WAKATI takwimu za ongezeko la ukuaji wa sanaa ya muziki wa kizazi kipya nchini zikipanda huku kazi za wasanii wengi zikianza kukubalika kimataifa, mwaka 2013 umekuwa wenye mafanikio makubwa kwa baadhi ya wasanii nchini. Angalau wameweza kuvuna mkwanja mkubwa kupitia muziki wao.
Hii inatukumbusha miaka 20 iliyopita wakati harakati za kuzaliwa kwa muziki huo zilipoanza kwa kuwahusisha wanamuziki kadhaa akiwamo Joseph Mbilinyi ‘Mr. II’ wakati huo, sasa ‘Sugu’.
Mwaka 2013 pia umekuwa wa neema kwani kumekuwa na ongezeko kubwa la malipo ya shoo yaliyowawezesha wasanii wengi kujikimu kimaisha na kufanya mambo ya maendeleo.
Wengi wamejenga nyumba, wamenunua mashamba pamoja na kutimiza malengo yao, achilia mbali kununua magari.
Ingawaje miaka ya nyuma wasanii walipata ujira wa kuanzia Sh1 milioni, katika baadhi ya matamasha mwaka huu, wasanii walilipwa kuanzia Sh3 milioni kwenda juu.
Wakati neema hizo zikiendelea, wasanii wengi walitoa vibao vyao kadhaa ambavyo zaidi yake vipo vilivyoweza kubamba zaidi na kukamata nafasi za juu.
Kuanzia Januari mpaka mwanzoni mwa Desemba, wapo wanamuziki 10 walioweza kufanya vizuri na kazi zao kutamba sokoni sambamba na kuangaliwa na idadi kubwa ya mashabiki ndani na nje ya Tanzania kupitia mtandao maarufu You Tube.
Nyimbo hizi ndizo zilizohusika kwa kiwango kikubwa kuwatafutia mastaa hawa shoo za maana na zenye malipo makubwa. Ndani ya vibao hivi vilivyotamba ndiko wanakozaliwa wasanii waliofanya vizuri kwa mwaka kulingana na kazi zao walizozitoa kwa kipindi cha miezi 12.
My Number One (Diamond)
Video ya wimbo huu imepata watazamaji zaidi ya 1.5 milioni tangu ulipowekwa You Tube kwa mara ya kwanza mwezi Septemba. Ni wimbo ulioweza kumtambulisha Diamond kimataifa.
Alirekodi katika studio ya kawaida sana, Burn Records, lakini wimbo huo umeweza kumkutanisha na mastaa wakubwa barani Afrika.
Kwa mara ya kwanza ameweza kufanya kolabo na Davido, Iyanya na wanamuziki wengine mashuhuri barani Afrika. Ameweza kutambulika kimataifa kutokana na video hiyo kuonyeshwa katika televisheni nyingi Afrika sambamba na mahojiano.
Dear Gambe (Young Killer)
Ni wimbo wa mwanamuziki chipukizi, Young Killer. Huyu ameweza kutamba na vibao vingine pia kikiwamo ‘Mrs Super Star’, lakini Dear Gambe ndiyo umeoongoza katika vibao vyake.
Amepata shoo nyingi, ni kijana mdogo aliyeibukia katika Super Nyota 2012. Ameweza kuliteka soko na kupata shoo nyingi zilizomwingizia kipato kikubwa.
Tupogo (Ommy Dimpoz)
Ni wimbo uliowakusanya wanamuziki kadhaa akiwamo J. Martin na vionjo vimewekwa na Mafumu Bilali. Shoo alizozipata Ommy Dimpoz mwaka huu zimechangiwa mno na wimbo huu kipenzi cha wengi.
Ni wimbo unaoelezea upendo na kudumu katika mapenzi, umekuwa kipaumbele hata kwenye harusi nyingi.
Cheza Bila Kukunja Goti
(Mwana FA & AY)
Hapa tunamkuta tena Mafumu Bilali akiwa na tarumbeta lake. Yeye ndiye aliyeweza kuunogesha zaidi wimbo huu kwa kuongeza vionjo kadha wa kadha.
