Saturday, 25 January 2014

TFF YAMTIBUA MZUNGU WA YANGA

Kocha Mkuu wa Yanga Muholanzi, Hans Van Der Pluijm


KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Van Pluijm, amepata taarifa za kusimamishwa kwa Emmanuel Okwi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini akatikisa kichwa kwa masikitiko na kusema hajawahi kuona uamuzi wa ajabu kama huo.
Akizungumza na Mwanaspoti jana Ijumaa alfajiri baada ya kutua kwa kikosi chake jijini Dar es Salaam kikitokea kambini Uturuki, alishtushwa na taarifa za kuzuiwa kwa Okwi na Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji na kusisitiza hajaona sababu ya msingi.
“Sijaona hoja ya msingi kutoka kwa TFF, nafikiri hapo wameonyesha wasiwasi katika kufahamu utaratibu kwa wote waliohusika kufanya uamuzi, unawezaje kumzuia mchezaji ambaye amepata hati ya uhamisho ambayo inaidhinishwa na Fifa?” Alihoji Pluijm.
“Si uamuzi sahihi kabisa, unapomsajili mchezaji na kupewa hati ya uhamisho tafsiri rahisi ni kwamba kila kitu hapo kimekamilika na mchezaji husika ni halali kuchezea timu yako, sijafurahishwa na hizo taarifa. Ni mbaya kwetu kama Yanga kwani Okwi alikuwa katika mipango yetu kuanzia mchezo dhidi ya Ashanti United.
“Hakuna shida ingawa ni pigo kumkosa Okwi, katika kikosi changu; kuna nyota wa kutosha na tutaangalia nani tumpe majukumu ya Okwi nafikiri hilo ndiyo tunalotakiwa kulifanya sasa ingawa kama tungekuwa na Okwi nadhani tungekuwa na nguvu zaidi kutokana na uwezo wake,”alisisitiza kocha huyo akionyeshwa kukerwa vilivyo na uamuzi huo.
TFF imesimamisha usajili wa Okwi ikitaka maelekezo kutoka Fifa ambayo awali ilimwidhinisha mchezaji huyo kuichezea SC Villa ya Uganda ambayo ilimuuza Yanga.

No comments:

Post a Comment