Thursday, 31 October 2013

'BABU SEYA AFUTIWE HUKUMU

Juni 25, 2004 Mahakama ya Kisutu iliwatia hatiani Babu Seya na wanaye hao Papii Nguza ‘Papii Kocha’,
Nguza Mbangu na Francis Nguza kwa makosa ya kubaka na kulawiti watoto

MWANAMUZIKI, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na wanaye watatu, wameiomba Mahakama ya Rufaa kuufuta ushahidi uliowatia hatiani na hivyo kuhukumiwa kifungo cha maisha jela katika kesi ya kulawiti watoto, wakisema ushahidi huo una makosa ya kisheria yaliyofanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu.
Ombi la familia hiyo ya wanamuziki liliwasilishwa jana Jumatano kupitia wakili, Mabere Marando, aliyedai kuwa mahakama iliteleza  katika kutoa hukumu iliyowatia hatiani wateja wake na kwamba kuteleza huko kunaonekana waziwazi kwa dosari za kisheria.
Akiwasilisha ombi hilo kwa takribani saa mbili mbele ya jopo la majaji watatu; Nathalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk pamoja na Salum Massati, Marando alisema wateja wake wanapaswa kuachiwa huru.
Akifafanua Marando alisema: “Ushahidi wa watoto hao ulichukuliwa bila ya kufuatwa kwa taratibu za uchukuaji wa ushahidi wa mtoto, ndio maana unapaswa kufutwa.
“Katika hukumu yenu mlikubaliana na sisi kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kupokea ushahidi wa watoto, ila mlisema hilo si hoja kwani kuna ushahidi unaounga mkono mkauona ushahidi huo ni bora.
“Mtoto anapotoa ushahidi licha ya tahadhari, ana uwezo wa kutambua zuri na baya, hivyo ni lazima  ushahidi wake uwekwe  kwenye kumbukumbu na kwamba usipoonekana ushahidi wote ni batili na uondolewe.
“Tunaomba ushahidi wa wale watoto ufutwe, uondolewe na washtakiwa waachiwe huru.”
Aliendelea: “Kwenye sheria ya ushahidi, kama tukio limetokea na ushahidi unaonyesha kuna mtu anayetajwa kuliona tukio, ili kutenda haki upande wa mashtaka unapaswa kumwita mtu huyo mahakamani.
“Mtu yeyote anayeacha kumpeleka mahakamani shahidi huyo kwa makusudi basi mahakama itambue kuwa ameacha kwa sababu angempeleka angeharibu kesi yake na hivyo ndiyo ilivyokuwa kwenye kesi hii.
“Kwenye hukumu mlidai watoto walipokuwa wanaingia nyumbani kwa Nguza walikuwa wanatokea katika duka la Mangi na kwamba yeye alikuwa anajua yote yaliyokuwa yanafanyika pamoja na Zizeni, kwa nini upande wa mashtaka haukuwaita mahakamani?”
Marando aliendelea kuilalamikia hukumu hiyo mashahidi wa utetezi walisema wapo watu wanaoishi katika nyumba ya Nguza akiwamo mchumba ama mke wake, mama yake pamoja na wapiga muziki wa bendi yake, hivyo watoto hao wasingeweza kuingia humo ndani bila ya kuonekana.
Alisisitiza mahakama hiyo iipitie upya hukumu, kurekebisha makosa ya kiutelezi na ifute kutiwa hatiani kwa wateja wake.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Jackson Mlaki, alipinga hoja za Marando kwa madai kuwa hazina usahihi kwa mujibu wa sheria.
Baada ya kuzisikiliza pande zote, Jaji Kimario, alisema mahakama inaliahirisha shauri hilo mpaka hapo pande zote zitakapotaarifiwa.
Juni 25, 2004 Mahakama ya Kisutu iliwatia hatiani Babu Seya na wanaye hao Papii Nguza ‘Papii Kocha’, Nguza Mbangu na Francis Nguza kwa makosa ya kubaka na kulawiti watoto.
Walidaiwa kutenda makosa 10 ya kubaka watoto wenye umri kati ya miaka sita na minane na makosa mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri huo. Walidaiwa kufanya makosa hayo kati ya Aprili na Oktoba, 2003 katika eneo la Sinza kwa Remmy, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment