Kikosi cha Mbeya City |
TULIWAHI kuzishauri timu za majeshi nchini zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kufikiria kuungana ili kuwa na timu moja yenye nguvu.
Tukafafanua kwamba suala la majeshi nchini kuwa na timu nyingi linakera pale ambapo timu hizo zinakuwa ni zenye kupokezana kupanda na kushuka daraja
.
Ni kutokana na hali hiyo tukashauri viongozi wa majeshi kukaa na kuja na mpango mkakati ambao utawafanya wawe na timu moja yenye nguvu. Mathalani mpango mkakati unaweza kuziunganisha timu za JKT Ruvu na Oljoro JKT na nyinginezo kuwa timu moja ambayo itakuwa na nguvu.
Tunaamini timu ya aina hii itakuwa na nguvu kiuchumi na hivyo kuwa na uwezo wa kushindana katika ligi na hata kumudu mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara kwa muda mrefu badala ya kupanda na kushuka.
Wiki kadhaa baada ya kulielezea hili, Rais wa TFF aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga kati ya mambo aliyoyazungumza katika siku zake za mwisho ni suala hili la timu za majeshi kuwa na timu moja.
Hoja ya Tenga ilisimamia katika maelekezo kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambao wanatambua athari zinazoweza kujitokeza na kuathiri ushindani wa kweli iwapo timu za majeshi zitaendelea kuwa kama zilivyo. Nasi tunaiunga mkono hoja ya Fifa tukiamini kwamba timu hizo za jeshi tutake tusitake mara nyingi zinaangukia katika bosi mmoja, iwe ni Jeshi la Magereza, Polisi au Jeshi la Kujenga Taifa.
Bosi huyo ni mkuu wa jeshi husika nchini ambaye atakuwa na nguvu kwa timu ya jeshi husika mkoani Arusha, Pwani, Dodoma na kwingineko.
Mazingira ya aina hii ndiyo yanayotia hofu ya timu hizi kubebana inapolazimika kufanya hivyo ili kuisaidia mojawapo ya timu hizo ukizingatia ukweli kuhusu amri za kijeshi zinavyokwenda kuanzia juu hadi chini. Hatukatai kwamba timu hizo zimewabeba vijana
wengi, tunadhani juhudi hizo za kuwabeba vijana wa Tanzania zinaweza kuendelea kwa maana ya kwamba mpango huu hauzifuti timu za jeshi.
Timu za jeshi mikoani zitaendelea kuwapo lakini timu inayoshiriki ligi ibaki moja ambayo itachukua wachezaji walio bora kutoka katika timu nyingine za jeshi.
Mazingira ya aina hii yatawafanya wachezaji kupambana ili kupata nafasi ya kuwamo katika timu moja kubwa ya jeshi ambayo tunaamini itakuwa imara na yenye kutoa ushindani katika Ligi Kuu Bara.
Zaidi ya hilo, mpango huu kama tulivyosema awali utaziwezesha timu hizo kuwa na nguvu ya kiuchumi jambo ambalo lina umuhimu wa kipekee katika maendeleo ya mpira wa miguu. Kwa wakati wote ni rahisi kuihudumia timu moja ya jeshi katika Ligi Kuu badala ya mbili au tatu.
Kwa mantiki hiyo tunadhani huu ni wakati mwafaka kwa viongozi wa timu za jeshi kukaa chini na kuangalia namna nzuri ya kulifanyia kazi agizo hili la Fifa
Ni agizo ambalo linaweza kuwashangaza baadhi yetu na kuona ni gumu kulifanyia kazi lakini kwa upande wetu kama tulivyolizungumza hapo awali tunasisitiza tena kwamba lina maana kubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania
No comments:
Post a Comment