ALIPOIBUKA msanii wa Bongo Fleva, MB Doggy, kwa nyimbo zilizotamba za ‘Latifah’, ‘Mapenzi Kitu Gani’, ‘Ina Maana’, ‘Natamani’ na nyinginezo, alichochea chipukizi kadhaa nao kuiga staili ya uimbaji wake.
Miongoni mwa waliochipuka kwa mtindo sawa na huo na kupata umaarufu kutokana na vibao matata, ni Z- Anto aliyetamba na vibao vya ‘Binti Kiziwi’, ‘Mpenzi Jini’ na ‘Kisiwa cha Malavidavi’.
Baada ya kupata mafanikio kiasi cha haja, Z-Anto alianza kufifia na mwishowe kuwa kimya.
Hivi karibuni katika pita pita za Mwanaspoti jijini Nairobi, Kenya ilikutana naye na kuzungumza naye kama ifuatavyo.
Mwanaspoti: Kabla hujatueleza kisa cha ukimya wako, tueleze wewe ni nani?
Z-Anto: Mimi ni Ali Mohammed, nilizaliwa mwaka 1988 jijini Dar es Salam na nimekulia huko. Asili yangu ni Kenya kwani baba anatokea mjini Lamu (Mkoa wa Pwani). Mama ni mzawa wa visiwa vya Comoro, baada ya kukutana na baba ndio wakahamia Dar es Salaam. Lakini kwa sasa wazazi wangu wote ni marehemu.
Mwanaspoti: Pole sana. Sasa jina la Z-Anto ulilipataje?
Z-Anto: Z-Anto ni jina langu la kikazi. ‘Z’ ni herufi ya mwisho, maana yake mimi ni kitinda mimba kwenye familia ya watoto sita.
‘A’ inawakilisha jina langu la kwanza Ali, ‘N’ ni kiunganishi na ‘TO’ ni ufupi wa jina langu la zamani Tony.
Mwanaspoti: Mbona umekuwa kimya kiasi hiki? Ina maana ulipotoa vibao vya mwanzoni ulibahatisha?
Z-Anto: Ukimya wangu umetokana na mahangaiko na matatizo ya kimaisha na changamoto za kimuziki.
Z-Anto: Ukimya wangu umetokana na mahangaiko na matatizo ya kimaisha na changamoto za kimuziki.
Mwanaspoti: Kwa hiyo umeachana na muziki?
Z-Anto: Siwezi kuacha muziki. Hata unavyoniona sasa nipo huku Kenya kwa ajili ya shoo katika miji ya Kisumu na Nakuru. Pia nina mazungumzo na Shirika la Ndege la Kenya kwa ajili ya promosheni ya ndege zao mpya.
Mwanaspoti: Baada ya kutoa ‘Mpenzi Jini’ na ‘Binti Kiziwi’ ndio ukawa kimya, ulikwenda wapi?
Z-Anto: Nilibanwa na ratiba ya shoo nyingi tu, ndio maana nilichukua muda kabla ya kutoa ‘Kisiwa Cha Malavidavi’.
Mwanaspoti: Inadaiwa ulifilisika, ni kweli?
Z-Anto: Sijafilisika, ila mapato yamepungua. Unajua magazeti kwa kawaida hutafuta ‘headline’ ili kuuza. Ni hivi, nilikuwa na matumizi makubwa ya pesa, wakati mwingine nilinunua hata vitu ambavyo sikuvihitaji, lakini sikuishiwa.
Mwanaspoti: Mbona inadaiwa uliuza magari yako yote manne?
Z-Anto: Hah Hah, nyie wanahabari mna mambo, hizo ni hadithi tu. Kwanza sijawahi kuwa na magari manne. Ni matatu na yote bado ninayo. Ni vitega uchumi vyangu.
Mwanaspoti: Umesema ukimya ulitokana na changamoto za kibinafisi na pia kimuziki, ni changamoto zipi hizo za kimuziki?
