Kipa Abel Dhaira |
KIPA Abel Dhaira, ametamka kuwa anajua jambo kubwa lililofanya yeye kutemwa na Simba si kutokana na kushuka kiwango.
Akizungumza na Mwanaspoti, kipa huyo kutoka Uganda alisema kuwa ametemwa Simba kwa madai kuwa alikuwa akiuza mechi mara kwa mara na kufungwa kwake mabao matatu katika mechi dhidi ya Yanga kulizidisha makali ya tuhuma hizo.
Dhaira ambaye kwa sasa yuko Kampala, Uganda alisema: “ Kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuna kiongozi ambaye alinituhumu kuwa mimi nauza mechi.
“Tena iliniuma sana kwani sikuona haja ya kuihujumu timu yangu, nililenga kuisaidia Simba, hakuna kipa asiyefungwa, mimi naweza kufanya makosa ya kibinadamu na lawama zikawa za kuuza mechi, kwa kweli hata kama ningebaki tuhuma hizo zingeninyima amani.
“Lakini naijua kazi yangu ndugu yangu, kwa mambo wanayofanya Simba soka halitaenda kokote, itakuwa ni lawama kila kukicha,’’ alisema
“Nakumbuka Kocha Kibadeni aliniambia nia ya kumtumia kipa wa vijana Abou Hashimu kwenye mechi mbili za mzunguko wa kwanza ili kumsaidia kipa huyo kupata uzoefu wa kucheza ligi na mimi nililipokea hilo kwa moyo mmoja ili kumsaidia kijana huyo,” alisema Dhaira.
Dhaira anakamilisha mipango ya kwenda nchini Iceland Januari mwakani ambako huenda akajiunga kwa mara nyingine na klabu yake ya zamani ya Vestmannaeyja ‘ÍBV’.
No comments:
Post a Comment