Monday, 28 October 2013

FIESTA KERO TUPU


TOFAUTI na matarajio ya mashabiki wengi wa sanaa ya muziki, Tamasha maarufu la Fiesta lililofikia fainali zake juzi Jumamosi Jiji Dar es Salaam lilishindwa kubamba baada ya shoo hiyo kudoda kutokana na kukumbwa na dosari nyingi.
Fiesta ambalo ni tamasha la kila mwaka linaloandaliwa na Kituo cha Televisheni na Radio cha Clouds , lilifanyika Jumamosi likishirikisha wasanii wa ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo tamasha la juzi liliambatana na changamoto za hapa na pale na iliyoonekana dhahiri ni kufungwa vibaya kwa mitambo na kuwa sababu ya sauti kujirudiarudia (mfano wa Mwangwi) na hivyo kuwa kero kwa mashabiki kwani burudani iliyotarajiwa ilikosekana.
Tukio hilo liliwafanya wasanii kuimba chini ya kiwango na baadhi yao wakiimba pembeni huku msanii God Zilla akiamua kulalamika mbele ya mashabiki ambao walikuwa wakitukana na kupiga kelele za kukerwa mara kadhaa.
Wasanii waliokwepa jukwaa hilo ni Juma Nature, Dully, Young Dee, Young Killer, Mr Blue, Ommy Dimpoz na wengineo huku wasanii wa kike wakiimba kwa kujilazimisha.
Hali ilikuwa tofauti kwa Peter Msechu na Christian Bella ambao walifanya vizuri katika jukwaa hilo kwa kuwa walitumia bendi.
“Nashukuru mashabiki kwa kuniunga mkono ila tatizo ni Mwangwi ndiyo maana sauti ilikuwa inajirudia rudia,” alisema Zilla katika malalamiko yake.
Mmmoja wa waratibu ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake alisema kwamba ni tatizo la ghafla ambalo hawakulitarajia.
Wakati mratibu huyo akitoa kauli hiyo, mratibu mwingine, Arnold Kayanda yeye alikataa kuzungumza lolote juu ya tatizo hilo.
“Bado sijapata taarifa zozote kwa mafundi mitambo ili kujua kwa undani tatizo lilikuwa nini, hivyo siwezi kulisemea,” alisema.
Hata hivyo msemaji wa tamasha hilo, Sebastian Maganga alikiri udhaifu huo na kuahidi kutoa ufafanuzi baadaye.
“Unaniuliza kwa ajili ya habari au....,kama ni hivyo basi usiandike kwanza ndio tuko katika mazungumzo, tuko kwenye vikao, tafadhali usiandike,” alisema ingawa hakupatikana baadaye jana Jumapili kutoa ufafanuzi zaidi wa nini kilichojadiliwa katika kikao hicho. Shoo hiyo ilirudiwa jana Jumapili ambapo wasanii ambao hawakupanda Jumamosi walipanda jana.
Tatizo la umeme
Majira ya saa 10 za alfajiri wakati wasanii wengine wakubwa wakisubiriwa kupanda jukwaani, umeme ulikatika ghafla jambo lililowakera mashabiki waliokuwa katika tamasha hilo.
Akizungumzia hilo, Kayanda alikiri umeme kukwamisha mambo ingawa walijaribu kutatua tatizo hilo bila mafanikio na hivyo kuahidi kuwapa mashabiki shoo ya bure kama njia mojawapo ya kuwapoza.
Wadau waponda
Wadau wa sanaa na mashabiki waliozungumza na gazeti hili walionekana kutofurahishwa na shoo hiyo iliyojipatia umaarufu nchini.
“Huu ni uzembe kama tatizo ni mitambo maana yake ni kwamba hawakujipanga, mara umeme ukatike na wasanii wanaruka ruka tu jukwaani,” alisema shabiki mmoja huku akionyesha kustaajabishwa pia na vitendo vya uhalifu vilivyokuwa vikiendelea eneo hilo.
Walisema tamasha la mwaka huu limetia aibu huku akisisitiza kwamba kasoro zilizojitokeza zinatakiwa kufanyiwa kazi ili kurejesha imani kwa mashabiki wa Fiesta.
“Kila kitu kimeonekana kwa macho, hatuja ‘enjoy’ lolote kwa wasanii jukwaani, kila msanii anashindwa kukaa jukwaani,” alisema Vainess.

No comments:

Post a Comment