MTU mmoja mzee wa makamo anavuta sigara yake kubwa katika jumba la kifahari wakati huu eneo la Surrey kule Uingereza.
Anaweza kuwa katika nyumba hiyo au jumba lake jingine la kifahari jijini London ambalo lilimgharimu kiasi cha Pauni 48 milioni.
Anaweza kuwa anaogelea. Anaweza kuwa anapunga upepo kando ya bwawa la kuogelea. Anaweza kuwa amepumzika na mkewe akitazama mechi ya Ligi Kuu England huku akitafuna korosho zilizolimwa Mtwara.
Huyu ni Alisher Usmanov. Tajiri wa Kirusi. Rafiki wa karibu na pesa. Anatajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 18 bilioni. Ndiye mtu tajiri zaidi Russia. Anatajwa kuwa tajiri wa 34 duniani. Anaishi Uingereza na kwa sababu anaishi pale, kila kitu katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow pale London, basi huwa anatajwa kuwa mtu tajiri zaidi Uingereza.
Mwili wake unanukia pesa. Akili yake imeganda pesa. Suti zake zinanukia harufu ya benki. Akina Roman Abramovich wote wanasubiri mbele ya pesa zake. Usmanov ni shabiki mkubwa wa Arsenal.
Anamiliki asilimia 29 ya hisa za Arsenal. Unaweza kushangaa kuwa Arsenal wana mtu tajiri kuliko Chelsea, pengine kuliko Manchester City. Nini kinatokea? Watu waliokuwa na hisa nyingi Arsenal hawataki Usmanov aongoze timu. Badala yake hisa nyingi wamemuuzia Mmarekani Steve Kronke ambaye ndiye kama mmiliki wa Arsenal.
Kwanini hawataki? Hawataki kwa sababu mabosi wa Arsenal wanaongozwa na hisia za Arsene Wenger kwamba Arsenal wanapaswa kujiongoza wenyewe kifedha kwa kujikamua kupitia miundombinu yao kama mauzo ya jezi, mauzo ya wachezaji, viingilio na mikataba ya udhamini.
Wanadai kuwa hawataki mtu mwenye pesa nyingi aimiliki klabu hiyo kama mali yake ya mfukoni. Ndio maana waligoma kuuza hisa zao kwa Usmanov ambaye mawazo yake ni kuiendesha Arsenal kama Chelsea, Manchester City, Monaco au PSG.
Usmanov kila siku anawatukana. Anayo nafasi ya kuwatukana kwa sababu anaingia katika vikao vya bodi. Hisa zake zinamwezesha kuingia katika vikao hivyo.
Mara ya mwisho aliandika barua kwa bodi akilaani kuuzwa kwa Robin Van Persie kwenda Manchester United. Usmanov alibwatuka vilivyo. Akabwabwaja vilivyo.
Katika Dunia ya kisasa, mawazo ya Usmanov ndio sahihi zaidi. Lakini yanapingwa na mawazo ya Wenger ambaye anataka timu iundwe kama zamani. Wenger anataka timu ijijenge kwa kusubiri mchezaji kama Kieron Gibbs akomae. Lakini katika fasalafa za Usmanov, kama Gibbs bado hajakomaa, nafasi yake inabidi ichukuliwe na Marcelo.
Siku ambayo Usmanov atafanikiwa kuuziwa hisa nyingi Arsenal basi ujue ndio mwisho wa Wenger kwa sababu falsafa zao ni tofauti. Ndio siku ambayo Arsenal watafanya usajili wa kufuru kwa kuwanunua kwa pamoja, Radamel Falcao, Marcelo, Arturo Vidal, Luis Suarez na Thiago Silva.
Ni kama Abramovich alivyofanya au anavyoendelea kufanya Stamford Bridge. Ni kama ambavyo Sheikh Mansour anavyofanya Manchester City. Ndio maana timu zao huwa zinashindana katika mashindano na sio kushiriki.
Mchezaji wa bei mbaya siku hizi analipwa kwa wiki mshahara wa kuanzia Pauni 180,000 na kuendelea. Mshahara kama huo Arsenal inalipa kwa mchezaji mmoja tu, Mesut Ozil. Kwa Manchester City wachezaji sita wanalipwa kiasi hicho kwa wiki. Kwanini wasikupigie 6-0?
Wakati Man City katika safu ya ushambuliaji wana Sergio Aguero, Alvaro Negredo, Edin Dzeko na Jovetic, Arsenal wana Olivier Giroud peke yake. Anasaidiwa na mwanafunzi wa Shule, Yaya Sanogo, ambaye ametoka timu ya Daraja la Pili Ufaransa.
Dunia ya sasa suala la timu kuendeshwa kwa mapato ya mlangoni au mapato ya wadhamini, linaonekana kupitwa na wakati. Kama hauwezi kushindana na Warusi au Waarabu basi hakuna unachoweza kushinda kirahisi.
Tusipoangalia Barcelona inaweza kuwa timu ya mwisho duniani kupata mafanikio makubwa kwa kutumia wachezaji waliokulia klabuni kwa pamoja. Bahati yao ni kwamba katika mchakato huo walifanikiwa kumkuza mchezaji wa ajabu, Lionel Messi.
Vinginevyo hii ni Dunia ambayo inatawaliwa na pesa za Sheikh Mansour, Florentino Perez, Roman Abramovich na wengineo ambao wanaweza kuchomeka sindano ya noti katika akaunti ya timu na kumnunua Falcao, Cavani, Gareth Bale na wachezaji wa kariba hii.
Kama unataka kumuona Radamel Falcao anavaa jezi ya Arsenal subiri Usmanov aingie. kama unataka kumuona Eden Hazard katika jezi ya Arsenal subiri Usmanov aingie.
Septemba 2007, alinunua michoro ya mpiga tumba maarufu wa zamani wa Russia, Mstislav Rostropovich kwa Pauni 20 milioni. Sasa kwanini amuuze Van Persie kwa Pauni 25 milioni?
Lakini kwa hali ilivyo sasa, Wenger ataendelea sana kununua wachezaji wa bei rahisi kwa kisingizio cha kulinda tamaduni za klabu yake ambayo ni wazi imedumaa.
No comments:
Post a Comment