Tuesday, 3 December 2013

SAA 60 ZA MASHAKA MAKUBWA KWA WENGER


Arsene Wenger
LONDON, ENGLAND
ARSENAL imejinafasi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England, imefanya hivyo baada ya kukusanya pointi 31 katika mechi 13 ilizotia timu uwanjani.
Kitendo hicho kinawafanya mashabiki wake kuanza kuzungumzia ubingwa hasa kutokana na kiwango kinachoonyeshwa na timu yao  msimu huu. Timu imekuwa ikishinda mechi zote zilizoonekana zingekuwa kikwazo kwao.
Pamoja na kuongoza ligi kwa pointi nyingi hasa dhidi ya mabingwa watetezi Manchester United, jambo hilo halimfanyi kocha wake,  Arsene Wenger, kuanza kupiga soga za kutwaa ubingwa. Kuna kitu kinamnyima raha Mfaransa huyo.
Wenger amechukia, kisa ratiba inayomkabili kwa sasa. Mfaransa huyo anaamini ratiba ngumu iliyo mbele yao itatibua mbio zao katika kufukuzia ubingwa wa msimu huu.
Vinara hao watakwenda kucheza ugenini na Manchester City ikiwa si zaidi ya siku tatu baada ya kucheza na Napoli, ambayo ni mechi ngumu ya kutafuta kufuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa  Ulaya.
Kwenye mechi hiyo kama Arsenal itakubali kichapo cha mabao 3-0 basi itakuwa imetupwa nje ya michuano kitu ambacho Mfaransa huyo hataki kitokee.
Timu hizo zitakuwa na pointi sawa, lakini Napoli itasonga mbele kwa sababu ya kigezo cha mechi walizokutana wenyewe kwa wenyewe. Kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Emirates, Arsenal ilishinda mabao 2-0.
Tofauti ni saa 60
Mechi hiyo itachezwa usiku wa Jumatano, Desemba 11 nchini Italia. Itakapofika Jumamosi, Desemba 14, Arsenal itakuwa tena ugenini kwa Manchester City kwenye mechi ya Ligi Kuu England itakayofanyika mchana.
Wenger anapasua kichwa, kwa sababu mechi zote hizo ni ngumu na tofauti yake ni saa 60 tu, kwamba watacheza ugenini mechi mbili mfululizo.
Manchester City si timu rahisi inapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani. Imeinyuka sita Tottenham Hotspur, wakainyuka saba Norwich City na kuikandamiza nne Manchester United.
Kinachomuumiza Wenger ni kwamba Arsenal itarudi England asubuhi ya Alhamisi, Desemba 12 na itafanya mazoezi mepesi Ijumaa kabla kusafiri kwenda Manchester jioni.
Manchester City wao watacheza Jumanne usiku, Desemba 10, lakini hawatakuwa na kazi kubwa kwenye mechi hiyo kwani tayari wameshafuzu.
Arsenal haijatoa malalamiko yoyote rasmi kwenda kwa Bodi ya Ligi Kuu kwa sababu tofauti ya siku tatu, ratiba haiwezi kufutwa na haijalishi kama timu itachelewa kusafiri kutoka kwenye kituo kimoja hadi nyingine.
Kutokana na hilo, Wenger analalamika kwamba klabu za England zimekuwa zikikosa sapoti zinapocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati nchi nyingine zimekuwa zikisaidia klabu zao zinazocheza ligi za Ulaya kurekebishiwa ratiba ili kutokuwa na msongamano wa mechi.
Sheria ya siku tatu
Kwenye Ligi Kuu England hakuna mambo ya kubadili ratiba kama tu tofauti ya mechi moja na nyingine itakuwa ni siku tatu. Kwa kuwa Arsenal itacheza Jumatano hadi kufika Jumamosi zitakuwa siku tatu zimepita hivyo, hakuna sababu ya kuifanya mechi hiyo ichezwe Jumapili.
Lakini, Wenger anasema wasiwasi unaomkabili ni kwamba kutakuwa na saa 60 zitakazotofautisha mechi hizo mbili, kwa sababu kutoka Italia watarudi England Alhamisi, hawatafanya mazoezi kwa siku hiyo na watakuwa na Ijumaa pekee kabla ya Jumamosi mchana kukabiliwa na mtihani mwingine ugenini.
Habari pekee inayomfariji kocha huyo wa Arsenal ni maendeleo ya kiafya ya straika wake, Lukas Podolski, ambaye anaweza kuwa fiti kurejea uwanjani katika kipindi hicho kigumu baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kufuatia kuwa na tatizo la maumivu ya misuli.

No comments:

Post a Comment