ALI ya hewa baina ya mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi na uongozi wa timu hiyo, si nzuri na Mganda huyo ameamua kugomea mazoezi akishinikiza kumaliziwa chake.
Picha lilianza hivi; Okwi alisajiliwa na Yanga kwa usajili uliogharimu Dola 100,000 (Sh162 milioni) katika usajili wa dirisha dogo, lakini uongozi wa timu hiyo haukumpatia fedha zote na walikuwa na makubaliano maalum. Walimkatia dola 60,000 tu kwa kuanzia.
Okwi ameshaichezea Yanga mechi sita za Ligi Kuu Bara na juzi Jumanne aligoma kufanya mazoezi yaliyofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam akitaka kulipwa fedha zake zilizosalia, jambo ambalo limewakera mabosi wa Yanga ingawa wanafanya siri kubwa.
Katika mazoezi hayo, Okwi alifika mapema na kukaa nje jambo ambalo si kawaida huku wenzake wakijifua chini ya kocha, Hans Pluijm, ambaye jana Jumatano aliliambia Mwanaspoti kuwa sababu za Okwi kushindwa kufanya mazoezi zipo nje ya uwezo wake.
“Siwezi kuzungumzia hilo tatizo la kutofanya mazoezi kwa Okwi, nadhani lipo juu ya uwezo wangu, lakini ninachoweza kusema ni kwamba tangu nilipofika Yanga nimekuwa na uhusiano mzuri na Okwi, nafikiri hicho ndicho ninachoweza kukwambia,” alisisitiza kocha huyo.
Lakini Okwi alipotakiwa kutoa ufafanuzi hakuzungumza lolote mazoezini hapo.
Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu, alikiri Okwi kutofanya mazoezi, lakini akadai kwamba anahitaji muda kukaa na mchezaji huyo kujua tatizo ila akasisitiza hawadai.
“Nimepata taarifa kwamba Okwi hakufanya mazoezi, lakini nitaongea naye kujua tatizo lake. Ila si kweli kwamba anadai fedha zozote,” alisema Njovu.
Mmoja wa viongozi wazito na mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Yanga, alizungumza na Mwanaspoti jana Jumatano na kuonekana kukerwa na tukio hilo, lakini akakiri kwamba mchezaji huyo anawadai.
Bosi huyo aliyeonekana kuwa mkali, alisema mpaka sasa Okwi ameshafunga mabao mawili pekee katika mechi za ligi alizocheza ambapo ukiacha hata wachezaji wenzake kwa ujumla wameshindwa kucheza kwa kujituma wakielekeza akili zao katika kupata fedha pekee.
“Hapa Yanga hakuna tatizo la fedha lakini tunawezaje kutoa fedha wakati wenyewe hawajitumi? Fedha tunazowapa hazilingani na mchango wao kwenye timu, imefikia hatua wanakubali kufungwa na wachezaji 10 wa Mgambo ambao mishahara yao ni sawa na posho tu kwa Yanga,” alisema bosi huyo kwa hasira.
“Hivi tumpe dola 40,000 Okwi kwa kipi cha kutufariji alichotufanyia? Nataka nikwambie kama Okwi anataka fedha zake jibu ni rahisi sana, aonyeshe kwenye mechi aone kama atazikosa tena zitakuja bila ya kuomba na hilo si kwa Okwi pekee, bali ni kwa wachezaji wote, fedha tunazo lakini hawatutendei haki.
“Tunatumia fedha nyingi kuwalipa mishahara mikubwa, lakini angalia mchezo wetu uliopita wanakubali kufungwa kirahisi na hata haiwaumi, tena kwa timu ambayo wanalipwa malipo madogo na tatu wakiwa pungufu, sasa wanakuja wachezaji hao hao eti wanadai fedha, hatuendi hivyo.”
Alidai kwamba Okwi hajafanya kile walichokitegemea wakati wanamsajili na kwamba anapaswa kuwa muungwana pia kwa vile uongozi uligharamia fedha nyingi kukamilisha usajili wake kuliko walivyotarajia.
No comments:
Post a Comment