Rais mpya wa TFF, Jamal Malinzi (kulia) akiwa na rais aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga mara baada ya Malinzi kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa shirikisho hilo |
UONGOZI mpya na mambo mapya. Rais mpya wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameingia madarakani na kasi mpya ambayo imeungwa mkono na wajumbe wa mkutano mkuu.
Malinzi ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, alimshinda mshindani wake Athuman Nyamlani katika uchaguzi mkuu wa TFF uliofanyika jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita.
Uamuzi mzito alioufanya Malinzi baada ya kutangazwa Rais ni kufuta kamati zote zilizokuwa zimeundwa na Rais aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga kwa muongozo wa Fifa.
Kamati hizo ni ile ya rufaa, kamati ya rufaa ya madili, kamati ya uchaguzi na nyinginezo ambazo zilikuwa zikitoa uamuzi wa masuala mbalimbali ya soka la Tanzania chini ya uongozi wa Tenga.
Malinzi pia ameshitua umma baada ya kutangaza msamaha kwa Michael Wambura na Richard Rukambura waliokuwa wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali na TFF, hivyo kwa sasa wanaruhusiwa kugombea au kuongoza soka popote. Mbali na hao, Malinzi alitangaza msamaha kwa wahanga wote wa soka kuanzia ngazi ya wilaya mpaka Taifa ambao makosa yao hayahusiani na kutoa au kupokea rushwa.
“Tulikuwa vitani na kwenye vita kuna majeruhi, nawapa pole, mimi pia ni miongoni mwa majeruhi wa kamati ambazo zimekuwa zikiwahukumu watu kwa kisingizio cha maadili.
Hata rais mpya wa nchi anapoingia madarakani anatoa msamaha na mimi kama rais mpya wa TFF, natoa msamaha kwa watu wote waliofungiwa kuanzia ngazi za wilaya, mikoa mpaka Taifa,” alisema kiongozi huyo huku akishangiliwa na wajumbe ambao baadaye aliwaongozea posho na siku moja ya kuendelea kula bata Dar es Salaam.
“Kuna waamuzi kama akina Martin Saanya, wamefungiwa mwaka mzima. Ila msamaha huu hauwahusu waliofungiwa kwa masuala ya rushwa, iwe ametoa au kupokea,” alisema.
Saanya alifungiwa na Kamati ya Ligi chini ya Wallace Karia kwa kipindi cha mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuboronga katika mechi ya mzunguko wa kwanza kati ya Yanga na Coastal.
Uamuzi wa Malinzi unarudisha matumaini ya Wambura ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) kabla ya kuwa TFF, ambaye amekuwa mhanga kwenye kamati za TFF baada ya kuenguliwa mara kwa mara kila anapojitosa kuwania ungozi wa soka.
Wambura aliwahi kuenguliwa kwenye uchaguzi wa Simba na baadaye uchaguzi wa Chama cha Soka cha Mara (FAM) kabla ya kuenguliwa kwenye mchakato wa awali wa TFF akiwania Makamu wa Rais.
Hata hivyo mchakato huo ulifutwa baada ya Fifa kuingilia kati na kugundua dosari na kuagiza ziundwe kamati za maadili na kamati za rufaa za maadili ambazo zingetoa hukumu kwa Wambura na wengineo ili ijulikane wameadhibiwa kwa muda gani.
Awali Malinzi pia alienguliwa katika mchakato wa uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari mwaka huu kabla ya uchaguzi kurudiwa kwa maelekezo ya Fifa na ndipo alipoibuka na ushindi wa kishindo.
Kwa upande wake, Wambura hakujitosa tena kuwania uongozi ndani ya shirikisho hilo kwa kile alichoeleza kuwa hawezi kujikosha kwa maji taka.
Hata hivyo habari zinadai kwamba Wambura hakutaka kujitosa kuwania uongozi kwa hofu ya kupewa adhabu kali ambayo pengine ingeweza kumpoteza katika medani ya soka.
Mbali na Wambura, Richard Rukambura naye ni muhanga baada ya kufungiwa miaka 30 kwa kosa la kufungua kesi mahakamani kupinga kuenguliwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa awali. Pia wapo baadhi ya waamuzi ambao wamefungiwa kwa sababu mbali mbali.
“Kwa mujibu wa katiba ya TFF, kifungo cha 44 (7) na 39 (7)
uongozi uliopita na kamati zake zote zimemaliza muda wake tangu Desemba 13 mwaka jana, zipo kamati mpya ambazo zimeundwa juzi juzi, kuna kamati za kudumu na kamati ndogo ndogo za kisheria kama Rais mpya naomba kibali cha mkutano mkuu kwa sababu maamuzi yote yaliyoamuliwa na mkutano mkuu ni halali,
naombeni kibali chenu nivunje kamati zote niunde kamati mpya,” alimalizia huku wajumbe wakijibu kwa kishindo; “Umepata baba, sawa sawa vunja kabisa ruksa.”
Baada ya kauli hiyo Malinzi aliwafurahisha zaidi wajumbe hao wa mkutano mkuu kwa kuwambia:
“Mlitakiwa muondoke leo (Jumatatu) lakini mimi kama Rais mpya, naigiza sekretarieti ya TFF iwalipe posho ya siku moja zaidi na kulala hotelini kwa siku moja zaidi badala ya kuondoka Jumatatu mtaondoka Jumanne (leo),”alisema Malinzi na kuzidi kushangiliwa kwa nguvu zote na wajumbe wa mkutano mkuu waliokuwa wakipiga makofi na meza.
Wajumbe hao walilipuka zaidi kwa nderemo pale Malinzialiposema: “Viongozi wa mikoani, jiandaeni kupokea ugeni wa kamati ya utendaji ya TFF, sasa vikao vitakuwa vinafanyika kwa mzunguko kila mkoa na si kama ilivyozoeleka vikifanyika Dar es Salaam pekee.”
No comments:
Post a Comment