Ronaldo De Lima |
RIO DE JANEIRO, BRAZIL
HAJAWAHI kukosea ndani na nje ya uwanja. Baada ya penzi lake la mkewe, Bia Anthony, kufa Desemba mwaka jana, mkongwe wa soka nchini Brazil, Ronaldo de Lima, ameibuka kivingine kabisa.
Ronaldo ameanzisha uhusiano wa kimapenzi na DJ mrembo, Paula Morais, ambapo penzi lao linaonekana kushika chati nchini Brazil kama ilivyo ada kwa Ronaldo ambaye ni maarufu nchini humo.
Staa huyo wa zamani wa Barcelona, Inter Milan, Real Madrid na AC Milan, ameachana na mkewe aliyedumu naye kwa miaka saba na sasa inaonekana amezama katika penzi la Paula kiasi cha kufuatana naye kila mahali.
Penzi lao lilianza kudhihirika katika tamasha la Samba nchini Brazil hivi karibuni ambapo wawili hao walijitokeza hadharani na kuvutia umati wa mashabiki.
Kama vile haitoshi, Paula alitoa kiashirio kwamba yuko katika penzi zito na Ronaldo na kwamba anaiangalia afya ya nyota huyo kwa karibu hasa baada ya staa huyo kupunguza kilo 17 akifuata mpangilio wa vyakula kwa mujibu wa kituo kimoja cha televisheni nchini Brazil.
Paula alituma picha ya Ronaldo akiwa ameshikilia kikaangio kilichokuwa na mayai ya kukaanga huku akiandika ‘Jiko ni sehemu ya Mwanamume, nakupenda.’
Kama vile haitoshi, siku za karibuni Ronaldo alisafiri na Paula mpaka nchini Hispania kwa ajili ya kula raha katika miji mbalimbali nchini humo. Walionekana wakiwa katika fukwe za maraha za Ibiza wakiponda starehe.
Pia walionekana wameshikana mikono katika Jiji la Madrid wakiwa katika maduka ya Chanel & Hermes wakifanya manunuzi huku wakipiga stori za mahaba.
Kama inavyoonekana pichani, Ronaldo pia amekuwa akiwa sambamba na Paula hadi katika sehemu yake ya kazi huku akivamia katika chumba cha MaDJ ambacho ni maalumu kwa wapiga muziki peke yao.
Huu ni mwendelezo wa Ronaldo katika harakati zake za kupenda vimwana ambapo penzi lake la awali na mkewe Bia, liliingia katika dosari baada ya Ronaldo kukumbwa na kashfa ya kuingia chumbani na wanaume wanne waliojibadili jinsia. Hata hivyo ndoa yao baadaye iliendelea baada ya Ronaldo kuomba msamaha.
Mtoto wao wa kwanza, Maria Sophia, alizaliwa Desemba 24, 2008. Mtoto wa pili, Maria Beatriz alizaliwa Aprili, 6 2010 na Mtoto wao wa tatu aliyepewa jina la Maria Alice, alizaliwa miaka 10 kamili tangu Ronaldo apate mtoto wake wa kwanza wa kiume.
No comments:
Post a Comment