Wayne Rooney ameonekana mwenye furaha akiwa mazoezini na wachezaji wenzake
Rooney akijifua kujiandaa kuwakabili Bayern kesho
Wayne Rooney amewapa matumaini makubwa Manchester United kuelekea katika mchezo wa pili wa robo fainali kesho usiku, ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Bayern Munich baada ya kufanya mazoezi leo hii katika dimba la Allianz Arena.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rooney alishindwa kuitumikia Man United ikishinda mabao 4-0 dhidi ya Newcastle kwasababu ya majeruhi ya mguu.
Katika mazoezi ya leo, Ryan Giggs alishiriki baada ya kuwakosa Newcastle, lakini Marouane Fellaini, aliyetolewa nje katika dimba la St James' Park kufuatia kuumia, pamoja na Rafael hawakushiriki.
Rooney ameonekana kutougulia maumivu katika mazoezi ya leo kwasababu alionesha juhudi kubwa.
Awali Kocha wa Man United, David Moyes alisema Rooney alikuwa hatarini kuukosa mchezo wa kesho baada ya kuumia katika mechi ya sare ya 1-1 Old Trafford wiki iliyopita, lakini kwasasa inaonekana kutoathirika tena.
Hata hivyo, nyota huyo mwenye miaka 28 atacheza mechi hiyo kubwa zaidi kwa United msimu huu akitumia dawa za kuua maumivu.
Na kocha wa Bayern Pep Guardiola kwa upande wake hakuwa na wasiwasi kuwa Rooney ataikosa mechi ya kesho.
Alisema: 'Rooney anakwenda kucheza kwa asilimia 100. Atacheza, kama mtu anabisha naahidi kumpa zawadi kubwa endapo hatacheza"
Guardiola alimuelezea Rooney kuwa ni mmoja kati ya wachezaji wakubwa aliowaona katika maisha yake ya soka.
Man United baada ya kuonesha kiwango kizuri katika mchezo wa kwanza, wanaonekana kuwa na imani ya kufanya kazi vizuri na kusonga mbele dhidi ya mabingwa hao watetezi
No comments:
Post a Comment