ZURICH, USWISI
WAHISPANIOLA wana usemi wao ‘Cria fama y echate a dormir’ ambao maana yake ni kwamba unapokuwa maarufu huna haja ya kujisumbua kuulinda umaarufu wako
.
Waswahili nao wanadai ‘Uzuri wa mwanamke si sura, ni tabia’, yaani anaweza kuwa na mwonekano wa kuvutia, lakini undani wake ukawa ni hatari kubwa.
Kwenye soka ‘mke’ mzuri ni yule mchezaji anayefunga mabao katika mechi muhimu na kuipa mataji timu yake kama anavyofanya Cristiano Ronaldo wa Real Madrid bila kujali kwamba ataingia uwanjani akiwa amechana nywele zake au amenyoa kipara kama alivyokuwa akifanya Zinedine Zidane.
Mara kadhaa, Ronaldo amekuwa akiibeba klabu yake kwa mgongo wake na kuchuana na Barcelona ya Lionel Messi na mastaa wengine kibao kama Cesc Fabregas, Andres Iniesta na Xavi.
Hivyo kwa sifa za ndani ya uwanja, Ronaldo anastahili sifa zake ukiachana na mambo yake binafsi.
Straika wa Ivory Coast, Didier Drogba, alikuwa akiweka ‘karikiti’ nywele zake kila anapoingia uwanjani, lakini hilo halikumfanya aonekaze bishoo kwa sababu mabeki wa Kizungu wanajuta kumfahamu wanapokumbana naye.
Hii ni sawa na Waingereza wanaposema ‘Don’t judge a book by looking its cover’ kwa sababu ukweli ganda la nje la kitabu haliwezi kusadifu kilichoandikwa ndani.
Misemo hiyo yote inasadifu kisa cha hivi karibuni cha Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter dhidi ya wanasoka wawili mastaa; Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Blatter alitoa kauli yenye utata ambayo imetibua hali ya hewa Santiago Bernabeu kwa kuponda mwonekano wa Ronaldo na kusahau uwezo wake wa kisoka.
Alichodai Blatter ni kwamba Ronaldo anapoteza saa nyingi kusimama kwenye kioo na kujiremba, wakati Messi ni mchezaji mpole, hakuwaelezea katika soka wanalocheza kwamba ni mchezaji gani aliyetimia kila idara.
Kauli hiyo imemchafua na kumweka kwenye wakati mgumu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye tuzo za Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia (Ballon d’Or)
Ronaldo na Messi watachuana kuwania tuzo hiyo sambamba na wakali wengine ambao orodha yao ya awali ilitolewa wiki iliyopita kabla ya baadaye kufanyika mchujo na kupata wachezaji watatu watakaoingia fainali.
Soka si kigezo tena
Blatter ameichafua Fifa na kuthibitisha kwamba ujuzi wa soka la uwanjani na umahiri mkubwa wa kiuchezaji hauna maana tena katika kutafsiri ubora wa mchezaji.
Wakati mashabiki wa soka duniani kote wakiamini kwamba huenda safari hii kukawa na mabadilisho kwenye tuzo za Ballon d’Or kwa kuona sura nyingi kama Ronaldo, Franck Ribery, Robin van Persie na Arjen Robben zikitamba badala ya Messi, kauli ya Blatter imeibua hofu kubwa.
Bosi huyo amejikuta kwenye kashfa baada ya kutoa sifa kwa Messi kwamba ni mchezaji mtaratibu anayehusudiwa na kila mtu na kama angekuwa mtoto basi kila mzazi angehitaji awe mwanawe, huku akimponda Ronaldo kwamba ni mchezaji ambaye hana mvuto wa kiuchezaji na amekuwa kama ‘Kamanda’ awapo uwanjani.
Kauli hiyo imewakera Wahispaniola hasa Los Blancos kwa sababu Blatter amehukumu kwa mtazamo wa nje. Hakujali uwezo wa soka la Ronaldo ndani ya uwanja hata kama ana mambo yake mengine binafsi. Je, Blatter anamfahamu vizuri Messi?
Messi na upole wa kinafiki
Blatter amenaswa na upole wa kinafiki wa Messi anapokuwa uwanjani, lakini kama angepata nafasi ya kuwamo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya Barcelona japo kwa saa 24 tu angemfahamu vizuri mchezaji huyo.
Kitendo cha kuwahi kumgomea aliyekuwa kocha wake, Pep Guardiola, kinatosha kueleza kwamba Messi si mtoto mwema kama anayeelezewa na Blatter.
Kama hilo halitoshi, wachezaji kama Zlatan Ibrahimovic na hata David Villa na Samuel Eto’o wanafahamu hila za mchezaji huyo na kwamba hawawezi kuketi na kusapoti kauli ya Blatter kwasababu wanaujua ukweli kuhusu Messi.
Kinachomlinda Messi ni kuficha makucha yake anapokuwa uwanjani, wakati Ronaldo hajali kitu na amekuwa akifanya yanayomhusu mwenyewe bila ya kuingilia uhuru wa mtu.
Wengi wanafahamu uhodari wa Ronaldo na utu wake na hakika ni taswira ya baadhi ya vijana wanahitaji kuwa kama yeye si kwa ubora wa ndani ya uwanja pekee bali pia wa nje.
Kwa sababu ni ngumu kumtambua mtu mambo yake mengi binafsi, Blatter kama bosi wa chombo kikubwa cha kusimamia soka hakupaswa kutoa kauli yenye utata kama aliyoitoa kwa sababu hamfahamu Messi vizuri kwa tabia zake Nou Camp.
Ronaldo amjibu Blatter uwanjani
Kabla ya kudai kwamba ana wasiwasi na upendeleo atakaoupata Messi kwenye tuzo za Ballon d’Or, Ronaldo alipanga kufanya kitu dhidi ya Blatter.
Baada ya kudaiwa kwamba yeye ni kama ‘kamanda’ anapokuwa uwanjani, supastaa huyo wa Kireno alishangilia kwa staili ya kupiga saluti na kuonyesha ukakamavu wakati alipofunga dhidi ya Sevilla kwenye mechi ya La Liga.
Wakati Ronaldo akifanya tukio hilo ndani ya uwanja, Blatter alikuwa jukwaani akitazama mechi hiyo ambayo staa huyo wa zamani wa Manchester United alifunga ‘Hat-Trick’
No comments:
Post a Comment