STRAIKA wa Azam FC, Gaudence Mwaikimba ameibuka na kusema wote wanaodhani amefulia, wanakosea kwani amepania kufanya mambo makubwa katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara mwakani.
Mwaikimba, ambaye ni straika mrefu aliyejengeka kwa mwili wa mazoezi,hakuwa akipata nafasi katika mechi nyingi za ligi na zile za kimataifa msimu huu na kuwaacha John Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Tchetche wakimiliki namba za ushambuliaji.
Mwaikimba aliiambia Mwanaspoti kuwa alicheza mechi chache za mzunguko wa kwanza lakini hataki kukaa benchi katika mzunguko wa pili utakaoanza Januari 25 mwakani.
“Sikupata nafasi kubwa ya kucheza mzunguko wa kwanza japokuwa nimecheza mechi tano na kufunga bao moja tu, unajua tupo wengi hapa (Azam), lakini nina imani mzunguko wa pili nitacheza tu,” alisema Mwaikimba, ambaye amewahi kuzichezea Ashanti, Yanga na Prisons ya Mbeya.
Alisema japokuwa kocha wao mpya James Omog hajaifundisha timu kwa muda mwingi tangu alipopewa jukumu la kuifundisha hivi karibuni, ana imani ataonyesha kiwango kizuri katika mazoezi na kumvutia ili ampe nafasi kikosi cha kwanza.
Katika mechi tano alizocheza, Mwaikimba alifunga bao moja tu dhidi ya Rhino Rangers Agosti 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora katika mchezo ambao Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-0. Bao jingine la Azam lilifungwa na Seif Karie.
No comments:
Post a Comment