![]() |
NAKIPENDA kisa hiki. Kinanisisimua sana. Ilikuwa mwaka 1974, katika pambano la Ligi Kuu Uholanzi baina ya Ajax Amsterdam na Rhoda, shabiki mmoja wa Ajax aliamua kuondoka zake uwanjani wakati wa mapumziko.
Waandishi wa habari walipomuhoji sababu za kuondoka, alidai kwamba binafsi alihisi kuwa alikuwa anawadhulumu wachezaji wa Ajax kwa sababu ya kiwango cha hali ya juu cha soka walichomwonyesha hakikufanana na bei ya tiketi aliyonunua. Alihisi amelipa pesa kidogo kuliko soka aliloonyeshwa.
Mei 2012, Brendan Rodgers, aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow na kwenda sehemu ya watu maalumu. Akapanda ndege kwenda Austria kutembelea kambi ya timu ya taifa ya Hispania iliyokuwa inajiandaa na fainali za Euro 2012.
Ilikuwa safari yake binafsi. Safari ya shujaa. Safari ya kujaribu kufanya anachokiamini katika falsafa zake za soka. Hispania ilikuwa imejaza wachezaji wa Barcelona. Lakini hapo hapo ilikuwa inacheza soka katika falsafa ya kipekee duniani.
Wachezaji wake karibu wote walikuwa wafupi, kasoro Sergio Busquet, Fernando Torres na labda Gerrard Pique. Wengine wote walikuwa wanamfikia begani. Lakini walikuwa wana uwezo mkubwa.
Umahiri wao na ubora wao ni kwamba walikuwa wana uwezo mkubwa wa kupasiana mpira kwa kasi, kwa uhakika. Adui asingeweza kuupata na kama angeupata, wachezaji wao wangeusaka kwa haraka na kuurudisha katika himaya yao.
Ambacho Rodgers alikiona na kukichukua, ndicho alichoenda kukiendeleza Swansea, sasa amekipeleka Liverpool. Wachezaji wafupi, wenye kasi, wanaopasiana kwa haraka na wenye hamu ya mpira.
Tofauti yake na kile alichokichukua katika kambi ya Vincent Del Bosque, ni kwamba Rodgers anataka Liverpool icheze kwa haraka zaidi katika eneo la mwisho tofauti na Barcelona au timu ya taifa ya Hispania.
Darasa lake bado halijatimia, lakini robo tu ya alichokifanya ungeweza kuona katika dakika 18 za pambano la Anfield ambalo Arsenal waliteketea kirahisi. Liverpool walikuwa wanapiga pasi za haraka na kasi kubwa.
Kupiga pasi na kupenya halikuwa tatizo, lakini nilikuwa nacheka peke yangu jinsi ambavyo Liverpool walikuwa hawawapi Arsenal nafasi ya kucheza. Walikuwa wanawapa presha ya kuwarudishia mpira pindi walipoupoteza.
Staili hii inaitwa ‘Pressing Game’. Mfalme wake hasa ni Pep Guardiola. Inakera na kuudhi. Katika mechi za Arsenal na Barcelona ungeweza kuona Samir Nasri, Cesc Fabregas na Jack Wilshere wakishindwa kabisa kucheza aina yao ya soka walilozoea.
Kama Barcelona wangeupoteza mpira, Xavi, Andres Iniesta na Lionel Messi, wangeenda kukaba kwa kasi. Ukifanikiwa kupenyeza pasi wanakuacha na kumvamia uliyempasia. Sekundu chache zinazofuata wanaupata tena na kuanza kupasiana.
Ndicho kilichomkumba Mesut Ozil siku ile. Alikuwa akipata mpira anataka aachiwe nafasi ya kutafakari na kuuchezea. Liverpool walikuwa hawampi nafasi hiyo. Mabao mawili yalitokea kwake.
Ni kitu hiki hiki ndicho kiliwafanya vigogo wapate shida kukabiliana na Swansea ya akina Joe Allen, Nathan Dyer na Wayne Routledge. Nilikuwa najiuliza, vipi kama falsafa ile aliyoiiba vema katika kambi ya Hispania ingepata timu yenye uwezo wa kipesa kama Liverpool?
Ndicho unachokiona kwa sasa. Ndio maana Rodgers alikuwa anatamani kulia wakati Luis Suarez akikazania kwenda Arsenal Agosti mwaka jana. Ufupi na wepesi wa Suarez ndio msingi wa falsafa yake. Ndio maana aliwauza akina Andy Carroll na Jonjo Shelvey. Wachezaji warefu hawawezi kupasiana kwa haraka na kupenya. Katika timu yake na falsafa yake, wachezaji warefu wataishia katika safu ya ulinzi tu kama Martin Skrtel.
Falsafa hii bado haijaiva. Kama ikiiva watu tutaanza kutafutana. Zile dakika 18 za mechi ya Anfield dhidi ya Arsenal zitatokea mara nyingi sana. Kama unakumbuka, hata Manchester City walipata wakati mgumu sana kucheza na Liverpool pale Etihad.
Juni 2011, Rodgers alikuja Tanzania kupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangia mfuko mmoja wa matatizo ya kansa nchini Uingereza. Mama yake na baba yake walikufa kwa kansa. Alifanikiwa kufika kilele cha kibo. Kushuka kwake ilikuwa rahisi.
Ni kama timu anayoitengeneza kwa sasa. Anajaribu kuipandisha mlima kwa nguvu zake zote. Lakini timu ikikubali, yeye atakuwa anakaa katika benchi tu akiitazama falsafa yake inavyoshuka mlima.
Ni mashabiki wangapi wa Liverpool walikuwa hawampendi wakati amechukua timu na wakawa wanasema Liverpool si saizi yake?
Lakini taratibu anaanza kushuka mlima kama alivyoshuka katika Mlima Kilimanjaro. Itakapofika wakati huo, hata mimi mwenyewe nitasafiri kwenda Liverpool kuitazama na wakati huo nadhani haupo mbali.
Kuitazama Liverpool itakuwa ni sawa na kumtazama Cleopatra wakati anaoga.
Nitaupita mnara wa Bill Shankly na kwenda kukaa jukwaa la Spion Kop. Kama kweli falsafa ya Rodgers itakuwa imekubali haswa, basi nitaondoka wakati wa mapumziko. Nadhani nitakuwa nawadhulumu wachezaji wa timu hiyo kama shabiki wa Ajax alivyohisi anawadhulumu wachezaji wa Ajax.
No comments:
Post a Comment