Sunday, 20 October 2013

LUKAKU;CHELSEA IMETOA MKOPO GARI LA MAGOLI

Mshambuliaji wa Eveton,Romeo Lukaku

WAKATI washambuliaji wa kocha, Jose Mourinho, katika klabu ya Chelsea wakiwa wamekaukiwa mabao, inashangaza kuona kocha huyo amemtoa kwa mkopo staa wake wa Ubelgiji, Romelu Lukaku, ambaye anafunga kadri anavyojisikia katika klabu ya Everton.
Pia Lukaku ameipeleka Ubelgiji katika fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil. Ni nani huyu Lukaku.
Azaliwa Ubelgiji, baba yake mwanasoka Congo
Lukaku alizaliwa katika Jiji la Antwerp, Kaskazini mwa Ubelgiji huku baba yake akiwa ni Roger Lukaku ambaye ni staa wa zamani timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Mdogo wake, Jordan yupo katika timu ya vijana ya Anderlecht ambayo Lukaku alipitia.
Lukaku alianza kucheza soka katika umri wa miaka mitano katika klabu ya Rupel Boom kabla ya kuonwa na maskauti wa klabu ya Lierse SK.
Aliichezea kuanzia mwaka 2004 hadi 2006 akifunga mabao 121 katika mechi 68. Baadaye akajiunga na timu ya vijana ya Anderlecht, akiifungia mabao 131 katika mechi 93.
Atua Anderlecht, Chelsea yamwona
Lukaku alisaini mkataba wa kulipwa na Anderlecht mnamo Mei 13, 2009 akiwa na umri wa miaka 16 na siku 11 baadaye aliichezea timu hiyo katika mechi dhidi ya Standard Liège. Kuanzia wakati huo, maskauti wa Chelsea walikuwa wakimfukuzia kwa kasi.
Amfuata shujaa wake Didier Drogba
Agosti 2011, Lukaku alijiunga na Chelsea kwa ada ya Pauni 12 Milioni ambayo ingeongezeka mpaka kufikia Pauni 17 Milioni kutokana na kiwango chake.
Alipewa jezi namba 18 na kwa kufanya hivyo alikuwa ametimiza ndoto zake za kukipiga na mshambuliaji Didier Drogba ambaye anamtaja kama shujaa wake wa maisha ya soka.
 Mechi yake ya kwanza alicheza dhidi ya Norwich akiingia uwanjani kuchukua nafasi ya Fernando Torres.
Akataa kushika Kombe la Ulaya
Siku za awali maisha ya Lukaku yalikuwa magumu kiasi cha kuishia kucheza mechi nyingi za wachezaji wa akiba.
Mei 13, 2013 wakati ligi ikielekea mwishoni, alionyesha kiwango cha juu katika pambano dhidi ya Blackburn Rovers huku akipika bao la kwanza la John Terry.
Mei 19, 2012 wakati Chelsea ikitwaa ubingwa wa Ulaya dhidi ya Bayern Munich, Lukaku alikataa kuligusa kombe hilo kwa madai kwamba hakujiona kama mshindi kwa vile hakufanya juhudi zozote za kulitwaa zaidi ya kuishia benchi.
Apelekwa kwa mkopo West Bromwich
Agosti 10, 2012, Lukaku alijiunga an West Brom kwa mkopo kisha akafunga bao siku nane baadaye katika ushindi wa 3–0 dhidi ya Liverpool. Akafunga tena bao la ushindi dhidi ya Reading mechi ya nyumbani.
Novemba 24 akafunga bao dhidi ya Sunderland na kupiga jingine la Marc-Antoine Fortune. Januari 2013 akafunga mabao mawili dhidi ya Reading katika kichapo cha 3–2.
Februari 10 akafunga bao lake la 10 la msimu dhidi ya Liverpool. Februari 23 akafunga mabao yote mawili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Sunderland. Akafunga jingine dhidi ya Swansea City baada ya kipa wa timu hiyo kuokoa penalti na mpira kumrudia Lukaku.
Amuaga Ferguson kwa Hat trick
Mei 19, 2013 ikiwa ni mechi ya mwisho ya Sir Alex Ferguson katika soka, Lukaku alipiga hat trick katika sare ya 5-5 dhidi ya Manchester United.
Mechi hii iliweka rekodi ya kuwa sare yenye mabao mengi katika historia ya Ligi Kuu England. Licha ya kutolewa kwa mkopo, Lukaku aliwafunika wachezaji wenzake wote wa Chelsea kwa kufunga mabao huku akiibuka mchezaji wa sita kufunga mabao mengi msimu wa 2012–13 akiwa na mabao 1
Mwanzoni mwa msimu huu, Lukaku alipania kuichezea Chelsea na kuonyesha makali yake. Hata hivyo aliuanza msimu kwa nuksi baada ya kukosa penalti katika pambano la Supercup dhidi ya Bayern Munich.
Katika siku ya mwisho ya dirisha la uhamisho alijiunga na Everton kwa mkopo. Alicheza mechi yake ya kwanza dhidi ya West Ham Septemba 21 na kufunga kwa kichwa katika ushindi wa 3-2.
Siku tisa baadaye akafunga mabao mawili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Newcastle na kupika lingine la Ross Barkley. Katika kichapo cha 3-1 dhidi ya Manchester City, Lukaku pia alifunga bao la kufutia machozi.
Aipeleka Ubelgiji Brazil mwakani
Lukaku aliitosa timu ya taifa ya Congo ambayo angeweza kuichezea kama baba yake Roger alivyoichezea, badala yake akaamua kuichezea Ubelgiji.
Aliichezea Ubelgiji mechi ya kwanza Februari 2010 dhidi ya Croatia. Mabao yake mawili ya kwanza yalikuwa dhidi ya Russia Novemba 17, 2010
Akafunga tena katika ushindi wa 4-2 dhidi ya Uholanzi Agosti 15, 2012. Wiki iliyopita, Lukaku alifunga mabao mawili ya Ubelgiji dhidi ya Croatia ambayo yaliipeleka timu hiyo katika kombe la dunia.
Anaongea lugha sita
Lukaku anaongea lugha sita ambazo ni Kifaransa, Kidachi, Kihispaniola, Kireno, Kiingereza na Kijerumani. Aliwahi kuwaambia wazazi wake kuwa asingependa kuhamia Chelsea kabla ya kuchukua shahada yake chuo kikuu.

No comments:

Post a Comment