Monday, 2 September 2013

ANGOLA KUIWAKILISHA AFRIKA KOMBE LA DUNIA


Mashindano ya mchezo wa kikapu
Wachezaji wa timu ya kikapu ya Angola

Mashindano ya Afrika ya mchezo wa
kikapu yamemalizika mjini Abidjan nchini Ivory Coast.
Timu ya Angola imeendelea kushamiri bila kupoteza kwenye mashindano ya mwaka 2013 ya FIBA kwa Afrika na hivyo kujipatia tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika nchini Uhispania mwakani pamoja na Misri na mshindi wa tatu Senegal.
Angola iliyomaliza ya pili mwaka 2011 iliongoza kundi C kwa kadi safi ya 3-0 kabla ya kupitia mashindano yote bila bughdha ikiitwanga Mali katika duru ya 16 82kwa 36, ikaichapa Morocco kwenye robo fainali 95-73 na mwenyeji wa mashindano haya Ivory Coast ilipoingia nusu fainali 66-59 kujivulia tiketi ya kushiriki fainali.
Misri kwa upande wa pili ilianza kwa kuizaba Tunisia 77-67 kisha kuikwaruza Cape Verde 74-73 na mbele ya Senegal ikashinda 70-63 na hivyo kujishindia fursa ya kupambana na Angola katika fainali ya mashindano haya ya mwaka 2013.
Kwenye fainali iliongoza kwa vikapu 13-12 kufikia robo ya kwanza, lakini Angola ikaziba pengo katika ulinzi na kuwabana wapinzani wake na kunyoa pointi 15 katikati mwa vipindi vya katikati ya mchezo huku wakiopoa vikapu 34. Robo ya nne Misri hawakua na lao ila kuiona Angola ikiwanyooshea mikono na kutamba kwa ushindi wa 57 -40
Mchezaji bora wa mashindano aliyetangazwa ni Carlos Morais wa Angola aliyesaidia katika ushindi wa timu nzima na binafsi kukusanya pointi 15.9.
Pambano la nafasi ya tatu likaiwezesha Senegal kuibwaga Ivory Coast 57-56 ushindi mfinyu uliowaacha mashabiki wa nyumbani wakitokwa machozi.
Hivyo Angola, Misri na Senegal zinajiunga na mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2014 Uhispania, washindi wa medali ya dhahabu KWENYE MICHEZO YA Olimpiki Marekani na wawakilishi wa FIBA bara Asia ambao ni Iran, Philippines na Korea, na vilevile wawakilishi kutoka kanda ya Oceania yaani Australia na New Zealand. Wakati huu wawakilishi wa kanda ya Ameicas anatafutwa kwenye mashindano ya FIBA Americas.

No comments:

Post a Comment