwenye mamlaka ya kipa gani atakaa golini kulingana na mchezo husika, hilo haliwezi kunitisha,” alisema Barthez.
“Suala la msingi hapa ni kuongeza juhudi katika mazoezi kwa kuwa ushindani wa kucheza utakuwa umeongeza tofauti na awali.”
Kwa upande wake, Dida, alisema: “Ni jambo zuri kufanya kazi kwa mara nyingine tena na Kaseja, niliwahi kuwa naye Simba kwa maana hiyo nafurahi kubahatika kuwa naye tena, naamini ushindani utakuwa umeongezeka ingawa suala la kucheza linabaki kuwa siri ya mwalimu.
“Hata nilipojiunga na Yanga nilimkuta Barthez, lakini wakati wangu ulifika na kucheza, hatupaswi kuogopa ujio wake bali kushirikiana kwa ajili ya malengo ya timu.”
Kocha wa Makipa wa Yanga, Razack Siwa, alipotakiwa kumzungumzia Kaseja, aligoma wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Yanga, Abdallah Bin Kleb, akisema pamoja na kumsajili kipa huyo hawana mpango wa kumtoa kwa mkopo Barthez.
“Barthez ataendelea kuwapo Yanga pamoja na makipa wengine Dida (Munishi) na Kaseja (Juma), hatuna sababu ya msingi kumtoa kwa mkopo,” alisema Bin Kleb.
Yanga imemsajili Kaseja kwa mara nyingine baada ya kufanya hivyo mwaka 2008 kabla ya hajarudi Simba msimu uliofuata alikocheza hadi mwishoni mwa msimu uliopita walipomuacha
No comments:
Post a Comment