Sunday, 26 January 2014

Juan Mata, Van Persie, Rooney ni hatari Man U




MANCHESTER, ENGLAND
ITAKUWA balaa tena. Itatisha kwa mara nyingine. Ndivyo Manchester United inavyotabiriwa kufufuka baada ya jana Ijumaa kukamilisha uhamisho wa kiungo mchezeshaji wa Chelsea, Juan Mata.
Lakini hapo hapo imetabiriwa kuwa Mata si suluhisho la matatizo yote ya Manchester United katika msimu huu ambao wameonekana kuwa ovyo kupita kiasi.
Kiungo wa zamani wa Liverpool, Jamie Redknapp ambaye sasa ni mchambuzi wa soka Uingereza amedai kwamba ujio wa Mata ambao utamuunganisha na wakali Wayne Rooney na Robin van Persie katika safu ya ushambuliaji ya Old Trafford utasababisha hatari kwa timu pinzani.
“Baada ya msimu wa ovyo, mashabiki wa Manchester United wamekuwa wakimtafuta shujaa. Kwa Juan Mata nadhani watakuwa wamempata shujaa. Baada ya kichapo cha Sunderland, Mata ni alama ya matumaini Old Trafford.” Alisema Redknapp.
“Ni mchezaji wa ajabu, ana tabia njema na anaweza kupiga pasi murua.  Ni mshindi lakini pia usisahau kuwa Mata siyo suluhisho la matatizo yote ya Manchester United. Kuwasili kwake ni onyo kwa wapinzani lakini bado kuna matatizo Manchester United.” Aliongeza Redknapp.
“Manchester United inabidi iondokane na wachezaji wengi ili warudi juu na wanahitaji wachezaji wenye ubora kama sita hivi.Wachezaji kama Patrice Evra, Nemanja Vidic na Rio Ferdinand wataondoka katika kipindi cha majira ya joto, ni wakati wa kuanzisha mradi mwingine. Lakini hata hivyo usajili wa Mata ni mwanzo mzuri.”
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho alithibitisha kiungo huyo kutimkia Manchester United baada ya kupokea ofa nzuri.
Alisema: “Mambo yanakwenda vizuri kabisa. Tumemruhusu Mata kusafiri kwenda kufanya vipimo vya afya. Mchezaji anastahili heshima na kwasababu ofa ni nzuri tumemruhusu.”
Mata alitarajiwa kusaini mkataba wa miaka minne na atalipwa Pauni 140,000 kwa wiki huku akiwa mchezaji ghali zaidi katika rekodi ya Manchester United akisajiliwa kwa Pauni 37 milioni.
Ana kazi kubwa ya kurudisha matumaini ya mashabiki wa Manchester United ambayo mpaka sasa inashika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu England wakiwa wameachwa kwa pointi 14 na vinara Arsenal.

No comments:

Post a Comment