Thursday, 27 February 2014

Mholanzi apewa Stars, Kim alamba mil 160




SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetimua benchi zima la ufundi la Taifa Stars huku likimpa notisi ya mwezi mmoja kocha mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen huku Rais wa TFF, Jamal Malinzi akitarajiwa kumtangaza kocha mpya Mholanzi leo Alhamisi.
Licha ya kupewa notisi hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo mwajiri wa Poulsen, italazimika kumlipa mshahara wa miezi sita kocha huyo kwa mujibu wa mkataba wake endapo utasitishwa ukiwa na zaidi ya miezi sita. Kim atalipwa mshahara wa miezi sita ambao ni dola 102,000 sawa na Sh162 milioni.
Habari za ndani kutoka TFF zinaeleza kuwa, kocha atakayerithi mikoba ya Poulsen ni raia wa Uholanzi na mchakato wa kumpata ulianza tangu uongozi wa Malinzi uingie madarakani.
Juzi Jumanne, TFF ilitangaza kikosi cha Stars bila kumshirikisha Poulsen ambaye jana Jumatano alionekana katika ofisi za TFF akisaini baadhi ya fomu akiwa sambamba na Malinzi na Evodius Mtawala ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Wanachama.
Mwanaspoti linajua kwamba katika benchi la Stars aliyenusurika katika timuatimua hiyo ni mtunza vifaa, Fredy Chimela huku kocha msaidizi Sylvester Marsh ambaye amelazwa Hospitali ya Ocean Road, na meneja Taso Mukebezi wakitupiwa virago.
“Poulsen amepewa barua ya kusitishiwa mkataba ila wamempa notisi ya mwezi mmoja. Mambo mengine ya kisheria yatafikiwa mwafaka muda wowote,” kilisema chanzo chetu ndani ya TFF.
Marsh ambaye amekuwa na timu hiyo kwa miaka mingi, jana Jumatano alitarajiwa kufanyiwa uchunguzi mwingine baada ya kufanyiwa upasuaji wa awali wa koo.
Wakati huohuo, Poulsen amegomea ofa ya kuwa mkurugenzi wa ufundi aliyopewa na TFF wakati wa mchakato wa kuvunja mkataba wake.
Taarifa kutoka ndani ya TFF imesema kuwa, wakati shirikisho hilo likijadiliana na Kim kuhusu kuvunja mkataba wake wa kuifundisha Taifa Stars, walimpa ofa ya kuwa mkurugenzi wa ufundi ambayo sasa inashikiliwa na Salum Madadi kwa muda baada ya Sunday Kayuni kumaliza mkataba wake lakini kocha huyo amekataa.osi mmoja wa TFF alisema mara baada ya Kim kupewa ofa hiyo aligoma kuchukua madaraka hayo ambapo shirikisho hilo liliamua kubaki katika mjadala wa kuvunja mkataba wake uliotakiwa kumalizika Mei mwakani

No comments:

Post a Comment