Thursday, 27 February 2014

Tanzania kuna vipaji vingi, hakuna wachezaji




NOVEMBA mwaka jana, Simba iliachana na kocha Abdallah Kibadeni na kumpa mkataba wa miezi sita, Zdravko Logarusic, wa Croatia.
Kibadeni aliondoka na watu wa benchi lake la ufundi wakiwamo Kocha Msaidizi Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Kocha wa Makipa, James Kisaka (marehemu sasa).
Uongozi ulimteua Selemani Matola kumsaidia Logarusic na Idd Pazi akapewa jukumu la kuwafundisha makipa.
Ndani ya muda mfupi Logarusic amekuwa kocha kivutio na anayeonekana kuwa na uamuzi usiopinda hasa kwa mchezaji anayefanya vibaya. Hana masihara na wachezaji wazembe.
Kama hujui, Logarusic atakwambia, ukifanya vizuri hawezi kusita kukusifu. Vituko vyake mazoezini na kwenye mechi, vinawafanya mashabiki kumfurahia licha ya hivi karibuni Simba kupata matokeo yasiyoridhisha.
Vituko vya kocha huyo ni pamoja na lugha ya vitendo anayopenda kuitumia, huwa anatumia vidole, miguu na hata kichwa ili kufikisha ujumbe kwa wachezaji wake. Ana tabia za kushangaza, hiyo ni pamoja na kumwingiza mchezaji, kisha kumtoa haraka kama hachezi kwa kufuata maelekezo yake.
Mmoja wa waathirika wa tabia hizo za Logarusic ni mshambuliaji Betram Mwombeki ambaye katika mchezo dhidi ya Rhino Rangers hivi karibuni, aliingia na kutoka baada ya dakika 20, kisa kikiwa ni kucheza chini ya kiwango.
Tanzania vipaji vingi, hakuna wachezaji
Mwenendo wa Simba katika Ligi Kuu Bara ni wa kusuasua baada ya kutoka sare katika mechi mbili na kufungwa mbili pia. Simba imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na Mbeya City. Logarusic anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na vijana wenye vipaji vya kucheza soka, lakini kwa bahati mbaya haina wachezaji wanaofuata misingi ya soka.
“Kuna vipaji vingi sana hapa Tanzania, ila tatizo elimu ya soka ni ndogo na wengi wenye vipaji hawapati elimu za awali kutoka kwa makocha, kitu ambacho si sahihi,” anasema.
Anasema hiyo ni changamoto katika ufundishaji wa timu yake kwani mambo anayowafundisha yanaonekana kuwazidi uwezo wachezaji wake.
“Tatizo wamenileta hapa kufundisha elimu ya chuo kikuu wakati wachezaji wengi hata elimu ya msingi hawana, hili ni tatizo hivyo ipo haja ya kuwafundisha vijana hawa kuanzia ngazi za chini,” anasema Logarusic.
Kocha huyo anakiri kulipwa vizuri kuliko alivyokuwa analipwa Kenya wakati anaifundisha Gor Mahia na kuongeza kuwa majukumu anayopewa kocha Tanzania hayatofautiani sana na Kenya.
Kuhusu ushirikiano kati ya kocha na viongozi wa timu, Logarusic anasema kwa Tanzania ushirikiano upo mkubwa tofauti na Kenya.
“Wakati nasaini mkataba wangu Simba, niliuomba uongozi uniamini, kitu ambacho wanaendelea kukifanya ndiyo maana nilianza vizuri,” anaongeza.
Utani wa jadi Simba, Yanga
Logarusic anapenda jinsi upinzani wa jadi kati ya Simba na Yanga unavyofanya kazi katika soka la Tanzania kwani unapendezesha soka nchini na kuhamasisha ushindani katika ligi.
“Utani huu wa jadi si mgeni sana kwangu kwani kwa Kenya timu ya Gor Mahia na AFC Leopards zina utani wa aina hiyo japokuwa kwa hapa Tanzania umezidi, lakini ni muhimu kwa kukuza soka la nchi maana bila upinzani huwezi kuwa na ligi bora,” anasema.
Hata hivyo, Logarusic anasema mechi za watani wa jadi mara nyingi zimekuwa na madhara ambapo timu moja inapofungwa lazima itazua chokochoko iwe kwa haki au vinginevyo.
Licha ya Simba kusuasua katika ligi, amepanga kuhakikisha anafanya vizuri katika mchezo dhidi ya Yanga uliopangwa kuchezwa Aprili 27.
Akizungumzia viwanja vya Tanzania, kocha huyo anasema vingi kuanzia vya mazoezi hata vya mechi, havina ubora.
“Vingi havina nyasi na havipo sawa vina mabonde. Hali hiyo huwa ni ngumu timu kucheza katika kiwango kizuri muda wote,” anasema.
Anasema ligi ya Tanzania ina ushindani mkali baina ya timu na timu tofauti na Kenya ambako timu kali ni Leopards, Gor Mahia na Tusker pekee wakati hapa nchini hata ukizitoa Yanga, Simba na Azam, zipo timu nyingine zinazotoa upinzani mkubwa ikiwamo Mbeya City.
Timu za Bongo zinajiandaa vizuri kuliko Kenya
Tofauti na Kenya, Logarusic anasema timu za Tanzania zina maandalizi mazuri katika ligi na hata kabla ya ligi kuanza huwa zinajifua kikamilifu hivyo kuweka upinzani mkubwa katika michuano yoyote ile.
“Tanzania timu zinajiandaa sana, hali hii ni tofauti na Kenya kwani kule muda wa mazoezi si mwingi. Ndio maana Tanzania timu ziko katika hali ya kushindana wakati wote,” anasema Logarusic.
Kocha huyo anasema hata waandishi wa habari wa Tanzania wanajitahidi kufuatilia mambo ya timu kuanzia katika kikosi hadi vitu vinavyofanyika uwanjani siku ya mechi hata mazoezi.
“Hapa naona kuna magazeti mengi zaidi tofauti na Kenya na pia waandishi wengi wanafuatilia michezo kwa makini na kuandika zaidi,” anasema .
Mipango yake Simba
Logarusic anayefurahia maisha ya Tanzania yaliyojaa amani na upendo miongoni mwa watu wake, anasema amejipanga kutengeneza kikosi imara cha timu yake ili kiweze kushindana kitaifa na kimataifa siku za usoni.
“Simba haijashinda taji kwa miaka miwili sasa, kwanza nataka kuwapatia ubingwa wa Bara kisha kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika, kwani kushiriki michuano hiyo ni ndoto yetu,” anasema kocha huyo.
Logarusic anasema mambo yote aliyopanga yanaweza kufanikiwa endapo atashirikiana vyema na wenzake katika benchi la ufundi na uongozi wa Simba bila kujali masilahi ya mtu.

No comments:

Post a Comment