Mshambuliaji wa Liverpool, Luiz Suarez (kushoto) akibishana na mlinzi wa Arsenal, Bacary Sagna katika pambano baina ya timu zao juzi. |
LONDON, ENGLAND
KATIKA msimu wa soka wa mwaka 2008/09, Liverpool ilifurahia mwisho mzuri kwenye Ligi Kuu England. Kipindi hicho mashabiki wake walikuwa wakiimba nyimbo zote tamu za kujisifu kwamba wanamiliki kiungo bora kabisa duniani.
Hakika, kipindi hicho klabu hiyo ilikuwa na watu watatu makini katika idara ya kiungo, walikuwapo Javier Mascherano, Xabi Alonso na Steven Gerrard. Si tu watu watatu makini, bali timu nzima ilikuwa kwenye kiwango cha ubora.
Nyimbo hizo sasa zinaimbwa na Arsenal kwa namna fulani. Kichapo walichokitoa juzi Jumamosi dhidi ya Liverpool kimeibua mijadala mingi na hasa kubwa la kiuchezaji kwenye safu ya kiungo.
Wakati kikosi cha Arsene Wenger kikionekana kubarikiwa na vipaji vya haja kwenye safu hiyo, mashabiki wa Liverpool wao wanasikitikia udhaifu unaowakabili kwa msimu huu mpya kuhusu wachezaji viungo.
Si kwamba Liverpool haina viungo wa kati wa kutosha, wapo na kuna uwiano mzuri kitu kinachowatatiza ni kiwango. Katika mechi hiyo dhidi ya Arsenal, walishindwa kumiliki mpira tofauti na matarajio ya wengi na hata ya kocha wao, Brendan Rodgers.
Wiki iliyopita, Liverpool iliikamata West Brom na kuinyuka mabao 4-1 ambapo kwenye safu yake ya kiungo kulikuwa na watu watatu; Lucas Leiva, Steven Gerrard na Jordan Henderson ambao waling’ara na kutawala.
Lakini, watatu hao walipopewa mtihani wa kukutana na timu yenye viungo wengi mafundi kwenye ligi hadithi ikawa tofauti na tatizo lilijiweka bayana.
Wanaoaminiwa Lucas na Gerrard
Mbrazili Lucas Leiva hayupo vizuri na si kiungo mlazimishaji, ni tofauti na alivyokuwa miaka miwili iliyopita. Kuwa majeruhi kwa muda mrefu kumeshusha kiwango chake na amekuwa akifanya makosa yanayofanana kila mechi, amekuwa akisababisha faulo na kupoteza mipira kirahisi.
Hana uwezo wa kumiliki mpira na si mtu anayebadilika. Gerrard ana umri wa miaka 33, amepungua nguvu na si msumbufu tena uwanjani. Alipopangwa na Lucas alishindwa kufurukuta mbele ya viungo wa Arsenal wanaochakarika.
Gerrard amecheza mechi nyingi, amekuwa akianzishwa kila mechi za Liverpool kwenye ligi na anapokuwa timu ya taifa ya England
Alionekana kuchoka tangu aliporejea kwenye mechi za kimataifa na pale Emirates juzi Jumamosi ilionekana wazi. Liverpool imemsajili Joe Allen mchezaji mwenye uwezo wa kumiliki sehemu ya kiungo, tatizo la Rodgers anataka awapange pamoja na Gerrard.
Henderson alilazimika kufanya kazi ya viungo wengine wawili mara kadhaa uwanjani kwa sababu Gerrard na Lucas walishindwa kuipeleka timu mbele kushambulia. Henderson hakuwa tatizo, Gerrard na Lucas bure kabisa.
Mabadiliko wakati wa mapumziko
Mabadiliko aliyoyafanya Rodgers wakati wa mapumziko yalikuwa yenye kueleweka. Aly Cissokho alikuwa mchezaji ambaye aliwafanya mashabiki kumkumbuka Jose Enrique.
Lakini lililofanyika ni kumchezesha mchezaji huyo abaki kwenye mstari wa nyuma. Kuingia kwa Philippe Coutinho kucheza kushoto, kuliwafanya wadhaifu Lucas na Gerrard kubaki wenyewe katikati na hivyo walipitwa kirahisi na viungo makini wa Arsenal.
Muundo wa safu yao ya kiungo uliipa nafasi Arsenal kushambulia kupitia mabeki wao wa pembeni, hilo liliwapa wakati mgumu mabeki wa kati wa Liverpool.
Mastraika wawili mbele
Kwa mfumo wa soka la kisasa, ni adimu kuona mastraika wawili wa kati wakipangwa pamoja hasa ukihitaji kumiliki sehemu ya kiungo. Mahali hapa ndipo walipokosea Liverpool.
Kocha Pep Guardiola anaamini hivi: “Ni mara chache sana kushinda mechi kwa sababu ya mastraika na mabeki wazuri, akikisisitiza kwamba haiwezekani kama hutokuwa na wachezaji mahodari kwenye kiungo.”
Liverpool imekuwa ikishinda mechi kwa sababu ina mastraika mahiri, lakini inapokutana na timu yenye ubora mkubwa, viungo wake hawana uwezo wa kupambana.
Kitu cha kufanyika
Kwa Liverpool kukwepa kilichowakuta kwa Arsenal ili kisijirudie ushauri kwa timu nyingine itakayokutana na Arsenal, kuna mambo mawili yanapaswa kufanyika.
Kwanza ni uchaguzi sahihi wa wachezaji wa kiungo na mbili ni muundo au uchaguzi wa fomesheni. Mfumo wa 4-2-3-1 kwa kuwa na viungo wajanja na wengine wawili wanaotumia nguvu hilo litatoa nafasi ya kuitawala Arsenal kwenye sehemu hiyo ya katikati ya uwanja.
Rodgers alipokuwa Swansea alitengeneza kikosi kilichokuwa na kiungo inayotaka kuwa na mpira muda wote na wachezaji wake wa pembeni walikuwa na kazi, hivyo kama angeanza na Luis Suarez na Victor Moses kwenye wingi kati ya wachezaji watatu wa mbele hilo lingempa nguvu ya kuishinda kiungo ya Arsenal.
Coutinho angecheza namba 10 na nyuma yake kungekuwa na Allen na Henderson ambao wangetengeneza pembetatu ya wachezaji wajuzi na wenye uwezo wa kumiliki mpira huku wakibadilika kutokana na kasi ya mchezo.
Kwa hali iliyoonyeshwa na Lucas na Gerrard, Rodgers anahitaji kufanya usajili wakati dirisha la uhamisho litakapofunguliwa mwakani
No comments:
Post a Comment