Alikuwa kocha wa Man U,Sir Alex Ferguson |
KABLA haujakata roho, kuna vitu 50 vya michezo ambavyo unapaswa kuvifanya. Aprili 2004, Gazeti la Observer la Uingereza liliandika kuwa tukio la kwanza kati ya matukio hayo ni kutazama pambano la SuperClasico. Unalifahamu pambano hili?
Achana na uchafu wa Barcelona na Real Madrid unaoitwa El Clasico, baba wa Clasico zote duniani ni SuperClasico wakati Boca Juniors na River Plates zinapocheza Uwanja wa La Bambonera jijini Buenos Aries, Argentina.
Ni pambano la machozi, jasho na damu. Ni uwanja wa vita. Ndiyo maana, katika miaka yake yote 26 akiwa katika benchi la Manchester United, Sir Alex Ferguson alikuwa na ndoto moja tu kubwa, kutazama pambano la Superclassico jijini Buenos Aires.
Si pambano la Superclassico tu, Sir Alex anaendelea kutimiza ndoto zake nyingi wakati huu akila pensheni yake. Anataka kwenda kutazama mbio za farasi Melbourne, Australia. Anataka kutazama tenisi Marekani katika Michuano ya US Open.
Kwa nini asifanye hivyo? Pesa inaruhusu. Anaweza asiguse mishahara yake yote aliyokusanya Manchester United kwa miaka 26 iliyopita, lakini bado akajikuta mtu tajiri zaidi miongoni mwa wazee wa Kiingereza tena kwa utajiri anaouvuna baada ya kustaafu kufundisha soka.
Hata baada ya miaka 26 ya kuvuna mshahara wake Manchester United, nimegundua ndiyo kwanza pesa inazidi kutiririka kwa Sir Alex Ferguson. Pesa inakwenda katika mkondo wa pesa.
Licha ya kustaafu kwake, kila anapoamka Sir Alex anaingiza pesa zaidi. Kila anachogusa anaingiza pesa zaidi. Kwa sasa, kila sehemu ambayo Sir Alex anaitwa kama mzungumzaji wa mada mbalimbali zinazohusu soka au maisha yake ya soka, anapokea kiasi cha Dola 100,000. Ina maana akizungumza katika sehemu tano tu anaingiza Dola 500,000, ambazo zinatosha kuipa udhamini ligi fulani ya ukanda wa SADC (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika).
Ni watu mashuhuri wachache wanaoweza kupokea kiasi hicho kwa kuzungumza tu. Barrack Obama anaweza kupokea baadaye akistaafu, lakini kwa sasa inasemekana Bill Clinton na mkewe, Hilary Clinton wanapokea kiasi hicho.
Manchester United wamemchagua kama balozi wao katika shughuli zao mbalimbali duniani. Unajua wanamlipa kiasi gani? Pauni 2 milioni kwa mwaka. Unadhani anafanya kazi hiyo kwa siku 364? Hapana. Anafanya kazi hizo kwa siku 20 kati ya siku 364.
Kwa wakati huu anajiandaa kutoa kitabu cha maisha yake. Hapana shaka moja kwa moja kitakwenda kuwa kitabu kinachoongoza kwa mauzo Uingereza.
Atazungumza jinsi alivyompiga kiatu David Beckham, atazungumza alivyomsajili Cristiano Ronaldo, atazungumza jinsi alivyokwenda kumtoa selo Roy Keane siku mbili kabla ya pambano la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Unajua nini? Kabla ya kuuza aliamua kufanya promosheni ya kitabu chake kwa kuzunguka kumbi mbalimbali kuongea maneno machache kabla ya kuonyesha kitabu chake kitakavyokuwa.
Ndani ya saa chache tangu ratiba itangazwe, tayari tiketi zote zilikuwa zimeisha katika miji mbalimbali ya Uingereza. Kuanzia Salford, Glasgow, London, Aberdeen, Dublin, Preston na kwingineko tiketi zilikuwa zimekwisha.
Watu wanataka kuona sura yake. Wanataka kusikia sauti yake kwa karibu. Lakini kwa kufanya hivi, kila tiketi moja ilikuwa inauzwa Pauni 40. Anatengeneza pesa!
Wakati David Moyes akiteseka na vipigo vitatu vya Ligi Kuu katika mechi saba tu, Sir Alex Kila anachozungumza kwa sasa ni pesa. Kila anachoandika ni pesa na kila anachogusa ni pesa.
Mtu yeyote atakayemgusa Sir Alex kwa ajili ya kuchambua mechi za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil nadhani atalazimika kumlipa zaidi ya Pauni 1 milioni. Kwa mara ya kwanza anapatikana akiwa hana kazi, na wala hajiandai kwa maandalizi ya mechi za msimu mpya.
Bao la mwisho ambalo Sir Alex atapiga ni kuanza kuuza mali zake za kumbukumbu. Unajua atauza kiasi gani koti lake alilochukua nalo ubingwa wa Ulaya mwaka 1999 wakati Ted Sheringham na Ole Gunnar Solskajaer wakifunga mabao ya dakika za mwisho Nou Camp? Bei yake itaanzia Pauni 500,000.
Unajua atauza kiasi gani viatu alivyovaa wakati Manchester United ikiichapa Arsenal 8-2 katika Uwanja wa Old Trafford? Unajua atauza kiasi gani kitabu chake cha kuandika takwimu za mechi katika pambano lake la kwanza katika maisha yake ya soka Manchester United dhidi ya Oxford?
Hivi ndivyo Sir Alex anavyotiririsha pesa. Wakati fulani unakaa chini na kuwaza jinsi ambavyo maisha hayatendi haki sana.
Wakati babu fulani mstaafu kijijini kwetu Namasakata Tunduru akisumbuka na jembe, Sir Alex anacheza gofu New York na pesa bado inaingia.
No comments:
Post a Comment