KULIKUWA na kikao kwenye chumba maalumu cha mikutano ofisini kwa Edward Woodward huko Old Trafford, mara simu ikasikika ikiita.
Ulikuwa usiku wa nusu fainali ya Kombe la Ligi, Manchester United ilipomenyana na Sunderland na kupoteza kwa mikwaju ya penalti. Hilo lilikuwa pigo jingine kubwa kwa Man United katika msimu huu.
Ndani ya chumba hicho kilichokuwa kikijadiliwa ni uhamisho wa kiungo Mhispaniola Juan Mata. Mambo yalikuwa bado magumu, hawakuwa wamempata staa huyo ambaye huenda akawasaidia kwenye nusu fainali hiyo.
Hata hivyo, mazungumzo ya kumnasa Mata kutoka Chelsea yalikuwa kwenye hatua nzuri. Woodward alionekana kuwa na shughuli nyingi sana kwenye kulikamilisha suala hilo na hivyo kuacha kunywa kahawa yake iliyokuwa kwenye kikombe mezani alipoketi.
Tangu alipochukua nafasi ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Manchester United, Woodward amekuwa akifanya mikutano ya mara kwa mara na waandishi wa habari ofisini kwake. Ni mtu anayeonekana kutaka kila anachokifanya kipate kutambulika kwa haraka.
Kwa utendaji wake wa kazi, huwezi kufikiria kama Man United inaweza kuzama wakati huo akiwa madarakani.
Siri yafichuka
Man United inaonekana kufanya mikakati ya usajili wa kimyakimya. Kwenye mkutano huo, ndipo siri ya usajili wa Mata ilipofichuka rasmi. Kwenye majira yajayo ya kiangazi, Man United imepanga kufanya usajili wa nyota wa maana ili kukifanya kikosi hicho kuwa na nguvu zaidi na kurejea kwenye makali yake.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu England jambo ambalo limekuwa likiwasumbua wadau wake wengi wakiwamo mabosi wa klabu hiyo kwa sasa kufanya vibaya kunaingia hasara kubwa klabu.
Ofisini kwa Woodward ndipo kulikofahamika siri nyingi zinazohusu mipango ya klabu hiyo katika biashara za kufanya usajili wa maana baada ya msimu kumalizika, lakini kubwa likitegemea zaidi nafasi itakayoshika klabu kwenye ligi mwisho wa msimu.
Akiwa kwenye kikao hicho, mara simu yake iliita na kuwaomba samahani waandishi waliokuwa mbele yake kwamba anapokea simu. Kwa bahati mbaya, simu hiyo aina ya BlackBerry, ilijibonyeza spika ya nje kimakosa na hivyo mazungumzo ambayo yangekuwa ya siri yaliweza kusikika bayana.
Sauti ya mtu aliyekuwa akipiga simu ikasikika na wote waliokuwa kwenye mkutano huo na kufichua biashara za siri zinazofanywa na klabu hiyo katika mipango ya kujiimarisha zaidi.
Woodward alishituka sana baada ya kugundua simu yake inasikika. Kwa mshituko huo huo akamwambia aliyekuwa akizungumza naye. “Tafadhali, subiri, acha usizungumze kitu.” Kisha alichukua simu yake na kukimbilia kwenye chumba kingine na hapo akaponyeza kitufe cha kuondoa spika ya nje ili kuficha siri.
Hata hivyo, presha hiyo ilibainisha wazi jinsi bosi huyo alivyo kwenye wasiwasi mkubwa kutokana na mwenendo mbaya wa kikosi cha Man United msimu huu.
Imefichuliwa kwamba kinachomtokea Woodward kwa sasa kilimtokea pia mtangulizi wake, David Gill. Biashara zozote haziwezi kwenda vizuri kama timu inapokuwa kwenye nyakati ngumu na kupata matokeo mabovu kama ilivyo kwa sasa.
Usajili wa Mata
Man United ilipaniki na kuona hakuna namna nyingine ya kuweka sawa msimu wao pengine zaidi ya kumsajili Mhispania huyo. Walizama mfukoni na kumfanya staa huyo kuweka rekodi ya uhamisho kwenye kikosi chao baada ya kumnasa kwa pauni 37 milioni kutoka Chelsea.
