Monday, 28 October 2013

TIMU YA TAIFA YAINGIA KWENYE REKODI AFRIKA




USHINDI wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 ‘Tanzanite Stars’ kwa kuifunga Msumbiji mabao 10-0 juzi Jumamosi umeipa rekodi timu hiyo.
Ushindi huo uimeifanya timu hiyo kuingia katika orodha ya timu zilizoshinda mabao mengi katika mashindano ya kimataifa au ya Bara la Afrika.
Kufuatia matokeo hayo ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, Msumbiji inatakiwa kushinda zaidi ya mabao 10 ili kusonga mbele, jambo ambalo wengi wanachukulia kama linahitaji miujiza.
Wanawake wa Tanzania wanaingia katika rekodi ya miongoni mwa timu zilizovuna mabao mengi katika mashindano ya kimataifa au yale yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Timu ya wanawake ya Tanzania ingeongeza mabao mawili tu ingefikia rekodi iliyowekwa na Pamba ya Mwanza mwaka 1989 kwa kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kushinda mabao mengi katika mashindano ya kimataifa au yale ya Afrika.
Pamba ya Mwanza iliweka rekodi hiyo baada ya kuifunga Anse Boileau ya Shelisheli mabao 12-1 katika mechi ya marudiano ya iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi Afrika iliyochezwa mwaka 1990 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Pia ushindi huo ulikuwa rekodi ya Afrika kwani hadi kufikia mwaka huo hakuna timu ya bara hilo iliyowahi kushinda kwa idadi kubwa ya mabao katika mashindano mbalimbali.
Pamba iliitoa Anse Boileau katika mwaka huo kwani katika mchezo wa kwanza uliochezwa huko Victoria, Shelisheli, timu hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 na kuifanya kusonga mbele kwa mabao 17-1.
Kwa mujibu wa tovuti ya Televisheni ESPN, rekodi ya Pamba ilivunjwa mwaka 1994 na Mbilinga ya Gabon, ambayo iliicharaza Renaissance ya Chad mabao 13-0 katika mechi ya Kombe la Washindi barani Afrika mwaka 1994.
Pia rekodi za shirikisho la kimataifa linalojihusisha na historia na rekodi za soka zinaonyesha kuwa rekodi ya dunia inashikiliwa na Deportivo Arabe Unido ya Panama, iliyowahi kuichakaza Deportivo Jalapa ya Nicaragua 19-0 katika mechi ya Klabu Bingwa ya CONCACAF.
Rekodi za shirikisho hilo la kimataifa zinaonyesha kuwa Ajax Amsterdam ya Uholanzi inashikilia rekodi ya Ulaya baada ya kuiliza Red Boys Differdange ya Luxembourg katika mechi ya kwanza ya UEFA mwaka 1984.
Kwa bara la Oceania, timu ya Central United FC ya New Zealand ndiyo inayoshikilia rekodi baada ya kuilaza Lotoha’pai ya Tonga mabao 16-0 mwaka 1999

No comments:

Post a Comment