Lakini, unafahamu anachokiwaza Guardiola? Kocha huyo Mhispaniola anataka siku moja kocha wa timu pinzani atokwe na machozi ya damu. |
MUNICH, UJERUMANI
POINTI 26 kwenye Bundesliga, tisa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ameshinda mechi nane kati ya 10 kwenye Bundesliga, huku akiwa hajapoteza yoyote na kushika usukani wa ligi hiyo ya Ujerumani
.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ameshuka uwanjani mara tatu na kushinda zote kwenye Kundi D lenye timu pia za Manchester City, CSKA Moscow na Viktoria Plzen. Akiwa bingwa mtetezi kwenye michuano hiyo amefikisha pointi tisa, mabao 11 huku akiruhusu bao moja tu kwenye wavu wake. Eti kiwango bado.
Kwenye Bundesliga mechi 10 alizocheza na kuvuna pointi 26, amepoteza pointi nne tu baada ya kutoka sare mbili, amefunga mabao 22 na kuruhusu wavu wake uguswe mara sita. Kwa mashabiki inatosha hasa ukizingatia walitarajia timu yao ishuke kidogo kiwango kwa kuwa wachezaji wake watakuwa wamechoshwa na msimu uliopita baada ya kunyakua mataji matatu.
Lakini, hilo halipo na baada ya kuwa chini ya kocha mpya, Pep Guardiola klabu ya Bayern Munich imekuwa tishio zaidi Ulaya kwa sasa pengine kuliko klabu yoyote.
Achana na manyanyaso waliyoifanyia Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, wakati walipoinyuka timu hiyo jumla ya mabao 7-0 baada ya mechi mbili za hatua ya nusu fainali, Bayern Munich ya Guardiola, isikie hivyo hivyo.
Jose Mourinho na Chelsea yake alikiona cha moto kwenye Super Cup licha ya kiburi chake, kabla ya Manchester City kukumbana na dhahama kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya tena wakiwa nyumbani Etihad. Bayern Munich ni hatari sana.
Lakini, unafahamu anachokiwaza Guardiola? Kocha huyo Mhispaniola anataka siku moja kocha wa timu pinzani atokwe na machozi ya damu.
Ligi ya Mabingwa Ulaya
Bayern Munich mechi yao iliyopita walimkung’uta Viktoria Plzen mabao 5-0 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ilimiliki mchezo huo kwa asilimia 77 kwa maana Plzen walikuwa wanakimbiza vivuli vya wenzao tu ndani ya uwanja.
Walipiga mashuti 18 yaliyolenga lango la Plzen, wakati wapinzani hao hawakupiga hata shuti moja na hakuwa mchezaji yeyote wa Bayern Munich aliyeonyeshwa hata kadi ya njano.
Mabingwa hao wa mataji matatu msimu uliopita, hawajapoteza mechi yoyote msimu huu tangu walipofungwa na Borussia Dortmund kwenye DFB Super Cup
Lakini, unafahamu anachosema Guardiola, timu yake bado haijafikia ubora anaoutaka. Anasema Bayern Munich haijafika pale kwenye ubora anaotaka iwe.
Lakini, si Plzen pekee iliyoteseka kwa Bayern Munich kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu, Manuel Pellegrini na kikosi chake cha Manchester City walinyanyaswa sana nyumbani kwao kwa kupigiwa mpira mkubwa na walichapwa mabao 3-1.
Baada ya kuwachapa Plzen, Guardiola alituma ujumbe kwenye ukurasa wa Twitter wa klabu hiyo: “Tulicheza vizuri, lakini si sahihi. Tunapaswa kuboresha kiwango chetu...”
Kitu gani anataka?
Bayern Munich inacheza soka la kiwango cha juu sana kwa sasa, lakini kocha wake anasema hawajafikia kiwango anacholenga timu hiyo icheze. Guardiola anataka nini? Anataka wapinzani wake waangue vilio uwanjani ndipo afahamu Bayern Munich imefika kwenye ubora anaoutaka?
Kama anaona timu hiyo kiwango chake bado, Mhispaniola huyo anachotaka kuona uwanjani ni makocha wenzake kulia machozi ya damu, kuzimia na hapo atakiri kwamba sasa wamefikia kiwango. Lakini, kufika huko haitakuwa soka tena, yatakuwa manyanyaso.
Kinachomsumbua Guardiola ni kwamba amerithi timu ya kocha Jupp Heynckes, ambayo msimu uliopita alitwaa mataji matatu, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Bundesliga na DFB Pokal, hivyo ili kumfunika mtangulizi wake ni lazima icheze kwa kiwango cha ubora wa juu.
Ferguson atetemeka Wembley
Kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyofanyika Wembley, London mwaka 2011, Barcelona iliyokuwa chini ya Guardiola ilicheza soka la kiwango cha juu sana na kumfanya Kocha Alex Ferguson aliyekuwa akiinoa Manchester United kutetemeka mikono baada ya timu yake kuzidiwa sana ndani ya uwanja.
Guardiola, ambaye ilikuwa fainali yake ya pili dhidi ya Ferguson na zote akiwa amemshinda, kiwango kilichochezwa na kikosi chake cha Barcelona kwenye fainali hiyo ya Wembley kiliifanya Manchester United kuonekana kuwa timu ya chini sana na kufikia hatua ya kocha wao kutetemeka kwa hofu na hasira ya manyanyaso ya timu yake ilichokuwa ikikumbana nacho uwanjani. Sasa Guardiola anataka Bayern ya sasa icheze kuliko Barcelona ya miaka michache iliyopita.
Tatizo lililopo Bayern Munich
Bayern Munich inamiliki wachezaji wa nguvu, lakini kuna eneo moja linalohitaji marekebisho na kumaliza tatizo ili kuifanya timu hiyo kuwa bora zaidi. Uhusiano mzuri ni tatizo kidogo linalosumbua kwenye timu hiyo hasa baada ya tukio la hivi karibuni la Mdachi Arjen Robben kugomewa kupiga penalti kwenye Bundesliga.
Baada ya Guardiola kumtaka Robben asipige penalti hiyo kwenye mechi dhidi ya Mainz 05 na kutaka Thomas Muller apige badala yake, kitendo hicho kilimkasirisha Mholanzi huyo na kususia penalti iliyopatikana kwenye mechi dhidi ya Plzen.
Kocha Guardiola alimtaka Robben apige, lakini yeye alikataa na hivyo Franck Ribery kuchukua jukumu la kupiga mkwaju huo. Hilo ni tatizo ambapo Guardiola anapaswa kulisafisha ili Bayern Munich iwe timu tishio duniani.
No comments:
Post a Comment