Ni kati ya nyimbo chache zilizofanikiwa kutumiwa katika huduma muhimu za kwenye mitandao ya kijamii.
Ukimpigia mtu simu na usipompata hewani, unasindikizwa na wimbo huu huku ukipewa ujumbe kwamba mtu uliyempigia hapatikani.
(Ney Wa Mitego, Diamond)
Ni wimbo wenye vionjo vya aina yake. Mistari iliyoimbwa ndani ya wimbo huo iliwafanya wengi wahoji uhalali wa Ney Wa Mitego kuwasema wabana pua, hali kadhalika Diamond kuwasema Hip Hop kwamba wanatoboa pua.
Ni kolabo iliyoweza kuwaletea umaarufu mkubwa wasanii hao hasa pale walipoimba pamoja katika Ukumbi wa Dar Live na kuteka idadi kubwa ya mashabiki. Unapendwa na wengi.
Yahaya (Lady Jaydee)
Kwa kipindi kirefu kiasi, Judith Wambura, alikuwa kimya kidogo na hata alipotoa wimbo hakutingisha sana. Lakini alipotoa ‘Yahaya’ alitingisha.
Ni wimbo uliojizolea umaarufu na ndiyo ulioimbwa pia na mwigizaji wa filamu, Lulu, siku ya uzinduzi wa filamu ya ‘Foolish Age’. Yahaya pia ulimjazia Lady Jaydee mashabiki katika shoo yake ya miaka 13 ya Lady Jay Dee katika muziki.
Majanga (Snura)
Ni wimbo uliomtambulisha Snura katika ramani ya muziki akitokea katika uigizaji. Japokuwa Majanga aliiuachia mwaka 2012, lakini ulishika chati zaidi mwaka huu.
Kwa wimbo huo mmoja tu, ameweza kupata shoo zaidi ya 60 ambazo zimemwingizia kipato kikubwa ukilinganisha na alipojihusisha na uigizaji.
Majanga ni wimbo uliokuja wakati mwafaka kwani maudhui yake yalifanana na matukio yaliyokuwa yakitokea miongoni mwa jamii na hivyo kuwafanya watu kutunga msemo wa majanga wakisemea kitu kibaya au chenye kustaajabisha.
Roho Yangu (Rich Mavoko)
Ingawa wimbo huu bado haujaonyesha takwimu halisi ya shoo alizozifanya Rich Mavoko, lakini umetoa changamoto kwa wasanii wengine nchini ambao hawakuwahi kudhani kama msanii huyu ana uwezo mkubwa kimuziki.
Ndani ya mashairi yake, ameikumbusha jamii kwamba kitanda hakizai haramu lakini akimwachia msikilizaji maswali. Ni njia mojawapo ya mafanikio, kwani mpaka msikilizaji apate jawabu, tayari ujumbe unakuwa umefika.
Salamu Zao (Ney Wa Mitego)
Ni wimbo uliozua mtafaruku mkubwa miongoni mwa mastaa, lakini ulioelezea ukweli na kuleta mabadiliko makubwa miongoni mwa maeneo ambayo ameyagusa.
Mara zote Ney wa Mitego amekuwa akizungumza mambo moja kwa moja katika ngoma zake na katika sehemu ya wimbo huo anaimba;
‘’...Hizi Salamu ziende kwa Madam Rita na Bongo Star Search. Mshindi analipwa nini mbona kama magumashi? Namuona Walter Chilambo kapigika kama zamani, Haji Ramadhani kachoka yupo kitaani...Nauliza milioni hamsini zao anazila nani, acheni ubabaishaji wekeni mambo hadharani...”
Utamu (Dully Sykes)
Amewashirikisha Ommy Dimpoz na Diamond. Umepambwa zaidi na matarumbeta ya Mafumu Bilali. Ni kati ya nyimbo zilizofanya vizuri mwaka 2013 kwa kuangaliwa pia kwenye You Tube, pia umetamba katika miito ya simu zao za mkononi.
No comments:
Post a Comment