Friday, 8 November 2013

Neymar abadili namba yake ya simu kila siku

Nimeshindwa kutunza namba yangu ya simu kwa walau wiki mbili kwa sababu watu wanaojiita mashabiki-Neymarzetes – huwa wananipigia simu mida ya asubuhi au kunitumia meseji. Mbaya zaidi wanagundua pia namba za simu za watu wa familia yangu, rafiki yangu wa kike,  wanatunga stori nyingi na uongo na mwishowe naishia kubadilisha namba yangu ya simu.” Neymar

BARCELONA, HISPANIA
UGONJWA wa mashabiki kumpenda sana staa mpya wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Neymar, umekithiri na sasa kinda huyo mwenye sura ya mvuto amewaomba mashabiki wake wasiingilie sana maisha yake binafsi.
Ingawa ana tabia za kitoto, kiasi cha kutuma picha zake kila mara katika mtandao wa Instagram, Neymar amenyoosha mikono kwa mashabiki wake na kuwaomba wamuweke mbali. Hiyo ni kutokana na kumsumbua mara kwa mara nje ya uwanja wa soka.
Mashabiki hao wanasadikiwa kuwa wa nchini kwake Brazil ambako amekuwa akihusudiwa kuliko mchezaji mwingine yeyote nchini humo huku wengi wakiweka matumaini ya kutwaa Kombe la Dunia nchini mwao mwakani kupitia yeye.
Katika barua ya wazi aliyowaandikia mashabiki wake wenye wazimu wa kumpenda unaojulikana kwa jina la Neymarzetes, Neymar ameeleza jinsi anavyolazimika kubadilisha namba yake ya simu kila siku.
“Ninawapenda sana na sijui kama ningefika hapa nilipofika bila ya wao,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ambayo aliituma katika mtandao wa Instagram.
“Nimeshindwa kutunza namba yangu ya simu kwa walau wiki mbili kwa sababu watu wanaojiita mashabiki-Neymarzetes – huwa wananipigia simu mida ya asubuhi au kunitumia meseji. Mbaya zaidi wanagundua pia namba za simu za watu wa familia yangu, rafiki yangu wa kike,  wanatunga stori nyingi na uongo na mwishowe naishia kubadilisha namba yangu ya simu.”
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 21 kutoka katika Jiji la Sao Paolo,  hajapata matatizo katika kuizoea Ligi Kuu Hispania lakini nje ya uwanja amekuwa na wakati mgumu wa kupata usingizi kutokana na kusumbuliwa na mashabiki wa nyumbani kwao Brazil.
“Ninawaomba kwa moyo wangu wote kwamba kila anayenipenda mimi na ambaye amekuwa na mimi tangu mwanzo, kama kuna mtu anamjua anafanya hivi tafadhali amshauri aache tabia hiyo. Sijui kitu kingine cha kufanya,” aliongeza.
Neymar amejitahidi kuishi maisha ya kawaida tangu alipotua Barcelona akitokea Santos katika kipindi cha majira ya joto kilichopita. Ameondoa staili yake ya nywele maarufu kwa jina la Mohican na ameendelea kujaribu kuishi chini ya kivuli cha Messi.
Hata hivyo, mpaka sasa ameshindwa kabisa kuwadhibiti watu wanaoipata namba yake ya simu kwa njia za panya.
“Sijui nifanye kitu gani kingine. Hawa watu wananisababishia matatizo sana. tafadhali niacheni niishi kwa amani,” analalamika.
Kwa sasa Neymar amekuwa katika penzi zito na mrembo, Bruna Marquezine, mwenye umri wa miaka 17. Mrembo huyo ambaye jina lake kamili ni Bruna Maia Reis in Duque De Caxias, amekuwa staa wa tamthiliya za televisheni nchini Brazil huku akifanya kazi za uanamitindo.
Tangu mwaka 2003, Bruna ameshinda tuzo 11 akiwa ameanza kuigiza tangu akiwa na umri wa miaka minane. Alianza maisha ya kazi hiyo akiwa kando ya mtangazaji maarufu wa Brazil, Xuxa.
Kwa kuwa na uhusiano na Neymar, Bruna, ambaye alikuwapo uwanjani wakati Neymar akitambulishwa kuwa mchezaji wa Barcelona, anakuwa na bahati ya kuwa katika penzi na mmoja kati ya wanasoka wenye mvuto ndani na nje ya uwanja.
Neymar alisaini mikataba mingi akiwa na umri wa miaka 17 tu wakati jina lake linachomoza kwa kasi Santos. Machi 2011, alisaini mkataba wake wa kwanza na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike akiwa na umri wa miaka 11 tu.
Katika mwezi huo huo alisaini mkataba wa miaka miwili na kampuni ya Panasonic ambao ulikuwa na thamani ya Dola 2.4 milioni. Neymar pia alisaini mikataba na kampuni za Volkswagen, Tenys Pé Baruel, Lupo, Ambev, Claro, Unilever na Santander.
Kwa mikataba yake yote hiyo, Neymar anakusanya kiasi cha Euro 20 milioni kwa mwaka. Mei 2013, alitajwa kuwa mwanamichezo mwenye soko zaidi duniani mbele ya Lionel Messi aliyeshika nafasi ya pili na Cristiano Ronaldo aliyeshika nafasi ya nane

No comments:

Post a Comment