Monday, 31 March 2014

Kina Giggs wanunua timu ya mtaani kwao



SALFORD, MANCHESTER
WALITWAA mataji matatu mwaka 1999 pale Nou Camp pamoja. Walitwaa mataji mengine Old Trafford wakiwa pamoja. Lakini sasa mastaa watano wa zamani wa Manchester United maarufu kwa jina la ‘Class of 92’ wanataka kununua timu yao na kuipeleka Ligi Kuu England.
Ryan Giggs, Paul Scholes, Nicky Butt na ndugu wawili Gary na Phil Neville, kwa sasa wamekubaliana kuwa wamiliki wa klabu ya Salford City ambayo haipo daraja lolote, lakini wana mpango wa kuipeleka mpaka Ligi Kuu England ndani ya mpango maalumu wa miaka 15.
Kimahesabu timu hiyo iliyopo katika Jiji la Manchester, ni kama vile iko daraja la nane, lakini akina Giggs wana mpango madhubuti wa kuipeleka hadi Ligi Kuu na wana uhakika kitendo cha kumiliki timu hiyo kitasababisha kuvutia wachezaji wenye majina makubwa klabuni hapo.
Wanaamini kuwa kitongoji cha Salford kina rasilimali kubwa ya kuibua timu imara ambayo itatisha katika Ligi Kuu England misimu mingi ijayo.
Scholes anataka kuwa kocha wa timu hiyo kwa miaka mingi ijayo kama ikifanikiwa kupanda katika madaraja kadhaa. Nyota hao wameiweka Salford katika mioyo yao kutokana na ukweli kwamba mji huo ulikuwa nyumbani kwao kwa maana ya kwamba ndipo kulikuwa na uwanja wa mazoezi wa Manchester United kabla hawajajenga uwanja mpya wa mazoezi Carrington mwaka 2000.
Wakongwe hao wanataka kulipa fadhila katika mizizi yao ya soka ambapo walikuzwa angali wakiwa vijana hasa Giggs ambaye licha ya kuzaliwa Wales, lakini kwa kipindi kirefu cha maisha yake amekulia Salford.
“Kila mtu anajua umuhimu wa Salford kwangu, kwa hiyo hili ni chaguo la moyo wangu na ni kitu ambacho tunakiamini. Tunataka kuunganisha jamii na soka, kutumia uzoefu wetu na ufahamu wetu kwa ajili ya kuibua vipaji na kuifanya Salford iwe ya kuvutia zaidi,” alisema Ryan Giggs.
Gary Neville anasema Salford ni sehemu maalumu sana kwake kwa sababu ndio sehemu aliyoanzia utotoni kabla ya kuibuka na Manchester United na kuwa mchezaji maarufu duniani.
“Majaribio yangu ya kwanza na Manchester United yalikuwa Salford wakati nikiwa na umri wa miaka 14 na kamwe sijasahau jinsi ilivyokuwa muhimu sana kwangu. Salford FC inawakilisha maisha yangu ya miaka hiyo, njaa, hamu, mvuto, kiu, tamaa ya mafanikio na moyo wa soka. Nina furaha sana,” alisema Neville.
Kwa upande mwingine, Scholes ameelezea mipango mitano kwa ajili ya kuiendeleza timu hiyo kuifanya iwe maarufu na bora katika siku za usoni.
“Tunajua itakuwa ngumu, lakini tumepania kuanza hili tangu mwanzo na tuna mipango ya kuvutia kwa ajili ya kusonga mbele,” alisema Scholes ambaye pia ni mzaliwa wa Salford.
Hata hivyo, mmiliki mwingine mpya, Nick Butt, amekataa wazo la timu hiyo kuhamia katika Uwanja wa AJ Bell ambao unatumiwa pia na timu ya Rugby ya Salford City Reds.
“Ni uwanja wenye urithi wa zamani, una umri mkubwa zaidi eneo hili na inabidi ulindwe kwa ajili ya kumbukumbu ya vizazi vijavyo,” alisema.
Mwenyekiti wa sasa wa Salford City, Karen Baird, ambaye alikuwa chachu kubwa katika dili hilo la akina Giggs kuinunua klabu yake,  alionekana mwenye furaha na kushukuru uwepo wa dili hilo.
“NI muda wa kufurahisha kwa timu ya Salford City FC na naamini kuna mambo mengi yanakuja kwa ajili ya klabu. Naamini kutakuwa na mafanikio mengi siku za usoni. Bila shaka dili hili litasababisha kuwa na hali nzuri sana siku za usoni na ni tangazo kubwa kwa soka lisilo la ligi,” alisema Baird.
“Klabu inasapoti kundi hili na inaamini kuwa ni kitu kizuri kwa timu ya  Salford City FC na mji wenyewe wa Salford.”
Kwa Giggs na Gary Neville huo ni mwendelezo mwingine wa mapenzi yao kwa mji wa Salford ambapo mwaka jana walifungua mgahawa katika mji huo. Mgahawa huo ni mzuri kwa kutazamia michezo mbalimbali.
Kwa sasa Phil Neville ni Kocha Msaidizi katika kikosi cha kocha, David Moyes, ambacho kinaonekana kusuasua katika michuano yote wanayoshiriki msimu huu. Giggs ameendelea kuwa Kocha Msaidizi katika hicho.
Nick Butt yeye ni kocha wa timu za vijana Old Trafford wakati Gary Neville ameibuka kuwa miongoni mwa wachambuzi mahiri wa soka nchini England.

Katika orodha hii hayupo David Beckham ambaye hata hivyo na yeye amenunua timu ya Miami FC inayoshiriki soka la Ligi Kuu Marekani.

No comments:

Post a Comment