![]() |
YANGA imeonyesha kiburi baada ya kutibua na kuipiga chini dili ya kampuni moja ya Arabuni ambayo walikubaliana awali kuonyesha mechi zao dhidi ya Al Ahly kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga imekosa kiasi cha dola 70,000 ambazo ni zaidi ya Sh 112 milioni baada ya kushindwa kuafikiana na Kampuni ya MGB Misri kuhusu kuonyeshwa moja kwa moja michezo hiyo ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika makubaliano ya awali, Yanga ilipaswa kulipwa dola 35,000 kabla ya mechi na kiasi kingine kilipwe baada ya mechi hiyo iliyoisha kwa Wanajangwani kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, ofisa wa MGB, Francis Gaitho, alisema kampuni hiyo iliingizia Yanga kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake ya Misri lakini ikataka ilipwe fedha zote kabla ya mchezo huo.
Kutokana na mambo kwenda kinyume, MGB ilibidi ifanye jitihada mbalimbali za kuilipa Yanga lakini mambo yalipoenda kombo ikabidi wachukue dhamana kwa Ubalozi wa Misri nchini na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hata hivyo Yanga ilikataa dhamana hizo.
Kwa kuwa timu ya kurekodi mchezo huo kutoka Misri ingechelewa kutokana na ratiba za ndege, kampuni hiyo iliamua kutoa tenda hiyo kwa Star TV waweze kurekodi na kuwarushia halafu wao wasambaze kwa nchi za Afrika Kaskazini na Magharibi. Yanga haikukubali Star TV kufunga vifaa vyao uwanjani hapo kwa muda uliopangwa na hata iliporuhusu muda ulikuwa umeisha kuweza kufunga vifaa na kurusha mchezo huo.
“Nasikia viongozi wa Yanga ni matajiri lakini sielewi kwa nini dola 35,000 ziliwanyima usingizi, ni kiasi kidogo sana cha fedha lakini hawakujua thamani ya mchezo ule na kuamua kukataa kuonyesha mechi,” alisema Gaitho.
Alisema hiyo ilikuwa nafasi pekee kwa wachezaji wa Tanzania kujiuza kimataifa kwani vipaji vyao vingeonekana kote duniani na wangeweza kuitwa na klabu mbalimbali za ndani na nje ya Afrika.
“Yanga imewanyika haki watu wa Misri na Tanzania kutazama mechi ile ya kihistoria, Yanga ingejitangaza kote duniani kwani watu wangetaka kuona ni timu gani iliyowafunga mabingwa wa Afrika, hivyo bao lake pekee lingetazamwa kila mara ulimwenguni,” alisema Gaitho.
Mwanaspoti lilipowasiliana na Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema apigiwe baadaye pindi atakapopata taarifa rasmi kuhusu sakata hilo. Hadi jana saa 10:52 jioni katibu huyo hakuwa akipatikana katika simu na hata viongozi wengine hawakupatikana.
Baadaye saa 10:57 alipatikana Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Moses Katabalo ambaye alisema: “Tafadhali mtafute katibu kuhusu hilo suala, sipo katika nafasi ya kuzungumzia.”
Nyota wa zamani wa Al Ahly, Zakaria Nassef amelalamikia kitendo cha Yanga kuwabania kuona mechi hiyo aliyoiita ya karne.
Nassif alisema kupitia televisheni ya Al Ahly kuwa: “Inashangaza sana, ni mchezo wa raundi ya 32 lakini hili limejitokeza, je ingekuwa raundi ya 16 ingekuwaje?”
No comments:
Post a Comment