MREMBO Coleen Rooney anasubiri kwa hamu kubwa mazungumzo ya mkataba mpya wa mumewe, Wayne Rooney wa kuendelea kubaki klabu Manchester United. Taarifa zinabainisha kwamba mchezaji huyo anaandaliwa mshahara wa pauni 300,000 kwa wiki.
Mrembo huyo anadaiwa kumtaka mumewe asaini mkataba mwingine wa miaka mitano wa kubaki Manchester ili kuwasubiri watoto wao; Kai, 4, na Klay mwenye umri wa miezi minane kuwa na umri mkubwa kabla ya kuhama.
Mkataba ambao Manchester United inataka kumpa Rooney una thamani ya pauni 65 milioni na utamfanya straika huyo kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi England.
Kwa sasa analipwa kiwango sawa na mchezaji mwenzake wa Manchester United, straika wa Kidachi, Robin van Persie, pauni 250,000 kwa wiki.
Rafiki wa mrembo Coleen, 27, anasema: “Kitu kikubwa Coleen hataki wahame kutoka Kaskazini Magharibi na jambo hilo ni muhimu sana kwa Wayne. Hataki kuondoka eneo hilo na kutokana na kupokea ofa nzuri ya pesa nyingi anaamini hilo ni jambo muhimu akabaki klabu hapo.”
Manchester United imeipiga marufuku Chelsea kwamba isithubutu kumfuatilia straika wao huyo kwa sababu hawawezi kumuuza kwa wapinzani. Real Madrid pia inafukuzia saini ya staa huyo wa Old Trafford.
Lakini, Coleen hayupo tayari kuona watoto wake wakihamia London wangali wadogo hivyo, ukiweka kando Hispania. Anachotaka yeye waendelee kubaki Manchester hadi hapo baadaye.
Familia hiyo inaishi Prestbury, Cheshire, na wazazi wa Coleen, Colette na Tony wanaishi umbali wa maili 50 huko Formby, Merseyside, karibu na familia ya akina Rooney.
Coleen amesema Rooney, ambaye alijiunga na Manchester United akitokea Everton mwaka 2004, atapata shida sana kutulia kama atacheza bila ya sapoti ya familia zao.
Lakini, kuna mtazamo tofauti wakati kocha David Moyes akihaha na kuafiki mshahara wa pauni 300,000 kwa Rooney, wachambuzi wa soka wanadhani Manchester United inapaswa kulichukulia kwa hadhari suala la mchezaji huyo.
Staa huyo tayari anaonekana kuiringia Manchester United kwa kuweka kando suala la kusaini mkataba mpya akisubiri hatima ya klabu mwishoni mwa msimu kama itakuwa ndani ya nne bora na kama klabu hiyo itafanya usajili wa mastaa wapya.
Moyes amemnasa Juan Mata kutoka Chelsea, lakini hilo bado haliwezi kuwa dawa ya kumbakiza Rooney Old Trafford kutokana na matakwa ya staa huyo kwamba anataka wachezaji makini waongezwe kikosini.
Kwa sasa kikosi cha Manchester United kinahitaji mabeki wazuri, viungo wazuri na mshambuliaji mpya mzuri. Wachezaji hao wakifika huenda timu itafufuka na kuwa tishio zaidi. Lakini, kitu cha kukumbuka ni kuwa kupata timu kama ya awali ya kushitua Dunia kutahitaji muda kiasi na umakini mkubwa. Anza na mfano huu;
Januari 3 mwaka huu, straika mahiri wa Borussia Dortmund, Robert Lewandowski alisafiri kwenda Munich, Ujerumani na akasaini mkataba wa awali na wapinzani wao wakubwa kwenye Bundesliga, Bayern Munich.
Bado hajahamia rasmi kwenye timu hiyo lakini atatua baada ya msimu huu. Suala kwamba Lewandowski angeondoka akiwa huru haikuwa habari, kila mtu alifahamu hilo.
Kitu pekee kilichokwamisha mpango huo mpaka sasa ni ukweli kwamba Borussia Dortmund hawakutaka kumuuza, kisa, walimwona kuwa ni staa wao na walitaka abaki klabuni hapo baada ya Mario Gotze kwenda Bayern Munich.
Borussia Dortmund iligoma kupoteza wachezaji wawili kwa mara moja licha ya kutambua ukweli kwamba mapema tu, Lewandowski alionyesha dhahiri hataki kubaki na timu hiyo.
Kitu hiki kinafanana na suala la Rooney. Mwishoni mwa msimu uliopita, staa huyo alielezwa kwamba anataka kuondoka. Jambo hilo bado lipo kwenye akili yake kutokana na sasa kusuasua kusaini mkataba mpya japo Manchester United wanaamini kwa kutumia pesa watafanikiwa kumbakiza.
Borussia Dortmund waliamua kumbakiza Lewandowski katika klabu hiyo mpaka mkataba wake utakapomalizika kabisa, hawakujali kwamba watampoteza akiwa huru yaani watakula hasara.
Suala la Gotze na Lewandowski, halikuwa hivi hivi tu, wachezaji hao walifahamu kuwa wakihamia Bayern Munich watakusanya vikombe na fedha, walifahamu kama wangebaki Borussia Dortmund wasingepata fedha nyingi. Mashabiki wa Borussia Dortmund wamekasirika lakini ukweli unabaki pale pale kwamba wachezaji wamefanya uamuzi ambao wanaamini una manufaa kwao.
Ukimtazama Matthew Le Tissier, yeye aliamua kuchezea Southampton kwa mapenzi matokeo yake akashindwa kupata ubingwa wowote. Huenda Le Tissier ni tofauti na Lewandowski, yeye alipenda klabu yake Southampton na alijiona mwenye furaha, kwa hiyo akatulia. Leo kuna watu wanafurahia uaminifu wa Le Tissier, lakini wengine wanamlaumu kwa kukosa mtazamo mpya.
