Mashindano ya magongo |
Mashindano ya magongo kwa mataifa ya Afrika yaliyopangiwa kuanza Alhamisi wiki hii mjini Nairobi huenda yakaahirishwa kutokana na mkasa wa jumba la Westgate lililovamiwa na magaida wa Al Shabaab, na zaidi ya watu sitini kuuawa..
Mwenyekiti wa chama cha mchezo wa magongo cha Kenya Nashon Randiak anasema shirikisho la kimataifa,FIH, lina wasiwasi kuhusu usalama wa wachezaji mjini Nairobi baada ya magaidi wa Al Shabaab kulivamia jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi.
Licha ya Randiak kuwaeleza kwamba hali sasa ni shwari baada ya magaidi wote kuuwa na wanajeshi wa Kenya shirikisho la kimataifa limesema linataka mkuu wa polisi nchini Kenya kuwahakikisha usalama wa wachezaji.
Randiak ameshangazwa na msimamo huo akisema mashambulizi ya magaidi hutokea kote duniani hivyo anashangaa ni kwanini hili la Kenya linachukuliwa ni kama la kipekee..
Mataifa yanayotarajiwa kushiriki kwa wanaume ni Kenya, Ghana na Afrika Kusini na kwa wanawake ni Kenya, Tanzania,Ghana na Afrika Kusini. Timu ya Tanzania ikiongozwa na katibu wa chama cha magongo mkoa wa Dar es salaam Mnonda Magani tayari imeshawasili mjini Nairobi.
Timu ambazo zimejiondoa kwa sababu mbali mbali na sio hiyo ya Westgate ni pamoja na Nigeria, Namibia, Misri na Ushelisheli.
No comments:
Post a Comment