Wednesday, 9 October 2013

SUNDERLAND WAPATA KOCHA MPYA


Kocha mpya wa Sunderland Gus Poyet
Gus Poyet ameteuliwa kuwa Kocha mpya ya klabu ya soka ya Sunderland inayoshiriki katika ligi kuu ya soka nchini Uingereza.

Poyet ambaye pia amewahi kuwa Kocha wa klabu ya Brighton ya Uingereza inayoshiriki katika daraja la kwanza atakuwa Mkufunzi wa Sunderland kwa miaka miwili kwa mujibu wa mkataba aliotia saini.
Uongozi wa Sunderland ulimfuta kazi kocha Paolo Di Canio mwezi Septemba baada ya matokeo mabaya baada ya mechi 13 kama mkufunzi katika klabu hiyo.
Kocha huyo mpya mwenye umri wa miaka 45, atasaidiwa na manaibu wake Mauricio Taricco na Charlie Oatway wote aliofanya nao kazi wakati akiwa kocha katika klabu ya Brighton.
Poyeta anakuwa Mkufunzi wa Sunderland na kuingia katika orodha ya makocha sita ambao wamefunza katika klabu hiyo ya Stadium of Light ndani ya miaka mitano.
Mwenyekiti wa klabu hiyo Ellis Short amesema kuwa Poyet amedhihirisha kuwa ana uzoefu wa kutosha na yuko tayari kujitolea kuisaidia Sunderland kuimarisha kiwango chake cha soka katika ligi ya Uingereza.
Kocha wa mpito Kevin Ball ambaye alikuwa ameomba kupewa nafasi ya kuendelea kuifunza timu hiyo hakuwa na bahati baada ya kufungwa na Manchester United mabao 2 kwa 1 mwishoni mwa juma lililopita.
Kabla ya kuwa kocha Poyet alikuwa mchezaji wa klabu ya Cheslea na Tottenham Hotspurs zote za Uingereza na kuichezea timu ya taifa ya Uruguay mara 26.

No comments:

Post a Comment