STRAIKA wa Mgambo JKT, Mohamed Neto amedai kuwa kiungo wa Yanga, Hassan Dilunga alimpa refarii taarifa za uongo dhidi yake kwamba alikuwa ameficha kitu kinachodhaniwa kuwa ni hirizi kwenye sehemu zake za siri kitu ambacho si kweli.
Lakini mwamuzi huyo msomi, Alex Mahagi ameibuka na kuweka wazi usahihi huku akisisitiza kwamba madai ya mchezaji huyo si ya kweli na kwamba alikuwa na kitu chenye ncha kali.
Mahagi alisema: “Haikuwa kama ambavyo watu wanavyosema kwamba ni vitu vingine vya kishirikina na wala sikutaka kuingiza mkono katika sehemu zake za siri, nilimlazimisha kutoa alichonacho ili niweze kujiridhisha.”
Mchezaji naye akajibu; “Refa alitaka kuingiza mkono kwenye sehemu zangu za siri ili kuthibitisha kama ni kweli, mimi nikagoma.” Neto alionyeshwa kadi mbili za njano baada ya kuzozana na refa kuhusiana na suala hilo kwenye mchezo kati ya Yanga na Mgambo JKT hapo juzi Jumapili mjini Tanga wenyeji waliposhinda mabao 2-1.
“Nilikuwa napandisha soksi kisha nikaanza kuchomekea jezi yangu, sifahamu Dilunga aliona nini ndio akamwita refa na kumwambia kuwa nimeficha hirizi kwenye nguo zangu za ndani kitu ambacho si kweli kwani zile zilikuwa ni hisia zake tu.
“Mzozo ndipo ulipoanzia kwani refa alitaka kuingiza mkono kwenye sehemu zangu za siri ili kuthibitisha kama ni kweli, mimi nikagoma kisha akanionyesha kadi ya njano. Refa alisisitiza kunikagua ila nikagoma kwani pale palikuwa ni uwanjani hivyo nikamfunulia ili aangalie, yeye aligoma na kunipa kadi ya pili ya njano ambayo ilizaa nyekundu,” anasema Neto ambaye alishuhudia sehemu iliyosalia ya mchezo huo akiwa jukwaani baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu.
Mwamuzi mwenyewe ajitetea
Mwamuzi Alex Mahagi, ameshangazwa na taarifa zisizokuwa na usahihi juu ya tukio la kumtoa kwa kadi nyekundu Mohammed Neto, ambapo amesimulia kila kitu juu ya tukio hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti Mahagi alisema mchezaji huyo aliingia uwanjani na silaha ambapo mara baada ya kuruka juu kuwania mpira na mmoja wa wachezaji wa Yanga alibainika kuwa na kitu chenye ncha kali kilichomchoma mchezaji huyo wa Yanga.
Mahagi alisema: “Ukweli ni kwamba, haikuwa kama ambavyo watu wanavyodai kwamba ni ushirikina, wala sikutaka kuingiza mkono katika sehemu zake za siri, nilimlazimisha kutoa alichonacho ili nijiridhishe juu ya alichoweka ndani ya bukta ambacho ukiacha wachezaji wa Yanga hata mimi kilinichoma.”
“Nilipoona anagoma kwa kuwa tayari nilishakuwa nimempa kadi ya kwanza ya njano nilijua kwamba nitakapompa ya pili nitakuwa namtoa kwa kadi nyekundu, nilimwita nahodha wake nikamwambia amwambie mchezaji wake atoe alichonacho,”alifafanua Mahagi jana Jumatatu jijini Dar es Salaam.
Alisema nahodha huyo hakutaka kuonyesha ushirikiano badala yake alitengeneza mazingira ya kupoteza ushahidi kwa kutaka kukichukua kitu hicho ambapo alimfuata na kumwambia kwamba akishirikiana na Neto naye atamtoa kwa kadi nyekundu kauli ambayo ilimtisha na kuamua kuacha na baadaye kumtoa kwa kadi nyekundu Netto aliyekaidi.
Hata hivyo, Mahagi alisema tayari ameshawasilisha tukio hilo katika ripoti yake kwenda kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambapo akasema kumtoa kwake kwa kadi nyekundu kulikuwa ni sahihi ambapo Netto angeweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa tukio lake hilo. Ingawa mchezaji amekanusha vikali.
Kocha Mgambo
Kocha wa Mgambo JKT, Bakari Shime alisema; “Refarii alighafilika tu na kuamua kutoa ile kadi, ile ilikuwa si halali kwani hakuna kosa la msingi pale. Naiomba TFF ipitie upya picha za video za lile tukio na kuangalia uhalali.”
Kwa upande mwingine mchezaji wa Mgambo JKT, Mohamed Samata alidai kwamba kocha wao alistukia kwamba mapema watacheza pungufu akawapa mazoezi maalum; “Kocha wetu ni mzuri sana na anaona mbali kwani kabla ya mechi tulikuwa na mazoezi marefu sana ya kucheza tukiwa pungufu, alitujenga kisaikolojia na kuhakikisha kuwa hata kama tunakuwa pungufu uwezo wa kushinda tunao hivyo hilo lilitusaidia sana,” alisema Samata ambaye ni kaka wa Mbwana Samata anayekipiga TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
No comments:
Post a Comment