Lewandowski asingefanya jipya
Swali kwa Borussia Dortmund ni je, walikuwa na sababu za kumfanya Lewandowski abaki kwenye klabu? Kumbakiza kusingesababisha mabadiliko makubwa klabuni hapo katika ushindani wa ligi ya ndani.
Bayern Munich watakapokuwa na Lewandowski watakuwa na faida kwa sababu kwanza straika huyo atataka kuifanyia kitu klabu yake mpya tofauti na kama angeendelea kubaki Dortmund.
Kitu hiki kinataka kufanana na Rooney. Manchester United inaweza kushinda vita ya kumbakiza Rooney Old Trafford, lakini je mchezaji huyo ataendelea kubaki na moyo wa kuichezea timu hiyo.
Dortmund kama ingemuuza Lewandowski kwenye majira ya kiangazi mwaka jana ingetengeneza zaidi ya Euro 20 milioni.
Wangetumia pesa hiyo kusaka mshambuliaji mwingine mzuri zaidi ambaye angewapa faida. Kitu pekee ambacho Dotmund wanashikilia ni kuwa bado wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwamba kuwa na mshambuliaji wa aina ya Lewandowski kutawafanya kuwa tishio.
Anaweza kuwasaidia kwa sasa lakini ukweli unabaki pale pale kwamba Dortmund wanakubali kuendeshwa na moyo kuliko akili. Wamesahau kuwa muda unakwenda na watamtoa mchezaji huyo bure.
Rooney ni kama Lewandowski
Suala la Lewandowski pia lilikuwa likiangaliwa kwa karibu na Manchester United ambayo ilitaka kumnunua mchezaji huyo kuchukua nafasi ya Wayne Rooney ambaye alikuwa mbioni kuondoka. Rooney bado yupo lakini mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu ujao yaani Juni 2015.
Mtu anaweza kujiuliza ni kwa kiasi gani Rooney aliumia wakati timu yake ilipochapwa mabao 3-1 na Chelsea wikiendi iliyopita. Maumivu yake hayaishii kwenye mchezo huo pekee, anaumia kwa sababu anafahamu katika siku za karibuni hawatakuwa na uwezo wa kuwafunga wapinzani wao kirahisi.
Anafahamu wazi kuwa kwa sasa mambo mawili yanatendeka kwa Chelsea, huenda wamefikia kiwango cha juu au wanakaribia, hivyo kuwashusha itakuwa ni hadithi nyingine.
Kitu kingine kinachomuumiza ni ukweli kuwa kwa sasa timu yake inatakiwa kuchongwa upya, na suala hilo linaweza kuchukua zaidi ya msimu mmoja. Kibaya ni kwamba kengele ya miaka nayo inagonga, Oktoba mwaka huu anatimiza miaka 29, huenda kwa sasa ana mawazo kama ya Robin van Persie, alipoona kengele ya miaka yake hapo 2012 akiwa Arsenal, aliamua kutimkia Manchester United kuchukua chake mapema.
‘Chukua chako mapema’ ni msamiati mbaya kwa mashabiki na klabu, lakini msamiati huo una maana kubwa kwa wachezaji. Rooney alishinda tuzo ya PFA mwaka 2010 akicheza kama mshambuliaji wa kati na hivi karibuni alisisitiza kuwa hiyo ndio nafasi anayoipenda zaidi. Kizuri ni kwamba Jose Mourinho anamtaka akacheze kikosi kwake kama mshambuliaji wa kati akiwa Chelsea na hatakuwa na kazi kubwa kama anayofanya Manchester United kwa sasa.Kocha wa Manchester United, Moyes amekuwa akijaribu kumtuliza Rooney kwa kumwambia angoje kuvunja rekodi ya Bobby Charlton ya kuwa mfungaji namba moja wa klabu, lengo likiwa ni kumbembeleza abaki kwenye klabu. Lakini je, Rooney anajali kuwa mpachika mabao namba moja wa Old Trafford?
Mabao yake yanaweza kuongezeka hata akiwa Chelsea, huko atakimbiza rekodi ya Alan Shearer, ambaye alifunga mabao 260 kwenye Ligi Kuu England.
Anaweza kukimbiza rekodi hiyo akiwa Chelsea kama mshambuliaji wa kati kuliko kuwa mshambuliaji wa nyuma ya Van Persie, Manchester United.
Sababu nzuri za kumuuza
Rooney amebakiza miezi 12 tu, kabla ya kuwa na uhuru wa kusaini mkataba wa awali na Chelsea. Itakuwa ni jambo la busara kwa Manchester United kumuuza kabla jambo hilo. Hizi ndio sababu za kumuuza: Kwanza Man United wameshaona kiwango chake mpaka mwisho, miaka mitano ijayo hawezi kuwa bora kama miaka mitano ya nyuma.
Mbili; Kuna wasiwasi huenda Manchester United wasishiriki kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakimuuza watapata fedha za kununua mchezaji mpya, tena chipukizi wenye uwezo wa kuifanya timu hiyo kuwa bora zaidi.
Tatu: Kumuuza mchezaji nyota si mwisho wa timu bali ni mwanzo wa ustawi. Kwa mfano, Arsenal kwa sasa ni bora kuliko alipokuwepo Van Persie.
Liverpool ilimuuza Fernando Torres kwenda Chelsea watu walilalamika, lakini sasa wameopoa kifaa cha ajabu, Luis Suarez na Liverpool imekuwa tishio pengine kuliko Torres alipokuwa na kikosi hicho cha Anfield.
No comments:
Post a Comment