Wednesday, 16 October 2013

TFF YATHIBITISHA NKONGO KUCHEZESHA SIMBA NA YANGA


Mwamuzi ataechezesha mechi ya Simba na Yanga,Israel Nkongo
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limethibitisha kwamba, Israel Nkongo wa Dar es Salaam atachezesha mechi baina ya Simba na Yanga itakayofanyika Jumapili ambayo kiingilio chake cha chini ni Sh5,000
Mwanaspoti liliandika kwa mara ya kwanza wiki iliyopita kwamba Nkongo ndiye atakayekuwa mwamuzi wa mechi hiyo.
Mwamuzi huyo mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), alipigwa na wachezaji wa Yanga wakiongozwa na Stephano Mwasyika na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika mechi ambayo Azam ilishinda mabao 3-1 wakati timu hizo zilipokutana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Machi 10 mwaka jana.
Lakini kama hiyo haitoshi kwenye mechi ya Jumapili atasaidiwa na msaidizi yule yule, Hamis Changwalu, ambaye alikuwa naye wakati wa sekeseke la Yanga dhidi ya Azam.
Msaidizi mwingine Jumapili atakuwa Ferdinand Chacha wa Bukoba na mwamuzi wa akiba amepangwa kuwa Oden Mbaga wa Dar es Salaam huku Kamishna wa mchezo akiwa John Kiteve kutoka Iringa. Mtathmini wa waamuzi atakuwa Stanley Lugenge wa Njombe.
Msimu uliopita Nkongo alipata balaa jingine baada ya kuondolewa dakika za mwisho kuchezesha mechi ya mwisho ya msimu kati ya Simba na Yanga, Mei 18 mwaka huu na mechi hiyo ikachezeshwa na Martin Sanya wa Morogoro. Yanga ilishinda mabao 2-0.
Kuondolewa kwa Nkongo katika mechi hiyo ya mwishoni mwa msimu uliopita, kulitokana na ushauri wa ofisa usalama wa Fifa kushauri kuwa iwapo angechezesha mwamuzi huyo, Yanga ingeweza kufanya vurugu kutokana na kudai alivuruga mechi yao dhidi ya Azam.
Kuelekea mechi ya Jumapili, kwa mujibu mpangilio wa viingilio uliotolewa na TFF jana Jumatano, mashabiki 19,648 wametengewa viti vya rangi ya kijani kwa kiingilio cha Sh5,000.
Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu, kiingilio ni Sh7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa Sh10,000, VIP C ni Sh15,000, VIP B itakuwa Sh20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tu tiketi moja itauzwa Sh30,000.
TFF imesema tiketi zitaanza kuuzwa Jumamosi katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam; vituo hivyo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, Mgahawa wa Steers uliopo makutano ya Mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.
Katika hatua nyingine, TFF imesema mechi tatu za Ligi Daraja la Kwanza za makundi A na C zimesogezwa mbele kutokana na viwanja vya Kambarage, Shinyanga na Nangwanda Sijaona, Mtwara kuwa na shughuli nyingine za kijamii.


Katika kundi A, mechi kati ya Ndanda na Transit Camp iliyokuwa ichezwe Oktoba 19 mwaka huu sasa itafanyika Oktoba 21 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Stand United na JKT Kanembwa zilizokuwa zicheze Oktoba 19, sasa mechi hiyo ya kundi C itafanyika Novemba 2 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Nayo mechi ya Mwadui na Polisi Dodoma iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo Oktoba 26, imesogezwa hadi Novemba 3.

No comments:

Post a Comment