Tuesday, 12 November 2013

Mtibwa yagoma kusajili

WAKATI pazia la usajili wa dirisha dogo kwa klabu za Ligi Kuu Bara likifunguliwa rasmi Novemba 15 hadi Desemba 15 mwaka huu, Kocha wa Mtibwa, Mecky Maxime amesisitiza kwamba hatasajili mchezaji yeyote.
Kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya TFF, dirisha dogo la usajili ni kwa ajili ya kutoa nafasi kwa klabu kufanya usajili na kuimarisha vikosi kwa ngwe inayofuata mwakani.
“Timu yangu ni nzuri na sidhani kama kuna sababu yoyote ya msingi kuongeza mchezaji mpya kwa ajili ya mzunguko wa pili ingawa kweli kuna marekebisho ya kufanya, lakini si kwa kusajili mchezaji mpya,” alisema.
“Siwezi kufanya usajili wa fasheni kama Simba na Yanga kila wakati wanasajili na mwisho wake wanajikuta wakishindwa hata kuwatumia hao wachezaji na kuwaharibia maisha yao ya soka.”
Akizungumzia safu yake ya ulinzi kushindwa kuelewana katika mechi ya Simba na Yanga na kulala kwa mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam alisema: “Ni kweli kama ulivyoona ingawa tatizo hilo kwa sasa halipo tena, nafasi ya tano ambayo tumeishia si mbaya sana.”
Mtibwa Sugar ambao wamewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili, mwaka 1999 na 2000 wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wakiwa na pointi 20 sawa na Ruvu Shooting ya Pwani ingawa timu hizo zinatofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Wakati Mtibwa ikionyesha kukiamini kikosi chake, tayari Yanga wameanza kufanya usajili wao kwa fujo baada ya kumnyakua mlinda mlango aliyeachwa na Simba, Juma Kaseja ambaye katika mzunguko wa pili ataonekana akilinda lango la timu hiyo inayoongoza ligi hadi mzunguko wa kwanza unamalizika

No comments:

Post a Comment