Monday, 21 October 2013

MBWEMBWE ZA MRISHO NA ADABU YA MPIRA


UNATAKA kujua kwa nini Afrika haijachukua Kombe la Dunia mpaka sasa? Basi dakika ya 40 ya kipindi cha kwanza jana Jumapili ingekudhihirishia.
Usichukue mifano mingi isiyo na maana, jikumbushe alichokuwa anafanya Mrisho Ngassa katika Uwanja wa Taifa. Wakati Yanga ikiongoza kwa mabao mawili, katika upande wa Mashariki, Ngassa alikuwa anapiga magoti kupokea mipira. Akinyanyuka anasimama juu ya mpira. Hakutofautiana sana na Haruna Niyonzima.
Kisa? Yanga ilikuwa inaongoza mabao mawili. Yanga wakapoteza nidhamu. Mechi ilikuwa yao kwa sababu ya kikosi chao kukaa muda mrefu, kuweza kujiamini mapema, lakini pia kwa jinsi Kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni alivyochemsha katika upangaji wa kikosi cha kwanza.
Katika safu ya kiungo aliwapanga Jonas Mkude na Abdulhalim Humoud. Pembeni akawapanga Ramadhan Singano na Haruna Chanongo, huku mbele akiwapanga Betram Mwombeki na Amis Tambwe.
Hii ilikuwa na maana Simba haikucheza na kiungo yeyote mshambuliaji. Humoud na Mkude hawakuweza kutengeneza mashambulizi kabisa.
Yanga wakajaa katikati kwa sababu walikuwepo Athuman Idd, Frank Domayo na Niyonzima. Wakakata waya wa mawasiliano kabisa hasa ukizingatia Chanongo na Messi walikuwa wachanga katika mechi. Mwombeki na Tambwe wakakosa msaada.
Yanga walijaa kati na walipoanza kufunga mashambulizi wakajichanua kushambulia pembeni ambapo Simba walikuwa wamezubaa. Na mpira ungerudi eneo la katikati, Gilbert Kaze na Joseph Owino nao hawana maelewano ya kutosha.
Mabao yote matatu ya Yanga yalifungwa katika eneo la sita la Simba. La kwanza, alifunga mchezaji wa pili kwa ufupi uwanjani baada ya Messi, Ngassa aliyeunganisha mpira wa juu wa krosi ya Hamis Kiiza.
Bao la pili la Simba lilikuwa fedheha zaidi. Mpira ulirushwa na Mbuyu Twite, Didier Kavumbagu akaugusa, Kiiza akamalizia. Ni bao la aina ileile aliyofungwa Juma Kaseja na Kiiza katika pambano la mzunguko wa pili msimu uliopita na watu wakaanza kuhisi Kaseja amehujumu.
Bao la tatu lilikuwa vilevile lakini la chini. Kavumbagu alimpasia Kiiza ndani ya eneo la hatua la sita la Simba. Ukabaji wa Simba ulikuwa duni kama kawaida. Uwezo wa walinzi wao wa kati kukaba kwa pamoja (double marking) ukawa duni tena, hasa katika eneo lao la hatari.
Inavyoelekea kipindi cha pili, wachezaji wa Yanga na kocha wao walianza kupiga simu kwa wapenzi wao kueleza jinsi watakavyosheherekea ushindi mwishoni mwa mchezoni. Ilionekana wazi kwamba Simba isingerudi mchezoni na mabao matano waliyopigwa miaka miwili iliyopita yangerudi.


Yanga walionekana kuidharau Simba. Hawakuwa makini tena na mchezo kama ilivyo tabia ya wachezaji wengi wa Kiafrika. Ningekuwa Kocha wa Yanga, Ernie Brandts kwanza ningepoza mashambulizi na kuwasubiri Simba katika mashambulizi ya kushtukiza kwa sababu ni wazi Simba wangekuja kwa kasi.
Na ndicho walichofanya Simba. Kitendo cha kumtoa Humoud na kumuingiza William Lucien ‘Gallas’ kwa kiasi kikubwa kiliwaibua Simba. Gallas alikuwa na uwezo wa kukaba na kuipandisha Simba mbele kwa haraka, kitu ambacho Humoud na Mkude walikikosa katika kipindi cha kwanza.
Kadri Simba walivyosogea mbele, ndivyo Yanga walivyokosa nidhamu ya mchezo. Katikati ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondani kulikuwa na pengo kubwa dhidi ya viungo wao. Ni katika shimo hilo ndipo Simba walipatumia vizuri.
Jaribu kufikiri. Uzembe wa bao la kwanza ulisababisha Cannavaro aanguke peke yake na Tambwe. Mwombeki akamalizia kiulaini. Alikuwa wapi Yondani?
Yeye ndiye aliyepiga pasi ya ovyo ndani lakini badala ya kuwahi kumsaidia Cannavaro yeye akasimama. Mwombeki akafunga mithili ya penalti. Alikuwa wapi Chuji? Kiungo mkabaji alikuwa amesafiri ingawa alikuwa ndani ya uwanja.
Mabao mawili yaliyofuata ya Simba yalikuwa ya aibu. Tofauti pekee na mabao mawili ya Yanga katika kipindi cha kwanza ni kwamba yale ya Yanga yalifungwa chini, Simba wakafunga kwa kichwa.
Ndani ya eneo la sita, kwa nyakati tofauti, walinzi wawili wa kati, Joseph Owino na Gilbert Kaze waliruka pekee yao na kufunga wakiwa huru (free header). Sielewi Brandts aliwaambia wachezaji wake wakabe kwa staili gani, mtu na mtu (man to man marking) au kukaba nafasi (zonal marking).
Kwa chochote alichowaambia hakuna hata mchezaji mmoja aliyefuata maelekezo. Zaidi ni kwamba ilionekana wazi kuwa pumzi za wachezaji wake zilikuwa zimefika mwisho katika kusaka bao la nne. Simba walionekana wamefunguka zaidi na zaidi.
Mwishowe, Simba walifungwa mabao matatu katika kipindi cha kwanza kwa sababu moja kubwa ya ukosefu wa kujiamini. Maandalizi ya mechi yalionyeshwa watafungwa. Yanga walipouanza mpira kwa kasi na pasi za mbwembwe Simba wakazidi kuamini kuwa watafungwa.
Ngassa alipofunga bao la kwanza wakazidi kuamini katika kufungwa. Likaja la pili halafu la tatu. Tofauti kwa Yanga, kilichosababisha wafungwe mabao matatu kipindi cha pili ni kujiamini kulikopitiliza bila ya kujua kwamba watu wa Simba walivamia chumba cha kubadilishia nguo cha wachezaji wao wakati wa mapumziko kuinua morali ya timu yao.
Wakati Ngassa na Niyonzima wakiwaza jinsi watakavyokuwa wanapokea pasi kwa tumbo na makalio, Simba walikuwa wanahitaji bao moja tu kurudi mchezoni na kurudisha imani. Na kweli wakalipata bao hilo kupitia kwa Mwombeki.
Wakati Simba wakishangilia bao la tatu, Jerry Tegete aliyekuwa benchi alikuwa anamfokea Yondani. Shauri zao, sijui watapata lini tena nafasi kurudisha bao sita za Abdallah Kibadeni za mwaka 1977 au bao tano za mwaka juzi za Emmanuel Okwi. Hii ilikuwa nafasi ya dhahabu!

No comments:

Post a Comment