Friday, 6 December 2013

WANASOKA NYOTA DUNIANI WANAVYOMLILIA MANDELA



JUZI Alhamisi usiku, Nelson Mandela ambaye ni Rais wa zamani wa Afrika Kusini alifariki Dunia nyumbani kwake Johannesburg baada ya kupambana kwa muda mrefu na ugonjwa wa mapafu.
Ugonjwa huo ulimsumbua sana kiasi cha kusababisha apelekwe hospitali mara nne katika kipindi cha miezi tisa ya hivi karibuni.
Kifo chake kimetokea akiwa na umri wa miaka 95 na kuwaachia majonzi makubwa watu wa Afrika Kusini na Dunia kwa ujumla wakiomboleza msiba huo mkubwa.
Kupambana na kuifanikisha Afrika Kusini kuandaa fainali za Kombe la Dunia 2010 ilikuwa ni moja ya mapenzi ya kiongozi huyo katika michezo ukiweka kando historia yake kwamba alikuwa bondia wa ridhaa enzi zake za ujana.
Mpenzi wa soka
Jitihada na mapenzi yake kwenye mchezo wa soka yalikuwa sababu kubwa ya fainali za Kombe la Dunia kufanyika Afrika Kusini, ikiwa ni mara ya kwanza fainali hizo kuchezwa kwenye ardhi ya Bara la Afrika tangu zilipoanzishwa mwaka 1930.
Katika juhudi zake za kuondoa ubaguzi, Mandela alitumia michezo kuunganisha nchi hiyo, ambapo alisababisha kufanyika kwa fainali za Kombe la Dunia la mchezo wa rugby nchini humo mwaka 1995 na fainali za soka za Mataifa ya Afrika mwaka 1996.
Baada ya kufanikiwa kwa michuano hiyo, Mandela aliendelea kusapoti juhudi za kutumia michezo na hasa soka na hivyo nchi hiyo kufanikiwa kuandaa michuano mingine mikubwa ikiwa fainali za soka za Kombe la Dunia zinazoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).
Baada ya kushindwa kupata uenyeji wa fainali hizo mwaka 2006, miaka minne baadaye Afrika Kusini ikiongozwa na Mandela iliweza kushinda na hivyo kupata wenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2010, ambalo lilifanyika kwa mafanikio na Hispania kuibuka mabingwa.
Uwanja waitwa jina lake
Uwanja wa soka wa Port Elizabeth ambao ulitumika kwa mechi nyingi kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, ulipewa jina la Nelson Mandela Bay na hilo limekuja baada ya kufanikiwa kwenye kuzifanya fainali hizo kufanyika nchini humo.
Afrika Kusini inajivunia kuwahi kumpata kiongozi ambaye hakuvunjika moyo kutokana na kufungwa jela au mateso aliyoyapata katika harakati za kisiasa, badala yake alikuwa mtu mwenye kuhamasisha umoja na amani jambo ambalo limempa heshima kubwa duniani kote.
Wanasoka mbalimbali duniani kote wameguswa na kifo cha kiongozi huyo, aliyeiwezesha Afrika kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia, lakini akiwa amekufa siku moja kabla ya kufanyika kwa droo ya makundi ya fainali nyingine za Kombe la Dunia za mwakani zitakazochezwa Brazil.
Yaya Toure amlilia
Kiungo wa Ivory Coast na Manchester City, Yaya Toure, hakusita kuonyesha kuguswa na msiba wa Mandela na kuweka ujumbe maalumu katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter uliosomeka hivi: “Shujaa ni mtu ambaye anajitolea maisha yake kwa ajili ya manufaa makubwa bila ya kujijali mwenyewe atapatwa na kitu gani.
Dunia imepoteza shujaa na Afrika imepoteza baba...RIP Mandela.”
Pienaar haamini, Pele anena
Taarifa za kifo cha Mandela zimemshitua kiungo wa Afrika Kusini, Steven Pienaar na kusema kwamba haamini kama ripoti hizo ni za kweli kama Madiba amefariki Dunia.
Wakati Pienaar akishikwa na kigugumizi juu ya taarifa hizo, gwiji la Brazil, Pele alisema kwa sasa ni wakati mwafaka wa kuendeleza yale mazuri yake kwa vitendo ili kuendelea kumkumbuka kiongozi huyo kwa ushujaa wake.
Ronaldo, Blatter waomboleza
Kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, Cristiano Ronaldo alikutana na Mandela na kumpelekea jezi ya timu ya taifa ya Ureno iliyokuwa na Namba 16. Kwa dakika chache aliketi pamoja na kiongozi huyo na kupiga picha naye, Ronaldo amevuna vitu vingi na hivyo alionyeshwa kuguswa kwake kwa kifo hicho na kumshukuru Mandela kwa ushujaa wake na kuwa mfano bora.
Rais wa Fifa, Sepp Blatter, aliungana na jamii nyingine kutoka kwenye familia ya mchezo wa soka kutoa rambirambi kwa kiongozi huyo na kusema daima ataendelea kuheshimu jitihada za Mandela ambaye atabaki kuwa mpambanaji wa haki za binadamu katika kizazi chake.
Pique, Adebayor wamlilia

