Monday 20 January 2014

COASTAL WAWEKA HESHIMA OMAN




KOCHA na mchezaji wa zamani wa Simba, Talib Hilal ametamka kuwa kwa jinsi alivyoiona Coastal Union nchini Oman kwenye mechi zao na mazoezi wanayofanya Muscat, anaamini ikirudi nchini itakuwa tishio kwa klabu za Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili.
Kauli hiyo, imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Coastal, Hemed Hilal ‘Aurora’ kuwa, kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake nchini Oman, kimezivutia timu nyingi.
Talib, ambaye anaishi nchini humo na kuifundisha timu ya Taifa ya soka la ufukweni Oman, amekuwa akihudhuria mazoezi ya Coastal ambayo asubuhi hufanya kwenye Uwanja wa Chama cha Soka Oman na jioni kwenye uwanja wa klabu ya Seeb.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Oman, Talib alisema: “Tunao ugeni wa Coastal hapa, nimefika mazoezini na kuwaona kwa kweli wako vizuri kiuchezaji pamoja na mchanganyiko wa wachezaji waliona, wa damu changa na wazoefu wataisaidia timu.”
“Mbali na hilo, wana morali na hamu ya kufanya vizuri,” alisema Talib aliyekuwa mwenyeji wa Simba ilipoweka kambi Oman mwaka jana.
“Wanacheza kitimu na safu zote ziko vizuri,” alisisitiza Talib ambaye aliishuhudia Coastal kwa mara nyingine ilipocheza na Seeb Club na kutoka suluhu.
Katika mchezo huo, Seeb ilikuwa na wachezaji wawili Watanzania kutoka Ruvu Shooting straika, Elius Maguli na kiungo, Ally Kani.
Talib alikwenda mbali zaidi na kueleza: “Kwa hiki wanachokifanya Coastal hapa Oman, imani yangu watafanya vizuri zaidi mzunguko wa pili kwa sababu wa mazingira waliopo.”
Kwa upande wa Aurora alisema: “Tulitarajia kucheza mechi nne ambazo tumezikamilisha rasmi, lakini kutokana na kiwango walichokionyesha Coastal hapa kimezivutia klabu nyingi ambazo wanahitaji mechi za kirafiki.”
Coastal imeweka kambi Oman msimu huu kwa muda wa wiki mbili na mechi walizocheza ni pamoja na hiyo ya suluhu dhidi ya Seeb pamoja na waliyofungwa na  Fanja 1-0 na nyingine walizifunga Al Mussannah Club mabao 2-0 na Oman Club mabao 2-0

No comments:

Post a Comment