Lakini, usajili wa staa huyo ulikuwa wa mipango zaidi kwa sababu ilikuwa sehemu ya kupanua soko lao la kibiashara na kuongeza mauzo ya jezi baada ya kuona mambo yanaharibika kwenye upande wa matokeo ya timu kwenye mechi zake.
Mastaa kama Robin van Persie, Wayne Rooney na Marouane Fellaini, mauzo ya jezi zao yamekuwa si ya kasi sana kama ilivyokuwa mwanzoni na hivyo waliamini usajili wa Mata unaweza kuwa na kitu tofauti za kuzungumziwa katika klabu hiyo.
Hata hivyo, Mata ni mwanzo wa mipango ya usajili wa nyota wengine watakaofuata Old Trafford baada ya mambo kufahamika hadharani kwenye kikao hicho.
Ziara ya Dubai
Woodward alitengeneza mazingira ya kuipeleka timu mapumziko Dubai kwenda kufanya mazoezi kwenye mazingira ya hali ya hewa ya joto. Uamuzi wa kumbakiza Rooney kikosi hapo kwa pesa nyingi ulifikiwa kwa ajili ya mtazamo wa kibiashara zaidi.
Kwenye ziara yake ya Dubai, Man United ililenga kwenye wigo wa kibiashara ukiwa ni mpango wa kuweka mazingira sawa ya kucheza mechi za kirafiki katika ukanda huo kama sehemu ya kuingia pesa kufidia hasara itakayopata timu kutokana na kushindwa kuingia kwenye nne bora na kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Tayari Man United imeshawanasa wadhamini kadhaa ambao watawezesha kucheza mechi maalumu za kibiashara wakati itakaposhindwa kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao na kwamba watakuwa wakitembelea sehemu mbalimbali kuzunguka dunia kwa ajili ya mechi maalumu kitu ambacho kinadaiwa kunaweza kuzishawishi klabu nyingine kuingia kwenye mpango huo.
Matokeo mabovu ya uwanjani si kosa la Moyes wala Woodward, lakini katika harakati za kupambana na presha ya kuingia hasara uamuzi wa kucheza mechi za kirafiki zenye malipo ulifikiwa kama timu itafeli kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kwa nini Ferguson alishinda
Kwenye klabu ya Man United, Ferguson alikuwa mjanja sana. Aliwafanya wachezaji wa timu hiyo kuwa sehemu yake. Man United haikuwa na wachezaji tishio sana, lakini Ferguson aliwafanya kupambana kwa ajili yake wanapoingia uwanjani. Kitu ambacho alikifanya Mskochi huyo ni kwamba wachezaji wote aliowasajili alihakikisha wanawafahamu vizuri hadi familia zao.
Amekuwa akiwatembelea wazazi wa wachezaji wake na wakati mwingine kunywa nao chai kwenye makazi yao bila ya kujali kwambe yeye ni mtu mashuhuri.
Mfano mzuri alikwenda nyumbani kwa kiungo Darren Fletcher na kupata chakula pamoja na familia hiyo kwenye makazi yao ya hadhi ya chini huko Edinburgh. Ferguson aliifanya Man United kuwa mali yake, alimchagua kaka yake, Martin kufanya shughuli za kutafuta wachezaji.
Jambo hilo na staili yake ya kuishi na wachezaji ilifanya Man United kuwa klabu maarufu sana na kupata hadhi kubwa duniani na hivyo kupata mikataba mbalimbali ya kuvutia wadhamini. Lakini, ukweli halisi kama asingekuwa Ferguson, huenda Man United ingekuwa klabu maskini sana.
Kitu ambacho anapaswa kukifanya Moyes ni kuiga staili ya mtangulizi wake na kuwafanya wachezaji wake kucheza kama ndugu kama ilivyokuwa enzi za Ferguson kitu ambacho alikifanya na kufanikiwa.
Ni aibu, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliofanyika Jumanne iliyopita dhidi ya Olympiakos, Van Persie alimpasia mpira Rooney mara moja tu, jambo ambalo limeonyesha bayana kwamba ushirikiano wa wachezaji hao ndani ya uwanja si mzuri.
No comments:
Post a Comment