YUKO wapi yule aliyesema ya Kaisari mwachie Kaisari? Alikuwa anamaanisha kuwa mambo ya pesa au ya kidunia tuwaachie wenye dunia yao. Hakukosea sana. Sijawahi kusikia manabii wa zamani wakikosea.
Juni mwaka huu, yeyote atakayetua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sao Paulo, Guarulhos au ule wa Rio de Janeiro, Galeao kushuhudia fainali za Kombe la Dunia, macho yake yataanza kusuuzika kuanzia uwanja wa ndege.
Utahitaji nini zaidi? Wasichana warembo, joto la kadri ambalo litakufanya ukimbilie fukwe za Copacabana, chakula cha asili, madafu, ngoma za samba lakini zaidi kila sura ya mwanadamu inatabasamu. Wakati mwingine hata kama una pesa nyingi maishani kama haujawahi kufika Brazil basi hazina maana.
Bahati nzuri, Mungu ametuletea tena Kombe la Dunia nchini humo baada ya miaka 63. Ni ndoto ya kila mchezaji kucheza Kombe la Dunia katika ardhi ya soka Brazil. Ni ndoto ya kila mchezaji wa Brazil kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini kwao.
Kikosi cha Brazil cha wakati huo kilikuwa na mastaa wao kina Nílton Santos, Zizinho, Ademir, Jair na wengineo. Usisahau pia kumkumbuka kipa wao, Barbosa aliyewafungisha katika mechi ya fainali dhidi ya Uruguay na taifa zima likamtenga.
Mwaka huu kila mchezaji wa Brazil anatamani kuichezea Brazil. Utapata wapi tena bahati kama hii? Utapata wapi bahati ya kuliwakilisha taifa lako linaloabudu soka, tena katika ardhi yako?
Neymar, Lucas Moura, Oscar, David Luiz, Thiago Silva na wachache wengineo wanakaribia kuipata bahati hii.
Mtu mmoja anakaribia kuikosa nafasi hii. Kipa wao wa kwanza, Julio Cesar. Yuko Queens Park Rangers. Timu yake iko daraja la kwanza England. Namaanisha daraja la kwanza, siyo Ligi Kuu.
Unajua Cesar analipwa mshahara kiasi gani? Analipwa Pauni 90,000 kwa wiki. Tangu alipochukuliwa kutoka Inter Milan misimu mitatu iliyopita, huu ndiyo mshahara wake. QPR ni moja kati ya klabu ndogo zinazolipa mishahara mikubwa England.
Tajiri wa QPR anaitwa Toni Fernandes ambaye ni Muasia mwenye asili ya Uingereza. Mpaka sasa utajiri wa Fernandes unakadiriwa kuwa Dola 625 milioni. Ni tajiri wa 21 nchini Malaysia. Ni mmoja kati ya wamiliki wa Shirika la Ndege la Asia, Air Asia.
Tangu washuke msimu uliopita, Cesar kagoma kuhama. Timu zinamtaka, lakini zinamwambia apunguze mshahara wake. Lakini yeye mwenyewe na wakala wake wamegoma. Anataka kuendelea kuzichota noti za Fernandes. Kwake pesa ndiyo kila kitu.
Lakini usishangae sana. Jina la Cesar ni la Kihispaniola. Kwa Kihispaniola, Cesar na Caesar yana maana moja tu ambayo kwa Kiswahili ni Kaisari. Nadhani Cesar ameamua kufuata mambo ya Kaisari bila ya kujali sana ndoto zake za kuichezea Brazil Kombe la Dunia katika ardhi ya kwao Brazil.
Kocha wake, Fillipe Scolari mara kadhaa amemtishia kumwacha katika kikosi cha Brazil kitakachocheza Kombe la Dunia. Lakini bado namwona Cesar yupo yupo tu Queens Park Rangers. Anachukua mishahara yake ya mwisho.
Kwa sasa ana miaka 34. Alizaliwa mwaka ambao Askari wa Tanzania walikuwa wakirejea kutoka katika vita vya Idd Amin nchini Uganda, 1979. Nadhani anaona ni bora akose Kombe la Dunia kuliko kukosa mishahara yake ya mwisho mwisho.
Ndivyo wanasoka wa kisasa walivyo. Pesa kwanza. Ni huyu huyu Kaisari wetu Cesar ndiye aliyewachekesha waandishi wa habari wa Uingereza baada ya kudai kwamba alikuwa ametua QPR kutoka Inter Milan na ndoto yake ilikuwa ni kubeba ubingwa wa England.
QPR wangebeba ubingwa wa England wakati Man City wako wapi? Chelsea wako wapi? Man United wako wapi? Liverpool wako wapi? Lakini mbele ya pesa ni rahisi kudanganya. Yuko wapi yule mwanasiasa aliyedanganya kuwa angejenga daraja katika eneo ambalo halikuwa na mto wala mabonde?
Hata hivyo si kila mmoja anaishi kama Cesar. Mshambuliaji Loic Remy amehama kwa mkopo kwenda Newcastle kwa ajili ya kucheza soka la kishindani zaidi. Lakini Cesar amemkumbatia Kaisari mwenzake.
Bahati nzuri jina lake linafanana kabisa na yule kiongozi wa Warumi. Yule aliitwa Gaius Julius Caesar wakati yeye anaitwa Julio Cesar Soares Espindola. Wote ni wale wale tu. Mwache Kaisari amkumbatie Kaisari mwenzake. Hakuna tunachoweza kufanya.
No comments:
Post a Comment