Z-Anto: Tatizo kubwa ni kundi la Tip Top Connection lililokuwa likinisimamia kimuziki. Tip Top iliniangamiza kisanii, kundi hilo lilihujumu fedha zangu. Mwaka 2008 nilipangiwa shoo nyingi Kenya, niliondoka nikiacha albamu yangu ya ‘Binti Kiziwi’ na ya Ali Kiba ‘Cindellera’ zikitamba sokoni.
Baada ya shoo za Kenya nilirudi nyumbani, wasimamizi wa Tip Top Connection (Abdu Bonge na Babu Tale) wakanipa Sh10 milioni kutokana na mauzo hayo. Lakini baadaye nikagundua walinitapeli Sh58 milioni.
(Hata hivyo Babu Tale ambaye ni meneja wa Tip Top Connection, alipoulizwa kuhusu madai ya Z-Anto, alikana na kumtaka aende mahakamani kama anahisi alitapeliwa).
Mwanaspoti: Ikawaje, ulidai fedha zako?
Z-Anto: Niliwaachia tu, nikajiondoa katika kundi. Si peke yangu niliyeondoka, kuna akina MB Doggy, Cassim Mganga, PNC, Spark na Keisha, wote walitimka.
(Lakini Tale amesisitiza hakuwawadhulumu wasanii ndiyo maana Madee alianza na kundi na mpaka leo bado yupo).
Mwanaspoti: Kuna binti fulani ulikuwa na uhusiano naye, yuko wapi siku hizi?
Z-Anto: Hahaha, yule (tunahifadhi jina lake kwa sababu za kimaadili) nilikuwa na uhusiano naye. Alikuwa mke wangu ila ndoa yetu haikudumu.
Mwanaspoti: Mbona mkaachana? Ni kweli mama yako hakumpenda?
Z-Anto: Mama alikuwa miongoni mwa waliompenda, ndio maana hata nilipotengana naye sikumtaarifu mama kwa miezi mitatu.
Ndoa yetu ilidumu mwaka moja na nusu, tatizo lake ustaa ulikuwa mwingi na alishindwa kuumudu. Alianza kuwa na kampani mbaya ya wauza unga walioishia kumfundisha biashara hiyo. Nilimkanya lakini hakunisikiliza, ndio tukaachana.
Mwanaspoti: Kwa sasa yuko wapi?
Z-Anto: Amefungwa China. Alipatikana na hatia ya kuuza dawa za kulevya.
Z-Anto: Amefungwa China. Alipatikana na hatia ya kuuza dawa za kulevya.
Mara ya mwisho nilipozungumza naye baada ya kutengana, aliniarifu yupo China kibiashara. Ilikuwa safari yake ya kwanza nje ya nchi kwa ajili ya biashara hiyo na akaishia kukamatwa.
Mwanaspoti: Kwa sasa una mke?
Z-Anto: Ndio, ninaye na tumejaaliwa kupata mtoto mmoja.
Mwanaspoti: Kimuziki, utaendelea kuwa kimya?
Z-Anto: Nina kazi inayoweza kutoka muda wowote ‘Nipote’. Humo nimemshirikisha, Abdu Kiba, ambaye ni mdogo wake Ali Kiba.
Mwanaspoti: Tumalizie, inadaiwa kuwa kuna bifu baina ya Ali Kiba na Diamond Platinumz, ni kweli?
Z-Anto: Lipo, tena kubwa tu. Walifanya kazi mbili ambazo hazikutoka. Humo Ali Kiba aliimba sana kitu kilichomchoma Platinumz, akafuta baadhi ya mistari ya Kiba. Ali Kiba hakufurahi.
Mwanaspoti: Mafanikio ya Diamond unayazungumiaje?
Z-Anto: Ni mwimbaji mzuri, mafaniko yake yamechangiwa na promosheni anayoipata ambayo wengine tunaikosa.
Z-Anto: Ni mwimbaji mzuri, mafaniko yake yamechangiwa na promosheni anayoipata ambayo wengine tunaikosa.
No comments:
Post a Comment