Tuesday, 10 December 2013

MWALALA AWAHOFIA SAMATA NA NGASA



Samata 

STRAIKA wa zamani wa Yanga, Mkenya Ben Mwalala amesema Kenya ina nafasi kubwa ya kushinda mechi ya leo Jumanne dhidi ya Kilimanjaro Stars, lakini washambuliaji Mbwana Samata na Mrisho Ngassa wakiamka vizuri wenyeji watafungwa.
Kenya au Harambee Stars na Kilimanjaro Stars ya Tanzania zitaumana katika mchezo wa nusu fainali kuwania Kombe la Chalenji utakaochezwa kwenye Uwanja wa Machakos, Nairobi, Kenya.
Mwalala ambaye sasa ni kocha wa timu ya soka ya Halmashauri ya Tanga, aliliambia Mwanaspoti kuwa Kilimanjaro Stars ina kikosi kizuri kinachoweza kuisumbua Kenya katika mchezo huo lakini wenyeji wana uhakika wa ushindi kutokana na sapoti kubwa watakayopata kutoka kwa mashabiki.
“Kenya itafanya vizuri katika mechi ya kesho (leo Jumanne) ina kikosi kinachojengwa upya ili kifanye vizuri hapo baadaye, pia itabebwa na mashabiki wengi watakaojitokeza uwanjani na ndiyo maana wakahamisha mechi kutoka Mombasa hadi Machakos.
“Lakini Tanzania si timu mbovu, Samata na Ngassa wakiamka vizuri wanaweza kuichakaza Kenya hata kama ipo nyumbani, hawa ni wachezaji wazuri sana,” alisema Mwalala aliyeichezea Yanga kuanzia mwaka 2006 hadi 2009.
Mwalala alisema Kilimanjaro Stars ingeweza kufanya vizuri kama mchezo huo ungechezwa Mombasa, Watanzania wengi wangeweza kuhudhuria wakitokea mkoani Tanga.
Samata hana matatizo yoyote ya kiafya lakini Ngassa aliripotiwa kuwa na maumivu ya kifundo cha mguu aliyoyapata katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Uganda Jumamosi iliyopita hivyo huenda akaukosa mchezo huo.

No comments:

Post a Comment