Beki wa Barcelona, Mhispaniola Gerard Pique, anasema fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 zitabaki kwenye kumbukumbu zake daima na hii si kwa sababu nchi yake ya Hispania ilinyakua ubingwa, bali ni jinsi Mandela alivyoweza kufanya kitu hicho kutokea na kufanyika kwa mafanikio makubwa kwenye ardhi ya Afrika.
Wakati Pique akimshukuru Mandela kwa hilo, straika wa Togo na Tottenham Hotspurs, Emmanuel Abedayor, ambaye aliwahi kukutana ana kwa ana na kiongozi huyo, alisema hakika Mandela atabaki kuwa kiongozi bora wa nyakati zote kutokana na ujasiri wake na uhamasishaji na kwamba ameacha sifa ambayo itadumu karne kwa karne.
Kompany, Gyan na Bassong nao wamlilia
Kwenye taarifa yake, nahodha wa Manchester City, Mbelgiji Vincent Kompany, alisema moja ya mambo anayoyapenda kwenye maisha yake ni kusoma vitabu vinavyomhusu Mandela na jinsi alivyoikomboa Afrika Kusini.
Baada ya kupata taarifa za kifo cha kiongozi huyo, Kompany anakiri kuishiwa maneno yanayofaa kumzungumzia Mandela hasa kutokana na mambo aliyoifanyia Dunia na kuwa mfano mkubwa.
Beki Sebastien Bassong amesema daima ataendeleza mapenzi yake kwa Madiba na kwamba kiongozi huyo ni mmoja wa mashujaa wake kwenye maisha.
Straika wa Ghana, Asamoah Gyan, anaeleza furaha ya kuwahi kukutana na Mandela na kusema jambo hilo hakika litabaki kuwa la kipekee kabisa kwake huku akimtakia mapumziko ya amani.
Carrick, Ayew wamzungumzia
Kiungo Mwingereza wa Manchester United, Michael Carrick amemzungumzia Mandela na kusema moja ya hazina kubwa iliyowahi kutokea duniani na kwamba maisha yake yamekatika, lakini heshima yake itabaki daima.
Naye straika wa Ghana na Olympique Marseille, Andre Ayew, anaamini Madiba ni mtu makini zaidi aliyewahi kutokea duniani na hasa kwenye bara la Afrika.
Straika wa Tottenham Hotspura na England, Jermain Defoe, alipokea taarifa za kifo hicho cha Mandela akiwa kwenye ukumbi wa sinema kutika uzinduzi wa filamu inayohusu maisha ya kiongozi huyo wa Afrika Kusini.
Usichokijua
Wengi wameanza kumfahamu akiwa tayari mzee, mvi kichwani na tayari ameanza kuchoka. Hii ni kwa sababu tu, tayari alikuwa na umri wa miaka 71 macho ya wengi yalipoanza kumtambua kwa kuwa ndiyo kwanza alikuwa anatoka jela mwaka 1990.
Lakini, kwenye ujana wake, Nelson Mandela, alikuwa mwenye kimo kirefu, mwili uliojengeka vizuri, bondia na dansa ambaye marafiki zake walikiri kwamba alikuwa kivutio cha mabinti warembo.
Akizaliwa katika familia yenye hadhi ya kifalme kijijini Transkei
Mandela alikuwa mchangamfu na mwenye kujiamini. Maisha ya kifalme si kitu alichokitaka, baada ya kugundua mpango wa kumtaka aoe mara tu atakapomaliza shule, aliamua kutoroka na kukimbilia Alexandra, mji wa watu weusi uliokuwa nje kidogo ya Johannesburg.
Kama ilivyo kwa wanaume wote wa umri wake, mwenye afya alijihusisha na maisha ya wanawake na kwa sababu alikuwa mjini, basi haikuwa tabu kuwapata.
Akifanya kazi kama karani wa mahakama, akihitaji sheria nyakati za usiku kwa lengo la kutaka kuwa mkombozi wa taifa lake, Mandela alipanga katika nyumba iliyokuwa ikimilikiwa na Evelyn Mase, nesi mrembo aliyekuwa binti mdogo kipindi hicho.
Evelyn kwa mdomo wake alikiri kumpenda Mandela siku ya kwanza tu baada ya kukutana, kipindi hicho Mandela akiwa na umri wa miaka 26, alimchumbia mrembo Evelyn aliyekuwa na umri wa miaka 23 na wawili hao walioana Johannesburg .
Historia fupi
Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 kijijini Mvezo, Umtatu, ambayo baadaye ikawa sehemu ya Cape Province. Alipewa jina la Rolihlahla, neno la Xhosa lenye maana ya “msumbufu” kabla ya kutambulika kwa jina la ubini wake, Madiba.
Babu yake aliitwa Ngubengcuka, mtawala wa jamii ya watu wa Thembu. Alikuwa mmoja wa watoto wa mfalme, aliyeitwa Mandela na hiyo ndiyo chanzo cha jina la ubini wake. Kwa sababu Mandela alikuwa ni mtoto pekee wa mfalme kutoka kwa mkewe wa jamii ya Ixhiba.
Baba yake, Gadla Henry Mphakanyiswa, alikuwa chifu. Mwaka 1926, Gadla, alitumuliwa kazi kwa rushwa
Gadla alikuwa mume wa mitara. Alikuwa na wanawake wanne, watoto wanne wa kiume na tisa wa kike, waliokuwa wakiishi vijiji tofauti.
Mama yake Mandela alikuwa ni mke wa tatu wa Gadla, Nosekeni Fanny, aliyekuwa binti wa Nkedama kutoka jamii ya Mpemvu kutoka koo za Xhosa.
Pumzika kwa amani Madiba.

No comments:

Post a Comment