Saturday 18 January 2014

MDACHI WA YANGA AVUNA MAMILIONI




KOCHA mpya wa Yanga Mdachi Hans Van Der Pluijm, atavuna fedha ya maana Yanga ambayo ni Sh.96 milioni katika kipindi cha miezi sita alichosaini kuifundisha timu hiyo iliyoko kambini mjini Antalya,Uturuki.
Kocha huyo alisaini mkataba huo baada ya aliyekuwa kocha wao Ernest Brandts kufungashiwa virago kwa madai ya kuwa timu hiyo kushuka kiwango. Atakuwa akilipwa dola 10,000 kwa mwezi ambazo ni Sh 16 milioni.
Habari kutoka ndani ya Yanga, zinadai kuwa kutokana na bajeti yao waliamua kumchuku Pluijm ingawa bado mawazo yao ni kumpata kocha wa Gor Mahia, Bobby Williamson au Kocha wa Harambee Star, Mbelgiji Adel Amrouche.
Katika mazungumzo ya awali kocha wa Harambee Stars,Amrouche alionyesha nia wakati Williamson hakuonyesha nia ingawa uongozi wa Yanga ulikuwa ukimfuatilia kwa karibu sana.
“Tumempa miezi sita mpaka hapo tutakapomaliza ligi ndipo tutaangalia mipango mingine, tulitoa ofa hiyo kutokana na bajeti yetu, kuna walioomba kwa kukubali ofa tuliyoitangaza na wengine waliona ofa hiyo ni ndogo, Pluijm ni kocha ambaye tunaamini atatusaidia katika kipindi hiki cha mwisho wa ligi,” alisema.
Baada ya kumalizana na viongozi wa Yanga, Pluijm raia wa Uholanzi aliondoka nchini kuifuata timu hiyo iliyoweka kambi yao nchini Uturuki ikijiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Kabla ya kumpata kocha huyo, timu hiyo ilikuwa chini ya Kocha Msaidizi Boniface Mkwasa aliyechukuwa nafasi ya Felix Minziro na Juma Pondamali ambaye ni kocha wa makipa akichukuwa mikoba ya Razak Siwa ambao wote walitimuliwa. Yanga wamemwambia kocha huyo mpya kwamba wanataka atetee ubingwa wao wa Bara, wacheze soka ya maana na aipeleke timu hiyo angalau hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

No comments:

Post a Comment