Kocha wa Serbia, Kopunovic Goran aliyeomba kazi ya kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Simba. |
KOCHA wa Serbia, Kopunovic Goran ameomba kazi ya kuwa Kocha Mkuu wa Simba.
Kocha huyo ametuma maelezo yake binafsi (CV) kwa klabu ya Simba na Mwanaspoti imepata nakala yake.
Goran, ambaye alikuwa Kocha wa Police FC ya Rwanda kwa miaka mitatu alifanya maajabu na kuiwezesha timu hiyo ambayo ilikuwa ya kawaida kuwa tishio Ligi Kuu Rwanda.
Msimu wake wa kwanza 2010/11 akiwa na Police FC aliongeza upinzani baina yake na Kocha wa APR, Ernest Brandts, ambaye sasa yupo Yanga.
Makocha hao wanajuana vizuri kutokana na kuwahi kufanya kazi kwa wakati mmoja nchini Rwanda. Goran, alikuwa Kocha wa Police FC ya Rwanda kuanzia mwaka 2010 mpaka msimu uliopita alipotimuliwa baada ya kuifanya timu hiyo kushika nafasi ya pili.
Msimu wa 2010/11 aliiwezesha Police kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Rwanda jambo ambalo lilikuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo tangu ianzishiwe. Kwa mara ya kwanza pia msimu huo, Polisi ilitinga fainali ya Kombe la Amani la MTN.
Msimu wa 2011/12, Kocha huyo aliyezaliwa mwaka 1967 aliiwezesha Police kumaliza nafasi ya pili ambayo ilikuwa ni rekodi na mara ya kwanza timu hiyo kufikia hatua hiyo na safari hii pia ilitinga katika fainali ya MTN.
Msimu uliopita, kocha huyo aliiwezesha Police kushika nafasi ya pili kwa mara nyingine huku mabingwa wakiwa Rayon Sports na vigogo APR wakishika nafasi ya tatu.
Kwa mara ya kwanza katika historia, Kocha huyo aliiwezesha Police kucheza Kombe la Shirikisho (CAF).
Goran alimaliza miaka mitatu kwa kutimuliwa na Police FC Juni mwaka huu ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kumaliza mkataba wake Julai 21.
Goran amewahi kucheza timu mbalimbali za Ulaya ikiwa ni pamoja na kwao Serbia na Hungary lakini la muhimu zaidi amecheza mechi 11 za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kuleta maombi kwa kocha huyo kunaongeza upinzani Simba kwani klabu hiyo ya Msimbazi inamtaka kwa udi na uvumba kocha Bobby Williamson wa Gor Mahia ya Kenya ili achukue mikoba ya Abdalla Kibadeni. Williamson (52), ni straika wa zamani wa West Bromwich Albion na katika mechi 53 aliyoichezea timu hiyo alifunga mabao 11.
Williamson, ambaye ni raia wa Scotland alijiunga na Gor Mahia msimu huu na tayari ameipa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya ikiwa ni miaka 18 tangu timu hiyo itwae ubingwa wa Kenya mwaka 1995.
Williamson, ambaye alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Uganda na kuipa ubingwa wa Kombe la Chalenji mara nne, ni kocha anayesifika kutokana na kufundisha soka la kisasa kwa timu kushambulia na kukaba kwa pamoja.
Viongozi wa Simba wamesema wanasubiri kupata ripoti ya benchi la ufundi kabla ya kufanya uamuzi wowote lakini ni wazi kwamba benchi la ufundi msimu ujao litakuwa na kocha wa kigeni ambaye kuna uwezekano mkubwa akasaidiwa na Mosses Basena wa Uganda. Basena kwa sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Simba
No comments:
Post a Comment