Friday, 14 February 2014

Wachezaji Simba wamshtaki kocha Logarusic kwa Rage

WACHEZAJI wa Simba, juzi Jumanne mchana, walikuwa na kikao na Mwenyekiti wa klabu yao, Ismail Aden Rage na kuzungumza naye kuhusu sababu za timu kufanya vibaya katika Ligi Kuu Bara. Katika kikao hicho wakatoa sababu mbili kubwa ambazo si nzuri kwa kibarua cha kocha, Zdravko Logarusic.
Simba ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kisha ikafungwa bao 1-0 na Mgambo JKT katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumapili iliyopita, jambo ambalo lilizua utata kiasi cha uongozi kuamuru timu badala ya kwenda Mbeya, irudi Dar es Salaam kwa kikao cha faragha.
Mmoja wa wachezaji wa Simba aliyekuwa kwenye kikao hicho, aliliambia Mwanaspoti kuwa Rage aliwauliza sababu ya kutofanya vizuri katika mechi hizo na wakamjibu kuwa mara nyingi wanaingia katika mechi wakiwa na wasiwasi mkubwa kwani wanapokosea kidogo tu, kocha huwa anawakaripia kupita kiasi
.
“Tumemwambia Mwenyekiti kuwa tunacheza kwa wasiwasi mkubwa kila mechi hasa za mikoani, kocha amekuwa mkali kupita kiasi na hata ukipata nafasi kikosi cha kwanza unawaza kukaripiwa badala ya kucheza,” alisema mchezaji huyo.
Pia wachezaji hao walimwambia Rage kuwa wanataka kusafiri kikosi kizima wanapoenda mikoani kwani wana basi kubwa linaloweza kubeba watu zaidi ya 50, hivyo hakuna haja ya kuondoka na wachezaji 22 na nafasi zingine kujazwa na wanachama ambao hawana msaada kwa timu.
Jambo jingine waliloliomba wachezaji hao ni kuwahishiwa mishahara na ulipwaji sawa wa posho mbalimbali.
“Katika mfumo wa sasa, tunaopewa posho ni wachezaji wanaocheza na wanaovaa jezi tu. Tumekubaliana na Mwenyekiti kuwa tulipwe posho sawa kwa waliocheza na wasiocheza, hata wale wasiovaa jezi kwani sisi wote ni kitu kimoja, wasitugawe,” alisema mchezaji huyo.
Mchezaji huyo aliongeza kuwa baada ya kikao hicho, Rage alipanga kukutana na Logarusic na Mwanaspoti lina taarifa za Mwenyekiti huyo kukutana na kocha na kuzungumzia tuhuma hizo za wachezaji.

No comments:

Post a Comment