KILA mazoezi ya Simba yanapomalizika kwenye Uwanja wa Kinesi jijini Dar es Salaam, mashabiki wa timu hiyo humzunguka kocha wao Zdravko Logarusic na kumfananisha sura na straika wa Manchester United, Wayne Rooney, lakini kocha huyo amewatolea uvivu na kuwaambia wamfananishe na Didier Drogba
.
Mashabiki wa Simba hawaishiwi vituko, kwani humfuata Logarusic muda mfupi anapomaliza mazoezi na kikosi chake na hapo huanza kumwita kwa jina la Rooney huku wakimsifia kwa mambo mbalimbali.
Walipomwona mwandishi wa habari hizi akifanya mahojiano na Logarusic, mashabiki hao walisikika wakisema; “Mwambie Rooney mavitu yake tumeyakubali.”
Baada ya kauli hiyo ya mashabiki, Logarusic aliomba tafrisi ya maneno hayo na alipoelezwa na mwandishi wa habari hizi, alicheka: “hahaha, labda kama nimefanana naye, lakini waambie waniite Drogba maana wakati nacheza nilikuwa hatari sana.”
Logarusic amewahi kucheza soka mwaka 1975 hadi 1988 katika klabu ya daraja la kwanza ya Croatia ya Marsonia kabla ya kutimkia Sweden mwaka 1988 katika klabu ya Malmo iliyokuwa daraja la pili. Aliitumikia klabu hiyo kwa mwaka mmoja tu.
Mwaka 1990 hadi 1991, Logarusic raia wa Croatia mwenye umri wa miaka 51, aliichezea klabu ya daraja la pili ya Ujerumani ya 08 Willingen na baadaye mwaka 1992 hadi 1993 aliichezea klabu ya daraja la kwanza ya Perth ya Australia ambayo William Gallas anaichezea sasa.
No comments:
Post a Comment