Tuesday, 12 November 2013

Usajili, timuatimua makocha vinahitaji umakini



HUU ni wakati wa mapumziko ya Ligi Kuu Bara baada ya duru la kwanza kufikia ukomo Alhamisi iliyopita. Ni wakati mwafaka kwa klabu shiriki kutafakari kwa kina nini kinatakiwa kufanyika ili mechi za duru la pili mambo yaende vizuri.
Kwa maana nyingine huu ni wakati ambao mkurugenzi wa ufundi au benchi la ufundi linapaswa kuwa makini kwa kuyachambua matatizo yote na kuyafanyia kazi.
Ni wakati ambao klabu inatakiwa ifahamu wapi kwenye tatizo na nani anahusika na nini kinaweza kufanywa kuhakikisha tatizo hilo linatatuliwa.
Si wakati wa kutimua kocha kwa sababu timu yake imefanya vibaya, na si wakati wa kutimua mchezaji au kumtoa kwa mkopo kwa sababu tu alifanya kosa fulani katika mechi moja.
Vilevile huu si wakati wa kusajili tu kwa sababu tu kuna mchezaji mzuri ameonekana akicheza na timu fulani.
Badala yake ni wakati wa kufanya yote hayo tuliyoyataja hapo juu kwa umakini wa hali ya juu baada ya benchi la ufundi kufanya mapitio na kuona umuhimu wa kufanya linalofaa kwa maslahi ya timu.
Tunalisema hili kutokana na ukweli kwamba wakati huu wa mapumziko, klabu za ligi kuu mara nyingi zinakuwa na hulka ya kutimua makocha na hata kusajili bila kuzingatia kama kinachofanywa ni cha lazima au la.
Tunapenda kuona kipindi hiki kikitumika vizuri hasa kwa mambo hayo mawili yaani makocha na wachezaji, kama ni kumtimua kocha kuwe na sababu inayojitosheleza kufanya hivyo.
Kama ni kusajili au kutimua mchezaji ni vyema jambo hilo pia likafanywa kwa kuzingatia hali halisi ya timu na upungufu au mchezaji mzigo aliyepo.
Imezoeleka katika soka la Tanzania suala la usajili kufanywa kwa baadhi ya wanachama wakati mwingine bila hata kulihusisha benchi la ufundi.
Ni hivyo hivyo hata kutimua na kuajiri makocha, kumekuwa kukifanywa kienyeji na wakati mwingine majungu huwa sababu tosha ya kumtimua kocha na kumpa ajira mwingine.
Ni vyema klabu zetu zikabadilika na kuacha tabia ya kufanya mambo kienyeji. Kwa kusema hivyo si kwamba tunapinga au hatutaki kuona makocha wakitimuliwa bali tunapenda jambo hilo lifanyike baada ya kuonekana ni lazima kufanya hivyo.
Tumekuwa tukisikia makocha wengi wakifukuzwa hususan katika ligi za Ulaya hivyo si ajabu kwa makocha wa Ligi Kuu Bara nao kutimuliwa kutokana na udhaifu ambao utajitokeza katika timu zao.
Tusichokipenda ni ile hali ya makocha kutimuliwa ovyo, kwa wakati huu hatutashangaa kuona kocha anatimuliwa kabla hata hajawasilisha ripoti yake ya duru la kwanza . Tunaamini ripoti hiyo inaweza kuwa dira kwa uongozi kujua matatizo yaliyojitokeza, kwa nini timu imefanya vibaya na nini kinachotakiwa kufanyika.
Haya ni mambo ambayo ni nadra sana kufanyika badala yake timu inapofungwa anatokea mtu asiyempenda kocha, anamlaumu na kushauri atimuliwe na uongozi unaafiki. Madhara ya jambo hili ni kwamba hata huyo kocha mpya anayekuja anakosa pa kuanzia kwa kuwa ripoti ya mtangulizi wake ambayo ingekuwa dira kwake haipo.
Ni vyema tukabadilika ili timua ya makocha na usajili wa wachezaji uwe na maana kwa timu husika

No comments:

Post a Comment